Hayo yamesemwa na Mdhibiti wa zao hilo wa Bodi ya Pareto nchini, Edwin Margwe katika maonyesho ya Nanenane kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale vilivyopo jijini Mbeya.
Amesema uhitaji wa zao hilo hivi sasa ni mkubwa sana,hivyo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kupanua wigo wa soko hapa nchini na nje ya nchi kwa kulima zao hilo kwa wingi.
Amefafanua zaidi ya kuwa awali ilikuwa kampuni moja ambayo inanunua zao hilo,lakini hivi sasa kampuni zimeongezeka na uhitaji umeongezeka ndio maana wanahimiza wakulima kulima zao hilo kwa wingi.

"Naomba wakulima wa zao hili muongeze jitihada kuhakikisha mnalima zao hilo kwa wingi ili muweze kujiinua kiuchumi,"amesema Margwe.
Amefafanua zaidi, wakizalisha kwa wingi watasaidia utoshelezi wa uhitaji wa zao hilo hapa nchini.
Akizungumzia suala la mbegu, amesema wanashirikiana pamoja na taasisi ya utafiti wa kilimo nchini ili kuhakikisha wanapata mbegu bora kwa ajili ya wakulima kwenda kupanda katika maeneo mbalimbali.
Aidha amewataka vijana kujikita katika kilimo hicho kwa sababu hivi sasa kina soko kubwa kutokana na kuwa na mnyororo wa thamani wa matumizi ya zao hilo mashambani na majumbani.
Naye mratibu wa zao la Pareto Michael Bishubo kutoka Kampuni ya PCT, amesema moja ya faida ya viuatilifu ni kwa ajili kusaidia kukabiliana na wadudu waharibifu wa shambani na majumbani.
Akielezea namna ya pareto inavyotumika kama viuatilifu amesema,inapopandwa shambani maua yake ndio yanavunwa na kilichomo ndani ya maua ni kiuatilifu maua ambacho kinaenda kuchujwa na kutumika kama dawa ya kwenda kuua wadudu shambani.










