JKT yajisifu mafanikio katika kilimo ni kutumia taarifa za TMA

08Aug 2022
Renatha Msungu
MBEYA
Nipashe
JKT yajisifu mafanikio katika kilimo ni kutumia taarifa za TMA

JESHI la Kujenga Taifa JKT limesema siri kubwa ya mafanikio katika kilimo ndani ya jeshi hilo,imetokana na kutumia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kabla ya kuanza msimu wa kupanda.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT na Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo mkakati wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Hassan Mabena wakati akitembelea maonyesho ya kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale vilivyopo jijini Mbeya.

Brigedia Jenerali Mabena amesema mara baada ya kupata taarifa za TMA wamekuwa wakikutana na wataalam wa kilimo jeshini humo kuona namna ya kuanza taratibu za kupanda aina za Mbegu za mazao mbalimbali hapa nchini.

Amesema kutokana na kufanya hivyo,wamefanikiwa kupata mazao mengi katika mashamba ya vikosi vya jeshi ambavyo hulima mazao ya chakula na biashara.

Brigedia Jenerali Mabena amesema wamefanikiwa kupata mazao mengi kutokana na kuwa na utaratibu wa kuwasiliana na TMA ili kujua mabadiliko ya tabia nchi yakoje.

Akizungumzia kuhusiana na ushiriki wa maonyesho ya nane kitaifa amewataka wananchi kuzidi kujitokeza katika shamba darasa la jeshi hilo ili kuona namna ya kujifunza kilimo cha kutumia teknolojia ili kustawisha mazao.

Amesema shamba hilo lina kila aina ya mazao ambapo jamii inaweza kujifunza kupitia hilo kutokana na kupandwa kitaalam.

Kuhusu suala la Sensa aliwataka wananchi kujitokeza kushiriki ili waweze kuhesabiwa ili kusaidia taifa kuwa na idadi kamili ya watu katika kila eneo.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya maonyesho ya Nanenane kitaifa Kanali Lupi amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linazidi kupiga hatua kwenye sekta ya kilimo hasa ukizingatia wanapembejeo zote.

Kanali Shija Lupi amesema lengo lao ni kuona wakulima wanaiga mfano wa kuendesha kilimo cha kisasa chenye kuleta tija kwao na taifa kwa ujumla.