Samaki hatarini kutoweka 

29Feb 2024
Restuta Damian
BUKOBA
Nipashe
Samaki hatarini kutoweka 

​​​​​​​VIUMBE hai wakiwemo samaki wapo hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kilimo zinazoendelea kuharibu vyanzo vya maji mkoani Kagera.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Bonde la Ziwa Victoria Kanda ya Kagera, Revodius Bishanda wakati akizungumza na Nipashe juu ya athari za kimazingira zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu zinazoendelea kwenye vyanzo hivyo.

Bishanda amekitaja kilimo kuwa kinara katika uharibifu wa ikolojia ya viumbe hai wa majini na kusababisha kupotea kwa baadhi ya mazalia yake.

“Hii inatokana na kutifua udogo kwenye eneo la vyanzo hali inayoweza kusababisha eneo husika kujaa udongo na kupoteza asili yake ya maji hali inayosababisha maji kusambaa mahali ambako haikustahili na viumbe hai wanaotegemea maji hayo kukosa uhai,” amesema Bishanda.

Amesema mkulima anawaza kupata faida na sio athari ya kusababisha chanzo cha maji kukauka na kuathiri viumbe wengine endapo eneo likikimbwa  na ukame.

"Kina cha maji kikipungua kwa kusababishwa na binadamu aliyeona uzalishaji ni muhimu kuliko uhai wa wengine matokeo ya haraka utaanza kuona mabadliko ya tabia ya nchi kama ukame,” amesema.

Amewataka wakulima kuacha kufanya shughuli za kilimo kando ya chanzo chochote cha maji kwani ni kinyume cha sheria na kuonya kuwa atakayebainika sheria kali zitachukuliwa dhidi yake.

Mkazi wa Kata Bakoba Manispaa ya Bukoba, Sauli Thomas, amesema amekuwa akifanya shughuli za kilimo kando ya mto kwa miaka saba kwa ajili ya kujipatia kipato bila kufahamu athari zake kwa mazingira na viumbe hai..

“Kwa sasa nimepisha eneo hilo baada ya kutembelewa na viongozi wa mtaa na kunipa maelekezo kuwa natakiwa kuondoa mazao yangu ili kulinda chanzo cha maji kiwe salama,” amesema Thomas.