Mkulima alia na ukame, aomba msaada wizarani

13Sep 2023
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Mkulima alia na ukame, aomba msaada wizarani

MKULIMA wa Kijiji cha Lyagiti, Kata ya Lyabukande, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Shauri Mbelele, ameomba kuwezeshwa kuchimba mabwawa ya maji ili kuendesha kilimo chake.

Akizungumza na Nipashe kijijini humo, Mbelele alisema kazi yake kubwa ni kilimo, hivyo anaomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kumwezesha kwa kumchimbia mabwawa ya umwagiliaji ili aendeshe kilimo chenye tija.

Alibainisha kuwa kwa sasa ana shamba lenye ukubwa wa ekari 40 za mahindi yaliyo katika hatua ya kukomaa, lakini yameanza kukauka kutokana na kukosa mvua ya kutosha.

Mkulima huyo aliomba Wizara ya Kilimo kupitia wataalamu wake kutembelea kijiji hicho kujionea kilimo chake kilivyoathirika kutokana na ukame baada ya mabwawa aliyochimba kukauka.

Akisema kuchimbwa kitaalamu kwa mabwawa hayo kutakuwa msaada mkubwa kwa wanakijiji wote na kutoa fursa ya kuendesha kilimo pasi na kutegemea mvua.

Mkazi wa Kijiji hicho, Haruna Misamitana, alisema ni miongoni mwa vijana wengi waliohitimu masomo yao vyuoni, lakini hawana ajira rasmi, hivyo wakaamua kujikita katika kilimo.

Aliomba serikali kwa kushirikiana na asasi zinazotoa elimu ya kilimo kwa vijana, wasaidie kwa kuwachimbia kitalaamu mabwawa ya maji yatakayokuwa yanatunza maji ili walime kwa tija.

Ofisa Kilimo Manispaa ya Kahama, Richard Hegera, alisema wamekuwa wakitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo na kuwagawia vijana bure.

Masharti ni wanufaika kuwa na uwezo wa kulima walau ekari tano na mazao wanayopata ni mali yao na si ya halmashauri.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuondoa wimbi la vijana wanaoshinda mitaani wakicheza michezo ya kubahatisha.

Ofisa huyo alisema wamekuwa wanawafikia mashambani na kuwashauri namna ya kulima kisasa na kuyatumia mabwawa yaliyoko katika kilimo cha umwagiliaji.

Hegera alisema kuwa kati ya kata 20 zilizoko Manispaa ya Kahama, ni kata 11 pekee za pembezoni ambazo wananchi wanajihusisha na kilimo cha chakula na biashara.

Alisema wamewawezesha maofisa ugani vyombo vya usafiri ili wawafikie wakulima na kuwashauri kulima kisasa kulingana na jiogorafia ya ardhi ya kila mkulima.