‘Vijana acheni kulalamika, ajira ziko shambani, zizini’

13Sep 2023
Peter Mkwavila
BAHI
Nipashe
‘Vijana acheni kulalamika, ajira ziko shambani, zizini’

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, amewataka vijana kuwekeza katika kilimo, uvuvi na ufugaji ili wajiajiri wenyewe na kuajiri wenzao badala ya kuendelea kuinyooshea vidole serikali kwa kukosa ajira.

Justen Sangulah alitoa rai hiyo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Vijana.

Alisema kuwa badala ya kusubiri serikali itoe ajira, vijana wanatakiwa kujikita katika kilimo, uvuvi na ufugaji ambao utawawezesha kujiajiri wenyewe na kuajiri vijana wenzao.

“Wilaya yetu ya Bahi ina sifa ya kuwapo sekta mbalimbali ambazo zinazoweza kubadilisha vijana kimaendeleo na kiuchumi. Hivyo, ninawaomba badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini ni vyema wakajikita katika fursa hizo ambazo zitawabadilisha maisha yao,” alisema.

Sangulah pia aliwataka vijana wa wilaya hiyo kuiunga mkono serikali kwa juhudi zinazofanywa katika kuliletea Taifa maendeleo, pia kukataa kutumiwa na watu wasiotakia mema nchi kwa lengo la kuharibu amani.

Akifungua kikao cha baraza hilo, Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo, aliwataka kuungana kuanzisha vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali.

Alisema serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iko tayari kuwasimamia kwenye vikundi ambavyo vitaanzishwa kwa ajili ya kuhakikisha wanapata mikopo ambayo itabadilisha mitizamo ya maisha yao.

Pia aliwataka vijana hao kuhakikisha wanajiendeleza kielimu kupitia nafasi walizonazo ili wasimamie wenzao katika sekta mbalimbali zikiwamo za kijamii, kiserikali, kiroho na kichama kwa ujumla.

Aliagiza vijana wa wilaya hiyo kuwa mabalozi wa kuwashawishi wenzao kufanya kazi zinazokubalika ikiwamo za kilimo, uvuvi na ufugaji ambazo zitawabadilisha maisha yao kiuchumi.