Exim yazindua huduma ya upendeleo kwa wateja wakubwa

15Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar
Nipashe
Exim yazindua huduma ya upendeleo kwa wateja wakubwa

BENKI ya Exim Tanzania imezindua huduma yake mpya ya ‘Preferred Banking’ inayotoa upendeleo maalum katika utoaji huduma zake za kibenki sambamba na punguzo la gharama kwenye mahitaji ya kijamii kwa wateja wake wakubwa na wa kati.

Meneja Bidhaa wa Benki Ya Exim Tanzania, Aloyse Maro katikati.

Akizungumza kwenye uzinduzi maalum wa huduma hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Meneja Bidhaa wa benki hiyo, Aloyse Maro, aliyataja baadhi ya mahitaji hayo ya kijamii kuwa ni yale yanayoendana na aina ya maisha ya mteja husika (lifestyle), kama vile manunuzi (shopping), burudani, safari, malazi ya hoteli na huduma za vyakula.

“Huduma hii imebuniwa maalum kukidhi mahitaji na huduma za kifedha kwa wateja wetu wakubwa na wale wa kati. Kupitia huduma hii wateja wetu watarajie huduma nzuri kutoka kwa mameneja mahusiano tofauti waliopo kwenye matawi yetu ili waweze kufurahia upendeleo kwenye huduma zetu za kibenki pamoja na zile za mahitaji ya kijamii kulingana na ‘lifestyle’ zao,’’ alisema.

Alisema kupitia huduma hiyo, wateja watanufaika kwa kupata huduma za kibenki saa 24 kila siku kupitia simu zao, nyongeza ya muda wa utoaji huduma kwenye baadhi ya matawi pamoja na ongezeko la mashine za kutolea fedha (ATM), nchi nzima.

“Kifupi tunatambua matarajio ya mabadiliko ya kihuduma yaliyopo kwa wateja wetu. Huduma hii ya ‘Preferred Banking’ itaendana na mahitaji ya jamii ya Kitanzania ambayo kwa sasa ni ile ya kuhama hama, inayoingiliana na jamii za kimataifa na zaidi yenye shahuku ya kutambulika zaidi,” aliongeza Mkuu wa Hazina wa benki hiyo, George Shumbusho.