Kwa mujibu wa mtafiti wa zao hilo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) Ukiriguru, Dk. Paul Saidia pamba UKM 08 inayotumiwa na idadi kubwa ya wakulima inahitaji maji yasiyozidi milimita 500 tofauti na ilivyo kwa sasa maji yameongezeka zaidi.
Wakulima wanataja hali hiyo kushusha uzalishaji wa zao hilo kwa msimu ujao kutokana na mavuno kidogo yatakayopatikana kulinganisha na misimu mingine iliyokuwa na mvua za wastani.
Mkulima wa Kijiji cha Kitwechembogo wilayani Biharamulo, Charles Mbuga alisema, amelima ekari tatu kwa sasa ni eneo dogo ambalo lipo kwenye mwinuko ndilo lililobaki bila kuingiwa na maji ambapo analazimika kusubiri mvua ziishe ili apande upya.
“Matarajio kwa kipindi hiki ni madogo kwani ni tofauti na misimu mingine ambayo tulipata mavuno kutokana na mvua kuwa za wastani na zao hili haliitaji mvua nyingi kama za sasa,” alisema Renatha Jackson, mkulima kutoka Kata ya Ruziba.
Mkulima wa kutoka Ibuka, Bundala Maziku alisema, mashamba ya pamba yamejaa maji na sasa wanaendelea kuweka matuta kando ya mashamba ili kuzuia maji kuingia ndani.
Alisema wana shaka ya kushindwa kulipa gharama za pembejeo ambazo walichukua kwa mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Paul Mazinze kutoka Mwakalima wilayani Misungwi alisema, mvua imeifanya ardhi kutitia na muda wote inakuwa imejaa maji na kuwa majaruba jambo lililofanya washindwe kulima na kusubiri wakati mvua zitakapo koma.
Aliiomba serikali na wataalamu wa kilimo kuwatembelea ili kuwapa mbinu za kitaalamu ya nini wafanye kwa kuwa toka mvua ilipoanza hawajatembelewa na wataalamu na kuwafanya wasitishe shughuli hizo kwa muda hadi zitakapokata.
AMCOS YAELEZA UKUBWA WA TATIZO
Hali hiyo imezua hofu pia kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Kilimo na Masoko (AMCOS) kuhusu matarajio ya zao hilo kuadimika sokoni katika misimu ijayo huku wakiwahimiza wakulima kutokukata tamaa na mvua inapokata wapande tena.
Katibu wa AMCOS Kata ya Nyakahura Kahama, Emmanuel Paschal, alisema kwa msimu huu hawana mategemeo ya kufikia lengo kutokana na mvua.
Alisema katika msimu wa 2021/2022 walipata tani 59,000 kati ya tani 37,000 zilizokuwa zimelengwa katika makusanyo ya zao hilo, lakini kwa sasa hali ni tofauti na kulazimika kuwashawishi wakulima kurudia kupanda tena kwa mwezi Desemba mwishoni mwa Januari endapo mvua itapungua.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Uyogo-Ushetu, Maganga Msanja, alisema, wana wakulima 275 na matarajio yao ni kupata tani zaidi ya 100 za zao hilo, mvua imesababisha kutofikisha.
Alisema mvua inaathiri ukuaji wa kilimo hicho na kuwataka wakulima kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na wataalam ili kukabiliana na hali hiyo.
WATAALAMU WAANIKA MBINU KUKINUSURU
Mtafiti wa zao hilo kutoka TARI Ukiriguru, Dk. Paul Saidia, anasema wakulima wanaweza kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo kulima katika maeneo yasiyo ya bondeni.
“Wakulima ambao tayari wamepanda wahakikishe wanatengeneza mitaro itakayosaidia kuondoa maji shambani, walime kwa njia za matuta ili kuruhusu maji kupita katika maeneo ya wazi ili yasiathiri mazao yao,” alisema Dk. Saidia.
Aidha, alisema kwa mbegu bora ya pamba ya UKM 08 inayokua kwa muda usiopungua miezi sita itastahimili kiwango cha maji ya milimita 500 pekee na ikizidi hapo zao hilo linaweza kuoza na ni muhimu kuchukua taadhari.
“Mbinu zote tumekuwa tukizipeleka kwenye Bodi ya Pamba ambayo kazi yake ni kuhakikisha zinawafikia wakulima na kuwasaidia kulima kwa tija,” alisema Dk. Saidia.
Mkaguzi wa pamba kutoka Bodi ya Pamba (TCB), wilayani Kahama, Emmanuly Kireo, alikiri kuwapo kwa athari hizo na kusema kuwa mpaka sasa wameshindwa kujua ni hekari ngapi za mashamba zimelimwa na wakulima licha ya kuwa na marajio ya kupata tani 48,000.
Kireo alisema, wakulima wenye mashamba bondeni ndio wanaoathirika zaidi kulinganisha na wengine kwani maji yanapokuwa mengi shambani kama mashamba ya mpunga yanavyokuwa huwa pamba inashindwa kutoa maua yake.
Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Marco Mtunga akizindua msimu wa ununuzi hivi karibuni alisema matarajio yao katika msimu wa ununuzi 2023/2024 ni kufikia uzalishaji wa tani 400,000 kulinganisha na uzalishaji wa tani 174,031 za msimu wa ununuzi 2022/2023.
Aidha, bodi hiyo inatarajia kuongeza mauzo kutoka dola za kimarekani milioni 227.1 hadi dola milioni 238.46 huku wakiwa na bajeti ya Shilingi bilioni tano kwa ajili ya umwagiliaji wa zao hilo.
MIKAKATI YA WAKUU WA MIKOA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, alitaja mikakati ya kunusuru pamba mkoani humo ikiwa ni pamoja na kusisitiza usimamizi wenye tija wa zao hilo utakaofanywa na maofisa ugani.
Alidokeza mpango wake wa kukutana na maofisa ugani wa ngazi zote kutoka wilaya zote kupeana mikakati ya kuwasaidia wakulima kulima kisasa na kukabiliana na athari za mvua hizo.
“Wiki ijayo nitakutana tuweke mikakati ili tuone namna ya kulifanya zao hili liwe na tija kiuchumi kwa mkulima na taifa kwa ujumla," alisema Makalla.
Alisema tayari serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa sekta ya kilimo nchini na kwamba hakuna sababu ya uzalishaji wa zao hilo kukwama kwa aina yoyote wala kuzorota.
“Serikali imeweka mazingira rafiki kwa mkulima kwa kumpunguzia gharama za pembejeo na kuboresha mbegu bora, hivyo ni wakati mwafaka kwa Mwanza kurudisha uzalishaji na kutoa Pamba itakayokidhi soko la kimataifa na itawezekana baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu,” alisema Makalla.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme aliagiza maofisa ugani kuingia shambani wenyewe kukabiliana na tatizo hilo.
Aliwataka maofisa hao kuwatembelea wakulima na kuacha tabia ya kukaa ofisini ili kuwapatia elimu ya kilimo ambacho kinaendana na wastani wa mvua hizo.
“Serikali imetoa pikipiki 224 kwa Maofisa Ugani, hivyo hakuna kisingizio kwamba hamna usafiri lazima waende kwa wakulima wawapatie elimu ya Kilimo ambacho kinaendena na wastani wa Mvua sasa hivi,” aliagiza Mndeme.
Alisema mazao yaliyoharibika siyo pamba pekee ni pamoja na mahindi kutokana na kuzidiwa mvua na serikali itahakikisha inakuwa karibu na wakulima ikiwa ni pamoja na kuwapa mbegu na elimu ya kuhimili mvua.
*Imeandaliwa na Shaban Njia (KAHAMA), Marco Maduhu (SHINYANGA), Restuta Damian (BIHARAMULO), Thomas Wandiba (SAUT), Vitus Audax (MWANZA).










