Eka 1 mpunga gunia 5 Msalala

08May 2016
Marco Maduhu
Kahama
Nipashe Jumapili
Eka 1 mpunga gunia 5 Msalala

Wakulima wa mpunga katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wanavuma mpaka gunia 25 kwa ekari moja baada ya kunufaika na elimu ya kilimo cha kisasa.

shamba la mpunga.

Mafunzo kwa wakulima hao yalitolewa kwa kipindi cha miaka mitatu 2013-16 na Programu ya Serikali ya (MIVARF).

Programu hiyo imelenga kumuinua mkulima kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa kwa kushirikiana na Shirika la SAIDA, ambalo limekuwa likitoa elimu kwa wakulima kuacha kilimo cha mazoea.

Mmoja wa wakulima hao, Mathias Michael alisema baada ya kupata elimu ya kilimo cha mpunga cha kisasa, alisema amekuwa akipata wastani wa magunia nne mpaka tano kwa ekari.

Awali, alisema Miachael, alikuwa akivuna gunia tano katika ekari mbili.

Naye Mratibu wa Shirika la SAIDA, Kristina Heneriko alisema mradi huo umewafikia wakulima wa mpunga 1,195 kutoka kata sita za Halmshauri ya Msalala.

Alizitaja kata hizo kuwa ni Bulegi, Busangi, Tobo, Chela, Kashishi na Segese ambako pia wamewajengea wakulima uwezo wa kutafuta Masoko.

“Mwaka wa kwanza wa Mradi huu 2013 wakulima walilima hekari za mpunga 992 lakini baada ya kuipokea vizuri elimu mwaka wa kilimo 2014-15, zililimwa hekari 2,032 na kuvunwa tani 105,000," alisema Heneriko.

"Msimu wa mwaka kuu tunategemea mavuno mengi zaidi jambo ambalo linaleta faraja kwa wakulima kuinuka kiuchumi.”

Mtaalamu wa Programu ya MIVARF, Wangael Wilfred alisema mradi huo wa kumuinua mkulima kiuchumi, pia umewaunga wakulima kwenye vikundi vya ujasiriamali.

Aidha, programu hiyo imewajengea uwezo wa kutafuta masoko ya mazao yao, kuweka maghala ya kuhifadhia mazao na kuwatengenezea miundombinu imara ya barabara na unatekelezwa kwenye halmashauri 76 hapa nchini.