Albino waponzwa na ujinga wa ukosefu ushahidi wa kisayansi wa ulemavu

28Jun 2016
Francis Kajubi
Dar es Salaam
Nipashe
Albino waponzwa na ujinga wa ukosefu ushahidi wa kisayansi wa ulemavu

WADAU wa mapambano dhidi ya mauaji na unyanyapaa wa watu wenye ualbino walibaini kuwa, tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi za watu hao barani Afrika bado ni changamoto kubwa.

Hayo yalibainishwa na wadau kuwa, nchi nyingi za Kiafrika hazina sensa sahihi ili kuwabaini watu wenye ualbino iwe katika ngazi ya mikoa ama kitaifa.

Pia hakuna takwimu za kiutafiti kubaini ni nchi zipi barani Afrika zinaongoza kwa mauaji ya watu wenye ualbino na badala yake kinachofanyika ni utaratibu wa kukisia kulingana na matukio yanayoripotiwa kwenye vyombo vya habari pekee.

Hayo yalibainishwa katika Kongamano lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujaribu kubaini changamoto zinazowakabili na namna gani watachukua hatua kukabiliana nazo ili kuleta ustawi wa watu hao.

Waliohudhuria kongamano hilo ni washiriki 150 kutoka nchi 29 za kanda ya Afrika pamoja na Serikali, Mashirika yasiyokuwa ya Serikari, Taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wanaharakati, Wataaamu wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na wasomi

“Kongamano hili lilijikita zaidi katika kuleta hoja mpya za kuwalinda watu wenye ualbino barani Afrika dhidi ya mauaji pasipo kutathmini idadi yao, wala kujadili kuhusu adhabu ya kifo kwa watuhumiwa ambayo binafsi siiungi mkono,’ alisema Mtaalamu Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero.

Imani potofu katika jamii nyingi za nchi za Afrika ilibainishwa kuwa, zinachangia pia kuwepo mauaji ya watu wenye ualbino kwa kiasi kikubwa.

‘Mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa lengo la kuuza viungo vyao vya miili yanaendelea kutokea barani Afrika kutokana na ujinga kuhusu chanzo cha kisayansi cha ulemavu wa ngozi,vitendo vya kishirikina na hatua zisizoridhisha za Serikali,’ alisema Ero.

Biashara ya viungo vya miili ya watu wenye ualbino imesambaa takribani barani kote Afrika.

Nchini Tanzania, takwimu za Shirika la Under The Same Sun zinaonyesha kuwa, tangu mwaka 2006 watu wenye ualbino 74 wameuawa, 56 wakinusurika kuuawa.

Huko Malawi mashambulizi ya watu wenye ualbino yanazidi kuongezeka.Takribani watu wenye ualbino 18 waliuawa nchini huko tangu mwaka 2014 mwishoni na wengine watano wamepotea bila kujulikana walikoishia.

Matukio 45 ya kujaribu kuwaua watu wenye ualbino yariripotiwa mwaka 2014 japo idadi inakisiwa kuwa ni kubwa zaidi
Hata hivyo, bado hakuna takwimu sahihi za uhalifu dhidi ya watu wenye ualbino nchini Malawi

Paul Butao, kutoka Ofisi ya Ushirikiano wa Kimataifa nchini Malawi alikiri kuwepo mauaji mengi ya watu wenye ualbino nchini Malawi.

“ Ni vema Serikali za Afrika kuona umuhimu wa kuwatambua wataalamu wa tiba mbadala na jamii zifahamishwe walipo ili kuleta urahisi wa kuwabaini waganga wa jadi wanaoshirikiana na wauaji,’ alichangia Butao katika kongamano hilo.

Nomasonto Masibuko ni Mkurugenzi wa Taifa na mwanzilishi wa Shirika la Jamii ya watu wenye ualbino nchini Afrika Kusini alisema kuwa, tatizo la mauaji na unyanyapaa wa watu wenye ualbino barani Afrika hupotea na kuibuka kwa sababu jitihada za kuliua bado hazijazingatiwa kikamilifu kuanzia kwa mtu mmoja mmoja kwa imani yake hadi kitaifa.

Anaongeza kuwa, watu wengi barani Afrika bado wanaamini kuwa watu wenye ualbino huwa hawafi bali hupotea.

"Tatizo ni kwamba, jamii kubwa ya ki-Afrika bado inaamini kuwa, watu wenye ualbino hawafi badala yake hupotea. Hivyo imani hii huwafanya watu kuamini kuwa, kutoa viungo vya mtu mwenye ualbino ama kumuua ni kujiletea bahati ya kupata mali nyingi. Hii ni changamoto kubwa hususani kwa jamii ya vijijini inayohitaji uelimishaji bila kuchoka," anasema Masibuko.

Kwa upande wake Jane Waithera, anayefanya kazi na Shirika la Positive Exposure nchini Kenya, linalojishughulisha na utoaji uelewa kwa jamii juu ya watu wenye ualbino, anasema nchini Kenya kwa sasa wamechukua hatua chache kwa mwelekeo unaofaa ambapo serikali imetenga kiwango cha bajeti cha kushughulikia matibabu ya macho na ngozi.

Waithera anasema "Bado hatuna sheria inayowabana watu wanaohatarisha maisha ya watu wenye ualbino, hivyo serikali inatakiwa kuchukua hatua mapema, vilevile bado hatuna takwimu sahihi ya watu wenye ualbino nchini kote," anasema Waithera.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisa Mawasiliano na Uchangishaji Fedha, Sam Clarke, kutoka Shirika la Standing Voice, anasema kuwa ni asilimia mbili tu ya watu wenye ualbino nchini Tanzania huweza kumudu tatizo la kansa ya ngozi ili kufikia umri wa miaka 40 ya kuishi.

Asilimia 98 ya watu wenye ualbino nchini Tanzania hufa kabla ya umri wa miaka 40 kutokana na kansa ya ngozi.

Kwa upande wake Vicky Mtetema, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under The Same Sun anasema kuwa si sahihi sana kutanabaisha kuwa, mauaji ya watu wenye ualbino yamepungua nchini Tanzania, kwa kuwa yapo matukio mengi ambayo bado hayafikiwi na vyombo vya habari ila yanatokea kila leo.

" Kwa mfano, mwaka jana huko mkoani Tabora kuliripotiwa kuwa, mjomba alimteka nyara mpwa wake na kutaka kumuuza kwa wanunuzi wa viungo vya mwili akiwa hai, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka kumi baada ya polisi kupata taarifa zake mapema kutoka kwa raia wema," anasema Mtetema akiiomba jamii kuwa bega kwa bega na jeshi la Polisi katika vita hii.

Akizungumzia tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi kwa Mashirika hayo, Mkurugenzi wa Programu za Jamii, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Rais, Amadeus Kamagenge anasema kuwa ni wakati sasa wa Mashirika hayo kufanya kazi kwa ukaribu na Taasisi hiyo kwani ndiyo yenye takwimu sahihi za watu waishio vijijini wakiwemo wenye ualbino.

"Sisi hawa watu tunakutana nao kila baada ya miezi mitatu na kuelimisha jamii wakiwemo wanafunzi, watumishi wa afya, walimu, polisi na mengineyo kwa sababu sisi tuna takwimu ya Watanzania asilimia 15 ya wanaoishi vijijini na sisi TASAF tuna data asilimia kubwa," anasisitiza Kamagenge.

Takwimu za mwaka 2006, zilizotolewa na Shirika la Tanzania Albino Society (TAS), zaidi ya watu wenye ualbino sabini waliuawa nchini Tanzania na wengine kuachwa na ulemavu.

Watalaam wa afya wanasema kuwa, kila watanzania 1,400 mmoja ana ulemavu wa ngozi na zaidi ya watu 33,000 nchini wanaaminika kuwa na ulemavu wa ngozi.

Katika kongamano hilo, wadau na Mashirika ya kupinga na kupambana na mauaji na unyanyapaa wa watu wenye ualbino waliafikiana hatua nne za kuwalinda watu wenye ualbino.

Hatua hizo ni pamoja na kujengea makaburi ya saruji watu wenye ualbino na kuwawezesha kwa vifaa vya ujenzi, kama saruji na nondo ili wapate kuziimarisha nyumba zao ili kuepuka uvamizi wanaofanyiwa na wafanyabiashara wa viungo vya miili ya watu wenye ualbino.

Jambo jingine liloafikiwa katika hatua hizo ni umuhimu wa waendesha mashtaka na Polisi wanaoshughulikia kesi za watu wenye ualbino, kupewa kozi maalum ya kutambua umuhimu wa kuziharakisha kesi hizo.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero aliyataja kuwa ni hatua za kuzuia, hatua za kulinda, hatua za uwajibikaji na hatua za kupambana na ubaguzi.

Hatua hizi nne zilifikiwa baada ya mapendekezo mazuri yaliyojadiiwa katika kongamano lililodumu kwa siku tatu Juni 17-19 mwaka huu, na zitawasilishwa katika Mkutano wa Umoja wa Afrika unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Kigali nchini Rwanda, kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa ili nchi wanachama zianze utekelezaji.

‘Mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kuuza viungo vyao vya mwili yanaendelea kutokea katika bara la Afrika kutokana na ujinga kuhusu chanzo cha kisayansi cha ulemavu wa ngozi, vitendo vya kishirikina na hatua zisizo ridhisha za Serikali,’ anasema Ero na kuongeza kuwa ‘Ripoti ya vyama vya kiraia inaonyesha kulikuwa na mashambulizi karibu 500 katika nchi 25 yakiwa ni matukio yaliyoripotiwa pekee,’ alisisitiza Ero.

Aidha Ero alifafanua kuwa, matukio mengi hayaripotiwi kutokana na usiri katika masuala ya ushirikina, ushiriki wa familia, na uwezekano wa ushiriki wa matajiri na watu wenye nguvu.

‘Masuala ya haki za binadamu yanayowakabili watu wenye ualbino ni dharura katika nchi kadhaa za ukanda wa maziwa makuu na lazima kushughulikiwa kwa hatua maalum na za ufanisi,’ alisema Ero.

‘Hatua maalum zilizozingatiwa ni pamoja na Serikali kutoa nondo na vitasa madhubuti vya milango kwa makazi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, hasa katika maeneo ya vijijini kama hatua ya kujikinga dhidi ya mashambulizi, kuwarejesha haraka na kwa usalama watu waliokimbia makazi kutokana na mashambulizi, na utoaji wa saruji kwa famiia ili kuziwezesha kujenga makaburi ya ndugu zao wenye ulemavu wa ngozi ili mabaki yao yasiweze kuibiwa,’ alisema Ero.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora nchini, Bahame Tom Nyanduga alisema kuwa, kwa kiasi kikubwa kongamano hilo limeyatazama vyema mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali.

‘Ni bahati nzuri kuwa, mapendekezo yetu ya namna ya kuwakinga watu wenye ualbino yamezingatiwa na hivyo sisi kama Serikali tutashirikiana vyema na Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa katika kutekeleza mafunzo kwa waendesha mashtaka na polisi wetu ili kesi zisikae sana’aliieleza Nipashe Nyanduga.

Aidha alisema kuwa, kuna ulazima sasa wa kuzitazama upya sheria za tiba asilia ili kutokomeza vitendo vya kishirikina vinavyosababisha watu wenye ualbino kuwindwa na kuuawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under The Same Sun, Vicky Ntetema alisema kuwa, katika kuzuia mauaji yasiendelee, kutakuwa na uhakiki mipakani pale mtoto ama mtu mwenye ualbino anapovuka kutoka nchi moja kwenda nyingine.

‘Kuna ripoti kuwa, wapo watu wenye ualbino wanasafirishwa kutoka ama kwenda nchi za Malawi na Msumbiji, hivyo tunaitaka Serikali kuweka nguvu na mikakati ya kuzuia na kupambana na biashara hii ya viungo vya albino.

Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez aliishauri Serikali kuhakikisha kuwa kwenye bajeti yake inatenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mambo yanayowahusu watu wenye ualbino na vema kiasi hicho kinachotengwa kiwe kinaongezeka maradufu kila mwaka.

Akizungumzia suala la Kansa ya ngozi inayowakabili watu wenye ualbino, Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Standing Voice alisema kuwa Programu ya kuzuia kansa ya ngozi kwa watu wenye ualbino inatolewa katika kliniki 27 kwenye mikoa 9 ya Kaskazini na Magharibi mwa Tanzania na kuwafikia maelfu ya albino katika kila miezi minne.

Hata hivyo suala la upatikanaji wa takwimu sahihi na za uhakika za watu wenye ualbino limeonekana kuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi barani Afrika.

Washiriki kutoka Vyama vya Kiraia waliahidi kuzishawishi Serikali zao kufanya sensa za uhakika ya maalbino na kupata taarifa zao, ambazo ni muhimu kwa mipango sahihi na sera ya kukabiliana; kuhakikisha kuwa vifaa vya kuimarisha uwezo wa kuona vinapatikana kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi wanapokuwa darasani na kutoa vizuia jua nafuu kama tiba muhimu ili kuzuia kansa ya ngozi, ambayo inaendelea kuondoa maisha ya albino.

‘Sasa kwa kuwa tuna orodha ya hatua maalum zenye ufanisi ambazo si ghali sana kutekelezeka, Serikali hazipaswi tena kuwa na kiburi kuhusu nini cha kufanya kuhusiana na suala hilo.Kupitia kongamano hili tumefanya kazi yao kuwa rahisi na wao pia wamekuwa sehemu ya mchakato huu,”alisisitiza Ero.

www.guardian.co.tz/circulation