Wizara ya Fedha, BOT fanyieni kazi maagizo ya Rais Magufuli

24Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wizara ya Fedha, BOT fanyieni kazi maagizo ya Rais Magufuli

RAIS John Magufuli, juzi alitoa maagizo kadhaa kwa Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) lengo likiwa kuziba mianya inayosababisha Serikali kukosa mapato yake, kudhibiti watumishi hewa na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya BoT juzi, aliiagjza benki ya NMB kurudisha Sh. bilioni saba walizowalipa watumishi hewa 2,800 kama mafao ya kustaafu, akisema idadi ya watumishi hewa imefikia 12,446 na kuagiza kusitishwa ajira serikalini na promosheni kwa mwezi mmoja hadi kazi ya kubaini watumishi hewa itakapokamilika.

Pia alizitaka Wizara ya Fedha na BoT kuhakikisha taasisi za kifedha na benki zinawafikia wakazi wa vijijini kuliko kujiwekeza mijini. Alisema BoT na Wizara ya Fedha zinapaswa kushughulikia tatizo la kuwapo kwa riba kubwa katika benki kunakosababisha wajasiriamali wadogo kushindwa kukopa.

Kadhalika, aliziagiza kushirikiana kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kutoka katika kampuni za uchimbaji madini na kampuni za simu.

Aidha, aliagiza kuwa na akaunti moja ya kuhifadhia fedha zote za Serikali ili kuondokana na kuwapo kwa ulipaji wa hundi hewa na vile vile kuziagiza kuangalia upya akaunti zenye fedha, lakini hazijatumiwa kwa muda mrefu kwani zinatumika kutoroshea fedha nje.

Rais Magufuli alitoa agizo lingine kwa BoT na Wizara ya Fedha ambalo ni kuhakikisha mabenki na taasisi za benki ambazo zinakiuka masharti, pamoja na benki za serikali zinazojiendesha kwa hasara zichukuliwe hatua.

Rais alizungumza mambo mengi ambayo yamekuwa yakigusa wengi na tunakubaliana naye kwamba Wizara ya Fedha na BoT wanawajibika kuyatekeleza haraka kama alivyowaagiza.

Suala la wawekezaji katika migodi kulipa kodi limekuwa mjadala mzito kwa miaka kadhaa sasa tangu milango ilipofunguliwa kwa ajili ya uwekezaji katika uchimbaji wa madini na wawekezaji wengi kutoka nje kuingia nchini na kuchimba. Watanzania wengi wamekuwa wakilalamikia Serikali kutowatoza kodi wanayostahili kulipa kwa kuwa wanapata fedha nyingi.

Pia zimekuwa zikitolewa hoja na wataalamu wa uchumi nchini kwamba kama Serikali ingezitoza kodi upasavyo kampuni za uchimbaji za kigeni, zingepatikana fedha nyingi ambazo zingeifanya Tanzania kupaa kiuchumi. Ni vizuri sasa malaka husika kuaza kutekeleza agizo hilo mapema kwa kuwa tusipokuwa makini, tunaweza kukuta nchi yetu ikibaki na mashimo huku wawekezaji wameshachuma faida na kurejea kwao.

Kampuni za simu nazo zinatengeneza faida kubwa, licha ya kulalamika kila mwaka kuwa zinapata hasara, hivyo tunakubaliana na kauli pamoja na uamuzi wa Rais Magufuli wa kuagiza zifuatiliwe ili serikali ipate kodi yake kama inavyostahili.

Tumeguswa pia na hatua ya Rais Magufuli ya kusitisha ajira zote serikalini kwa takribani mwezi mmoja kwa ajili ya kuhakiki watumishi. Uamuzi huo ni mzuri kwa kuwa utasaidia kuwaondoa watumishi hewa ambao kwa sasa ni mzigo mkubwa kwa taifa kutokana na kuongezeka kwa kasi na kufikia idadi hiyo Serikali kulazimika kuwalipwa Sh. bilioni 577 kila mwezi, ambazo zingetumika kutoa huduma za msingi kwa jamii.

Ni ukweli usiopingika kuwa taasisi za fedha na benki zinatoza riba kubwa na kuwakwaza wenye kipato kidogo na na wajasiriamali wadogo, hivyo kuna ulazima kwa BoT na Wizara ya Fedha kuweka masharti kwa benki hizo kupunguza riba sambamba na kupeleka huduma katika maeneo ya vijijini ili Watanzania wote wanufaike nazo.