Timu hiyo inatarajia kuingia uwanjani kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Serengeti Boys itaanza kampeni zake kwa kuwakaribisha yosso wenzao kutoka Shelisheli mchezo utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa marudiano kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.
Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA kabla ya kurudi na rekodi ya mfano siyo tu Tanzania, bali Afrika Mashariki.
Katika mashindano ya AIFF, timu hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki katika jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani CONCACAF (USA) na AFC (India, Korea na Malaysia).
Pia Serengeti Boys iliyoko chini ya Kocha Mkuu Bakari Shime ilicheza mfululizo michezo saba ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani (USA).
Kabla ya hapo, timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Tuna imani na timu hii hasa baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano nje ya nchi, hivyo mchezo wa kesho utakuwa na kukamilisha ushindi.
Tunachukua nafasi hii kuwaomba vijana wetu kujituma uwanjani na kucheza kwa bidii kwa lengo la kuwakomboa Watanzania ambao kwa muda mrefu wamekuwa wanyonge linapokuja suala la michuano ya kimataifa.
Tunaamini, mafanikio waliyopata kwa kushiriki mashindano hayo nje na mechi za kirafiki, watayaelekeza kwenye mchezo kwa kupata ushindi mnono ili iwe rahisi kujipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Watanzania wengi wameonyesha imani na kikosi cha Serengeti Boys, kadhalika ni matumaini yao kuwa kesho kikosi hicho kitawatoa kimasomaso.
Ni vizuri basi wachezaji wetu wakacheza kwa kujituma kwenye uwanja wa nyumbani na kupata ushindi, kwani kwa kufanya hivyo kutawaongezea mashabiki hamu na kiu ya kutoa sapoti kubwa kwao.
Tunafahamu changamoto mbalimbali ambazo mnakumbana nazo katika maandalizi, zinazosababishwa na kukosekana kwa wadhamini, lakini hiyo isiwaangushe na kesho tunawaombea mpeperushe vyema bendera ya Tanzania katika michuano hiyo.
Kufanya vizuri kutaziamsha kampuni, taasisi na wadau ambao husubiri kuona mafanikio, ndipo wapeleke misaada. Huu ni wakati wa kuwainua Watanzania ambao wamechoka kuwa watazamaji kwenye mashindano ya kimataifa.
Kadhalika, tunawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi hiyo kesho kuwaonga mkono vijana wetu watakaokuwa wakipeperusha bendera ya nchi kwenye mashindano hayo ya vijana.










