Pia wafanyabiashara hao wametakiwa kutowachagua viongozi ambao watawalaghai kwa kuwapa fedha kwani watakuwa na nia kujinufaisha wenyewe. Wito huo umetolewa na mwanasheria kutoka shirika lisilo la kiserikali la Eguality For Growth (EfG), Mussa Mlawa, katika mkutano wa siku moja uliokuwa unatoa tathmini ya mradi wa maendeleo katika masoko ya Jijini Dar es Salaam, Ilala, Kiwalani na Buguruni pia mahusiano kati ya wafanyabiashara wa masoko na vyombo vya habari ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa) na kufadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Legal For Service (LFS). Katika tathmini ya mradi huo wa majaribio wa mwaka mmoja katika masoko, kumejitokeza changamoto mbalimbali ambazo zilitolewa na wafanyabaishara hao, ambao wengine walidai masoko yao ni machakavu huku ushuru ukiwa unakusanywa, pia wengine walidai wanashindwa kugombea nafasi za uongozi katika masoko kutokana na fomu kuuzwa kwa gharama kubwa. Pia wafanyabiashara hao walisema mradi huo umezaa matunda kutokana na elimu walioipata kutoka EfG juu ya kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia, kujiunga katika vikoba na wanawake kujengewa uwezo wa kugombea nafasi za juu katika masoko, pamoja na kuwa na mahusiano ya karibu na vyombo vya habari. Wafanyabiashara hao walisema bei za fomu za kugombea uongozi zinauzwa kwa Sh. 30,000, 40,000 hadi Sh. 50,000, hali hiyo inawafanya washindwe kununua kutokana na mitaji yao ya biashara kuwa midogo na kuwafanya kushindwa kugombea nafasi mbalimbali katika masoko. Mussa alisema katika mwongozo ambao wameutoa katika masoko unaelekeza fomu zote ziuzwe kwa Sh. 10,000 pekee ili kuwapa fursa wanawake kugombea nafasi mbalimbali katika masoko. "Tulipata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara juu ya uuzwaji wa fomu kwa bei tofauti tofauti hali hiyo ilitulazimu kuandaa mwongozo na kuutuma katika masoko ili fomu ziuzwe kwa Sh. 10,000 pekee ili kila mwanamke mfanyabiashara aweze kununua na kugombea nafasi yoyote ambayo ataona inamfaa,” alisema. Kwa mujibu wa Mlawa amewataka wafanyabiashara katika masoko ambayo yanatarajia kufanya uchaguzi hivi karibuni, kuhakikisha wanawachagua viongozi wenye sifa ambazo zitalilitea soko maendeleo na siyo kuchagua viongozi kwa kurubuniwa na fedha.
Wafanyabishara wapewa somo la uongozi
04Feb 2016
Nipashe
Wafanyabishara wapewa somo la uongozi
WAFANYABISHARA katika masoko, wametakiwa kufanya mabadiliko makubwa katika uchaguzi ujao wa viongozi kwa ngazi mbalimbali ili wachague viongozi wenye uwezo ambao watawaletea maendeleo.










