Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wazabuni wanaopewa kazi ya kukusanya ushuru hasa wa mazao, kutoroka na fedha za halmashauri hasa nyakati ambazo siyo za mavuno. Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi juzi mjini Rujewa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Francis Mtega, alisema Kamati ya Fedha imeamua kuleta pendekezo hilo kwenye Baraza ili kukabiliana na wazabuni wasio waaminifu kutokana na baadhi yao kutoroka na mapato ya Halmashauri na hivyo kuikosesha Serikali mapato. Mtega alisema kuanzia sasa mzabuni atalazimika kutoa kianzio cha makadirio ya miezi mitatu ili ikitokea anatoroka kabla ya kumaliza zabini yake, fedha hizo zitumike kufidia hasara ambayo halmashauri itakuwa imepata kutokana na kuondoka kwake. “Awali mzabuni alitoa kianzo cha fedha za mwezi mmoja, hali hii ilisababisha mzabuni huyo akiona amekosa mapato hasa nyakati ambazo siyo za mavuno anaamua kutoroka na fedha za halmashauri, hivyo tumeamua kubadili sheria ili wazabuni wawe wanatoa kianzio cha miezi mitatu,” alisema Mtega. Alisema kuwa hatua hiyo pia itatoa fursa kwa wataalam wa Halmashauri kuwafuatilia wazabuni na kuhakikisha wanalipa fedha za halmashauri kwa wakati na kwamba ikitokea wakachelewa kulipa watabainika kabla ya muda walioulipia fedha za kianzio haujamalizika. Mbali na mabadiliko hayo ya sheria, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Jeremiah Mahinya, alisema halmashauri yake pia imekamilisha kazi ya kufunga mfumo wa kielekroniki ambao utatumika kukusanya mapato ya halmashauri, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali Kuu. Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulamhussein Kifu, alisema utaratibu huo mpya utaiwezesha halmashauri hiyo kuepuka matatizo ya kifedha na kuwa na uhakika na ukusanyaji wa mapato yake. Alisema kwa muda mrefu Halmashauri hiyo ilikuwa ikipata hasara kutokana na wazabuni wanaopewa kazi kuwakimbia hasa nyakati za kilimo, hali ambayo ilikuwa ikikwamisha maendeleo kwa wananchi.
Mbarali kuwabana wazabuni wasiomaliza kazi
04Feb 2016
Nipashe
Mbarali kuwabana wazabuni wasiomaliza kazi
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imelazimika kubadili sheria zake za utoaji wa zabuni za ukusanyaji wa ushuru, ili kuziba miaya ya upotevu wa mapato na kukabiliana na hila inazofanyiwa mara kwa mara na wazabuni.










