Watembea kwa miguu wathaminiwe ujenzi barabara ya Mwenge

04Feb 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watembea kwa miguu wathaminiwe ujenzi barabara ya Mwenge

BARABARA ya New Bagamoyo jijini Dar es Salaam inayopanuliwa kipande kifupi chenye urefu wa kilomita 4.3, kutoka Mwenge-hadi Morocco ujenzi wake upo katika hatua za mwisho.

Kukamilika kwa barabara hiyo, kwa sehemu kubwa kutachangia kupunguza msongamano au foleni zilizokuwa zinakwamisha wasafiri kufika katika maeneo husika kwa mujibu wa ratiba zao.
Kuwapo kwa alama za usalama barabarani hususan alama za Pundamilia kwa ajili ya kuwahakikishia watembea kwa miguu wanavuka barabara salama uzingatiwe.
Barabara hii, itaruhusu njia tano za magari upana ambao haujawahi kushuhudiwa popote jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.
Imezoeleka kuwapo barabara za njia nne za kwenda na kurudi huku katikati kukiwa na eneo lililohifadhiwa kwa ajili ya bustani ama kwa lengo la kutenga tu barabara.
Barabara ya Sam Nujoma, Mandela na nyinginezo mfumo wake ni huo. Kitu kinachokuwa rahisi kwa anayevuka barabara kuangalia usalama wake kabla ya kuvuka upande mmoja.
Akitaka kuvuka hupaswa kutulia kwa dakika chache katika eneo la katikati, kabla ya kuhakikisha usalama wa barabara upande wa pili.
Pamoja na kwamba ni hatua za maendeleo kwa jiji kuwa na njia tano na kuruhusu magari mengi kupita kwa wakati mmoja,ni muhimu alama za Pundamilia ziwekwe katika barabara hii,ili kuepuka ajali.
Waendesha vyombo vya moto mathalani, magari, pikipiki na waendeshao baikeli ni wajibu wao kuheshimu vivuko vya wanaovuka baraabara muda wote ili kuhakikisha kuwa ajali hazitokei.
Eneo la barabara hii lililo 'busy ' zaidi kwa watu kuvuka ni kituo cha ITV sababu ya kuwapo wafanyakazi wa viwandani vilivyopo maeneo hayo.Pia eneo la Bamaga nako kuna wavukaji wengi kuelekea maeneo tofauuti.
Barabara hii inayotarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita, ni matokeo ya maamuzi ya Rais John Magufuli kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutumika kwenye sherehe za Uhuru zielekezwe huko.
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ilitoa wito kwa watembea kwa miguu na wananchi, kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha upanuzi wa barabara hiyo ili kufanikisha ujenzi ndani ya muda uliopangwa.
Kuna mwongozo na sheria, kanuni na taratibu za namna ya kuvuka barabara. Kwanza watembea kwa miguu wanapaswa kufuata kanuni za uvukaji barabara.

Tafuta sehemu salama ya kuvuka kisha simama kwenye ukingo wa barabara, angalia magari barabarani kushoto, kulia na sehemu zote za kukuzunguka, na sikiliza kama kuna gari linakuja liache lipite
Vilevile wakati hakuna gari linalokuja, vuka moja kwa moja barabara na usikimbie, angalia na sikiliza magari wakati wa kuvuka mahali palipo salama pa kuvukia.

Pili, chagua sehemu unapoweza kuona pande zote, ambapo dereva anaweza kukuona.

Pia inashauriwa kutovuka barabara pasipo na kona kali yoyote.

Mahali ambapo ni salama kuvukia barabara, ni pamoja na kwenye taa za barabarani, alama za Pundamilia, keep left, madaraja ya waenda kwa miguu kama pale Manzese na njia za chini au mahali palipo na askari wa usalama barabarani.

Iwapo kuna alama za Pundamilia karibu zitumie ipasavyo ila baada ya kumpa dereva muda wa kutosha kukuona, kusimama na kukuruhusu kabla ya kuvuka.
Aidha, madereva wanatakiwa kisheria kusimama pale watembea kwa miguu wanapoanza kuvuka kwenye alama.
Alama za barabarani, hasa Pundamilia zizingatiwe na watumiaji wote wa barabara kwa kuziheshimu alama hizi ili kuondoa ajali zinazoepukika.