Serikali ifikirie upya `sakata’ la TBC

03Feb 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Serikali ifikirie upya `sakata’ la TBC

SERIKALI imetangaza kutotangazwa moja kwa moja kwa sehemu yote ya vikao vya Bunge linalofanyika mjini Dodoma kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), lengo likielezwa kuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji wake.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, akautangazia umma kupitia Bunge, kisha akaungwa mkono na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba sehemu ‘itakayokatwa’ itarekodiwa na kurushwa kupitia kipindi cha ‘Leo katika Bunge’ nyakati za usiku.

Kwa maana hiyo, uamuzi wa TBC kusitisha sehemu ya matangazao hayo kutoka bungeni ni uamuzi wa serikali.

Wapo walioujadili uamuzi huo kwa namna tofauti, wengi wakipinga kwa vile utakuwa ni sehemu ya kuwanyima raia haki ya kupata taarifa kwa wakati.

Serikali ikiungwa mkono na baadhi ya wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikaelezea sababu za kufikia hatua hiyo kuwa, pamoja na kupunguza gharama, itatoa fursa kwa wananchi kuutumia muda waliokuwa wakiliangalia Bunge, kufanya shughuli nyingine za uzalishaji.

Tukizitazama sababu zilizotolewa na watawala kuhusu hatua hiyo, kimsingi hazifai kuwa nguzo imara ya kufikia uamuzi wa TBC kusitisha matangazo ya moja kwa moja.

Kwa maana hakuna gharama iliyo kubwa kwa TBC kuacha kuuwahabarisha na kuuelimisha umma kuhusu masuala yenye maslahi kwao, badala yake ikawaachia `ujinga’ kwa kutoyajua hayo!

Kukosa taarifa sahihi na kwa wakati unaofaa ni moja ya viashiria vinavyowafanya watu kutofikia uamuzi sahihi, lakini pia kujenga kizazi kinachojikita katika masuala yasiyokuwa na manufaa binafsi, kwa jumuiya za watu na jamii kwa ujumla.

Inapoelezwa kuwa watu washiriki shughuli za uzalishaji badala ya kuliangalia Bunge, waliofikia uamuzi huo walitoa fursa gani kwa kada kama wafanyakazi wanaoingia zamu usiku ama wanaofanya kazi nyakati hizo kitakaporushwa kipindi cha ‘leo katika Bunge’?

Pamoja na uhalisia huo, inaweza kukubalika vipi kwamba kupitia matangazo ya moja kwa moja bungeni tu, ndipo watu wanashindwa kuzalisha badala yake wanajielekeza katika chombo hicho cha uwakilishi wa umma?

Vipi kuhusu watu wanaoutumia muda huo kwa ajili ya kuangalia filamu kama za bongo movie, vichekesho, bongo flavor, filamu za ki-Nigeria na nyingine zozote zinazoonekana kupitia runinga?

Kwa maana kama hoja ni watu kutoitazama runinga nyakati za asubuhi na mchana, basi ingefaa kwa watawala kufikiria namna ya kuvidhibiti vyombo hivyo vya mawasiliano ili visitumike kwa namna yoyote ile, na si kwa jambo jema kama vikao vya Bunge tu.

Inavyoeleweka miongoni mwa walio wengi ni kwamba sababu za kisiasa zimetumika na kupewa uzito mkubwa katika kufikiwa kwa uamuzi huo.

Kwamba wabunge wa upinzani wamekuwa wakilitumia Bunge kujiimarisha zaidi kupitia namna bora ya kujenga hoja na kuikosoa serikali.

Kama taarifa hiyo ni sahihi ama lah, ikumbukwe kwamba matangazo ya moja kwa moja ‘yanaibeba’ pia serikali hasa pale inapotoa maelezo tofauti kuhusu kazi nzuri zilizofanyika, zinazofanyika na zitakazofanyika katika kustawisha maisha ya watu na maendeleo ya nchi.

Ni kupitia Bunge, serikali inaujulisha umma kuhusu masuala kama fursa za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hivyo ingefaa kwa raia kupata taarifa njema kama hizo kupitia matangazo ya moja kwa moja, badala ya kusubiri marudio ya vipindi visivyotoa uhakika wa kuwapo kila hoja iliyowasilishwa kutokana na uhariri unaofanyika.

Katikati ya hali hiyo, si rahisi kwa Taifa kujiaminisha kwamba kizazi cha sasa na kitakachokuja wakati marufuku ikiendelea, kitamudu kushiriki kwa ufanisi katika hoja na ushindani unaoiunganisha Tanzania kwa jumuiya hizo za kikanda.

Wakati Tanzania ikizuia matangazo hayo bungeni (japo kwa sehemu), Kenya inafungua milango zaidi ya uwazi wa taarifa pale wanaoomba nafasi za juu za utumishi wanapohojiwa na tume ama kamati mahususi, runinga zinatangaza moja kwa moja.

Hivyo ni vigumu kwa Mtanzania anayefungiwa wigo wa kupata taarifa, akashindana na Mkenya mwenye taarifa zinazolihusu taifa lake, mifumo na masuala yenye maslahi kwa umma.

Kujenga kizazi kisichokuwa na taarifa sahihi zinazotoka kwenye chombo cha uwakilishi mpana wa wananchi ni kuliangamiza taifa na kuungamiza uzalendo dhidi ya mataifa mengine hasa yaliyo wanachama katika jumuiya za kikanda kama ilivyo Tanzania.

Ndio maana, hata hatua iliyofikiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, kuwazuia waandishi wa habari wasitekeleze wajibu wao kwa matukio yaliyohusiana na baadhi ya wabunge kupinga kuzuiwa matangazo hayo, ulipaswa kuishangaza dunia!

Kwamba mwanataaluma ya habari na mawasiliano anapofikia hatua ya kunyoosha mkono akiziba sehemu ya kamera isichukue matukio ndani ya taasisi ya umma, anapata wapi ujasiri huo hata kuligeuza Bunge kuwa kama sehemu ya familia yake!

Owen angefanya hivyo ndani ya nyumba yake popote anapoishi nchini ingekuwa na maana, ama kama ingetokea akiwa katika masuala yake binafsi, isingekuwa na shida.

Lakini alipolifanya hilo ndani ya chombo cha umma, sina hakika kama anapaswa kuistahili heshima inayoistahili ofisi ya habari, elimu na mawasiliano ya Bunge.

Kumbe basi ipo haja kwa watawala kuufikiria upya uamuzi wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja, iziepuke sababu zisizokuwa na mashiko badala yake iutaze umma mpana na namna unavyonufaika kwa matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni kupitia TBC.

+255 754691540, 0716635612
[email protected],[email protected]