Wachezaji hao ni Oscar Joshua na Haji Mwinyi ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwekana benchi huku mmoja akitawala kwenye namba hiyo.
Alianza Joshua aliyejihakikishia namba kikosi cha kwanza kabla ya mambo kubadilika kutokana na ujio wa Mwinyi ambaye naye kwa siku za karibuni amepoteza makali yake na kujikuta akimpa nafasi ya kutamba Joshua.
Yanga imeongeza wachezaji wengine wanne katika usajili unaondelea sasa na miongoni mwa wachezaji hao yumo beki wa pembeni, Hassan Kessy aliyetua akitokea Simba.
Kessy alionyesha uwezo mkubwa na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kabla ya kutibuana na uongozi wa klabu hiyo na kuamua kuondoka.
Amesajiliwa Yanga na hatua hiyo inakwenda kukoleza moto na ushindani wa namba kwenye kikosi cha kwanza.
Kessy anasema hana hofu na vita hiyo kwa kuwa anajiamini na uwezo wa kucheza kwa mafanikio anao.
"Kwa nini nihofie namba... najua Yanga walikuwa na sababu ya kunisajili," alisema Kessy.
Beki huyo alianza mazoezi ya pamoja na timu hiyo wiki iliyopita na kusema: "Nanafahamu vita ya namba nayokwenda kukutana nayo klabu ya Yanga, lakini sina hofu...nimejiandaa kwa ushindani huo.
"Suala la kucheza kwenye kikosi cha kwanza huo utakuwa ni uamuzi wa benchi la ufundi, nafahamu hapa kuna wachezaji wengi wenye uwezo, lakini Yanga walikuwa na sababu maalum ya kunisajili."
Alisema atakachokifanya ni kuhakikisha anakuwa kwenye kiwango bora wakati wote ili aweze kutimiza majukumu yake kwa ufasaha pale atakayopewa nafasi ya kucheza.
"Mchezaji ukiwa kwenye kiwango cha juu utakosaje namba, hicho ndicho ninachotaka kukifanya, nitajituma na kuhakikisha kiwango changu kinakuwa juu na kumuachia kocha kuamua kunipanga au vinginevyo," Kessy alisema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na kocha wa timu hiyo Pluijm, ambaye aliliambia Nipashe kuwa Kessy ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa hapa nchini.
Anasema kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ataongeza changamoto kwenye timu yake.
"Changamoto ni jambo linalokufanya ufanye vizuri, naamini ataongeza kitu kwenye kikosi changu," alisema Pluijm.
MICHUANO YA KIMATAIFA
Kessy ambaye ameambatana na kikosi cha timu hiyo kwenda kuweka kambi nchini Uturuki, alisema kuwa amejiandaa kuhakikisha anaisaidia timu yake hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
Alisema kuwa ushiriki wa Yanga kwenye michuano ya kimataifa ni moja ya mambo yaliyomvutia kujiunga na 'Wakimataifa hao'.
"Hakuna mchezaji asiyependa kushiriki michuano ya kimataifa, kwangu hii ni changamoto nyingine kuhakikisha naisaidia timu yangu kufanya vizuri kwenye michuano hii," aliongeza.










