Pia timu hizio zitarudiana Julai 2, 2016 ugenini ili mshindi wa jumla kusonga mbele.
Serengeti Boys itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kwenye ziara ya India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016), ambako japo hawakurejea na Kombe, lakini wlifanya vizuri.
Kwa ujumla, Serengeti Boys imecheza michezo saba ya kimataifa ya kujipima nguvu bila kupoteza hata mmoja, kuanzia dhidi ya Misri mara mbili, India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani na kabla ya hapo itakumbukwa timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Serengeti Boys ilimaliza Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao 3-0. Serengeti Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na awali walipokutana walitoka sare ya 2-2.
Ukitazama timu ambazo zimecheza na Serengeti Boys katika mechi saba zilizopita za kimataifa, nyingi ni ambazo ziko vizuri kuliko wapinzani wajao, Shelisheli.
Kisaikolojia hii ni nzuri kwa wachezaji wetu, kwamba wanaweza kujiamini wameiva kiasi cha kutosha baada ya matokeo ya mechi za awali na kuamini wanakwenda kuifunga Shelisheli.
Lakini upande wa pili, inaweza kuwa mbaya iwapo kujiamini kwa vijana wetu kutafikia kwenye kuwadharau wapinzani – kwamba kama waliwafunga Misri kwa nini washindwe kuwafunga Shelisheli. Kama walitoa sare na Marekani nchini India watafungwaje na Shelisheli hata ugenini.
Ndiyo maana leo Lete Raha tunauambia uongozi wa TFF, hususan Kamati ya Soka ya Vijana kukaa na benchi la Ufundi kuwakumbusha umuhimu wa kuwandaa kisaikolojia pia vjana, wasilewe sifa mwisho wa siku wakaja kuumbuka mbele ya wale ambao wao wanaamini ni vibonde.
Soka ni mchezo unahohitaji nidhamu wakati wote, ukileta mzaha kidogo, unaambulia patupu – hivyo basi mafanikio ya awali yasiwavimbishe vichwa wachezaji wa Serengeti Bosy wakaidharau Shelisheli, bali wajiandae kikamilifu kwa ajili ya kwenda kupigania ushindi ili wavuke kizingiti hiki cha kwanza. Kila la heri Serengeti Boys.










