Wakizungumza katika semina ya wabunge kuhusu fursa za utangamano wa Afrika Mashariki iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa uliopo bungeni mjini Dodoma katikati ya wiki, Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, alisema yeye na wenzake hawana magari.
Aidha, Makongoro ambaye alikuwa mmoja wa makada 40 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 15, mwaka jana alisema hali yao ni tofauti na Wakenya.
Alisema Kenya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wana ofisi, tena kwenye jengo la ghorofa.
Akasema kwa Tanzania, Wabunge hao tisa wana ofisi Arusha pekee hivyo kuwalazimu kwenda kuzungumza kwenye mahoteli wanapopata wageni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Makongoro akadai kuwa yeye na wenzake hawana magari na kuomba serikali na Bunge la Jamhuri viwasaidie kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Kwa upande wa serikali, tayari Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga ameshasema kuwa wizara yake itawasaidia wabunge hao kupata ofisi ndogo katika mji wanaopendekeza, japo tunaamini Nipashe itakuwa ni Dar es Salaam.
Balozi Mahiga alisema ingawa ofisi yake ipo tayari kutatua changamoto ya ofisi kwa Wabunge hao, suala la magari itabidi aliombe Bunge liwakopeshe kama linavyofanya kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri.
Tanzania ina wabunge tisa kwenye Bunge la Afrika Mashariki, lenye jumla ya wabunge 45 kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Tunatambua, Nipashe, kwamba Wabunge hawa wa Afrika Mashariki wana mahitaji ya ofisi na usafiri kama ambavyo mwenyekiti wao amewasilisha kwa serikali na Bunge wiki hii.
Lakini pia tunaona, Nipashe, Wabunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania hawako sahihi kudai mahitaji kwa kujilinganisha na wenzao wa Kenya.
Hawako sahihi kudai mahitaji kwa kujilinganisha na wenzao wa Kenya kwa sababu nchi mbili hizi zinaweza kuwa wanachama wa Bunge moja lakini kiuchumi hazipangwi kwenye 'zizi' moja.
Bahati nzuri nchi za Afrika Mashariki pia zilisoma bajeti zake za mwaka 2016-2017 Jumatano iliyopita, na kama watakuwa wamesoma vizuri bajeti za nchi mbili hizi, tunaamini Nipashe, wabunge wetu waliona kuwa makadirio ya mapato na matumizi ni tofauti.
Kutaka Serikali itoe mikopo ya magari kwa Wabunge tisa hao, kwa mfano, kuna maana nchi ikatafute Sh. bilioni 810 katika tu ununuzi wa magari ambayo huambata na gharama za ziada katika mafuta na matengenezo ya mara kwa mara.
Na Sh. bilioni 810 hizo, Wabunge wetu ni lazima wafahamu, ni nje ya zaidi ya Sh. trilioni 7 ambazo ni pengo kati ya makadirio ya mapato na matumizi katika mwaka ujao wa fedha kama ambavyo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alibainisha Jumatano.
Wakumbuke wamekuja na madai wakati Serikali imepunguza fedha za matumizi ya kawaida katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha na kuelekeza asilimia 40 ya bajeti hiyo kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.










