Viongozi watakaochaguliwa Yanga leo wanatakiwa kuheshimu katiba

11Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi watakaochaguliwa Yanga leo wanatakiwa kuheshimu katiba

KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wake leo ambao utawaweka madarakani viongozi wapya kwa muda wa miaka minne ijayo.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia viongozi walioko madarakani ambao wanafanya shughuli za klabu hiyo kukaa kinyume na katiba ya Yanga baada ya kumaliza muda wao tangu mwaka juzi.

Viongozi watakaochaguliwa leo ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji nane.

Wanachama hao watafanya uchaguzi huo kwa kufuata katiba ya mwaka 2010 kutokana na mabadiliko yaliyofanywa katika katiba yao mpya kutopata baraka ya serikali. Pia wanachama wa Yanga watachagua viongozi wao kwa kutumia kadi za zamani ambazo zina sahihi ya mwenyekiti na si zile za Benki ya Posta.

Hata hivyo, viongozi waliobakia madarakani walikuwa ni wachache huku wenzao waliochaguliwa nao katika uchaguzi uliopita kutangaza kujiuzulu kutokana na sababu mbalimbali zilizotokea ndani ya klabu hiyo.

Licha ya kubaki pungufu na kutakiwa kufanya uchaguzi haraka, waliendelea kuongoza klabu hiyo huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo liko chini ya Rais Jamal Malinzi, Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga kuwaangalia na kutochukua hatua yoyote.
Hadi ilipofika mapema Machi, Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutoa agizo la kuwataka Yanga wafanye uchaguzi wao kabla ya Juni 30 mwaka huu ndipo TFF nayo iliamka kupitia Kamati yake ya uchaguzi iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Aloyce Komba kutangaza tarehe ya uchaguzi ya klabu hiyo.

Siku chache baada ya kamati hiyo ya TFF kutangaza Yanga itafanya uchaguzi Juni 25, Sekretarieti ya klabu nayo ikazinduka na kutangaza tarehe yake ya uchaguzi ambayo ni leo, jambo ambalo lilianza kuzua malumbano na mabishano ya pande.

Kama ilivyotarajiwa na wengi, Yanga iliibuka kidedea katika 'ubishi' huo na kupewa baraka za kufanya uchaguzi wake ambao umekuwa na kalenda fupi kuliko chaguzi nyingine za wanachama wa TFF zilizowahi kufanyika, licha ya kuvunja katiba, wamepewa baraka na leo wanachama watachagua viongozi wao.

Hayo yamepita, leo ni siku muhimu kwa wanachama wa Yanga kutumia vyema nafasi ya kuamua mustakabali wa klabu yao kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Wanachama wanatakiwa kufahamu kuwa leo ndiyo watafanya uamuzi wa kuiendeleza klabu hiyo wanayoipenda au wataiingiza 'kaburini' kwa kuchagua viongozi ambao hawatawafanyia yale ambayo yamekuwa kero kwa viongozi waliomaliza muda wao.
Ili kuitendea haki klabu yao ambayo ndiyo pekee imebaki kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wanachama wanatakiwa kutofanya uamuzi kwa shinikizo lolote bali waangalie sifa za wagombea ambao watawaletea maendeleo na kuifikisha Yanga kule wanakohitaji.

Wafikirie ukongwe na hadhi ya klabu hiyo ilivyo sasa, je inastahili kuwa hapo ilipo? Kabla ya kufanya uamuzi wa kupiga kura wafikirie ni kwa nini timu kama TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeweza kutwaa ubingwa wa Afrika na kucheza fainali ya Klabu Bingwa Dunia.

Inawezekana pia kwa Yanga, kikubwa ni kuchagua viongozi watakaotekeleza mipango na programu ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi. Kuchagua viongozi wenye uchu wa mafanikio na si wale ambao wanaona ni fahari kuitwa viongozi au kuonekana tu pale timu inapotaka kusafiri nje ya nchi kwenda kucheza mechi za kimataifa.

Wanachama wanatakiwa kuchaguzi viongozi watendaji, sio viongozi ambao wanamuangalia mtu mmoja kuamua na kutekeleza analotaka yeye, uongozi wa pamoja ni siri kubwa ya mafanikio ya taasisi, kampuni au klabu yoyote ndani na nje ya nchi.

Kikubwa viongozi watakaochaguliwa leo wanatakiwa kuondoa aibu iliyotanda kwenye klabu hiyo kwa kuvunja katiba na kuonekana kuwa inabebwa na TFF, wanatakiwa wafahamu kiongozi asiyeheshimu katiba, basi vile vile afahamu hata majukumu mengine kuyavunja haitakuwa tatizo kwake.

Katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, tunawaasa wale ambao kura hazitatosha katika uchaguzi huu kutoanzisha migogoro ya kuwagawa wanachama na badala yake waungane na viongozi watakaochaguliwa kuifanya Yanga iwe tishio zaidi ndani na nje ya nchi.

Kila la kheri wanachama wa Yanga katika kutekeleza jukumu hilo la kikatiba la kufanya uchaguzi.