TFF: Hatuna vita na ZFA

02Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
TFF: Hatuna vita na ZFA

SIKU moja baada ya Kamati ya Muda ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kumtaka Rais wa TFF, Jamal Malinzi, aombe radhi kwa kudai kutoitambua, shirikisho hilo la soka nchini limesema hakuna vita kati yake na ZFA.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TFF, hakuna uhasama kati ya pande hizo mbili bali "mawasiliano yanaendelea kati ya TFF na vyombo husika kuhakikisha ZFA ambaye ni mwanachama mshiriki wa CAF anaendesha shughuli zake kwa mujibu wa taratibu".
Taarifa hiyo ilifrafanua kuwa kanuni na taratibu za CAF ziko wazi kuhusu nani aongoze Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na anapatikana kwa utaratibu upi.
"Kikubwa ni kuzuia ZFA isipate madhara ya kufungiwa na CAF," ilieleza taarifa hiyo.
Juzi wajumbe wa Kamati ya Muda ya ZFA walitua jijini Dar es Salaam na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa Malinzi anapaswa kujitokeza hadharani na kuomba radhi kabla hawajamfikisha mahakamani.
Wajumbe hao walikwenda mbali zaidi wakidai kuwa Rais huyo wa TFF ndiye "chanzo cha mvutano wa viongozi wa soka visiwani Zanzibar".