Si hivyo tu, hapa baada ya majibu wa serikali kwenye swali la msingi, karibu nusu ya wabunge husimama kutaka kuuliza swali la nyongeza kwenye sekta hizo.
Aidha, tathmini inaonyesha kuwa nishati na maji ni sekta zinazoongoza kwa wabunge kuuliza maswali mengi zaidi ikilinganishwa na sekta nyingine.
Ni hapa ambako pia wabunge licha ya kuuliza maswali na kujibiwa na serikali mara kwa mara juu ya hatua zinazochukuliwa kutatua kero hizo, wamekuwa wakionekana hawaridhishwi.
Mradi kama wa maji katika vijiji 10 kila wilaya ambavyo uchimbaji wake ulifadhiliwa na Benki ya Dunia umekuwa ukilalamikiwa kila mwaka kwa kuwa haujaleta nafuu yoyote kwa wananchi.
Kwa upande wa umeme, wabunge wamekuwa wakisimama na kulalamika kuwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya pili haujaweza kufika kwenye maeneo mengi wakieleza kuwa wananchi wao wanaishia kuona nguzo vijiji jirani.
Katika kipindi cha maswali na majibu hasa wakati wa maswali ya nyongeza katika masuala hayo, wabunge wengi wamekuwa wakisimama kuonyesha kiu ya kutaka kujua ufumbuzi wa kero ya maji na umeme katika maeneo yao.
Kutokana na kiu ya wabunge kuhusu masuala ya upatikanaji wa umeme na maji, wabunge wamekuwa wakihoji lini miradi hiyo itakamilika, na kwa kila kikao kumekuwapo na maswali ya aina hiyo aidha ni ya msingi au nyongeza.
Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa ni la Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, aliyehoji serikali itakamilisha lini mradi wa REA kwa awamu ya kwanza na pili na utekelezaji wa awamu ya tatu utahusisha vijiji gani wilayani Sikonge.
Swali hilo liliwanyanyua wabunge wengi wakiwamo wa upinzani ambao nao walitaka kujua mikakati ya usambazaji umeme kwenye majimbo yao ikoje.
Maswali ya aina hiyo yamekuwa ni mengi katika mkutano huu na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikiahidi mradi wa REA awamu ya tatu unatarajiwa kuanza mwezi ujao na utavifikia vijiji ambavyo havina umeme.
Siku iliyofuata, mbunge wa Mpanda vijijini Moshi Kakoso (CCM) akiuliza swali la nyongeza akihoji ni kwa nini miradi hiyo ilibagua maeneo mengine ikiwamo mkoa wa Rukwa.
Kakoso alihoji ni lini serikali itapaleka umeme katika vijiji 49 vya jimbo lake ambavyo havina umeme kabisa na kuhoji miradi hiyo kutolewa kwa matabaka kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.
Hata hivyo swali la Kakoso linajibiwa kuwa miradi ya umeme katika mikoa ya kusini haikuwa na uwiano kama ilivyokuwa katika mikoa mingine nchini.
Pamoja na majibu hayo pia serikali ilisema mikoa ya kusini Magharibi iliachwa katika miradi ya umeme wa REA I na II na kwamba katika awamu ya tatu ya miradi hiyo, Wizara itatoa kipaumbele katika mikoa hiyo.
Sambamba na maswali ya umeme kuinua wabunge wengi pindi yanapoulizwa pia hata kwenye masuala ya maji ni hivyo hivyo.
Hata hivyo katika uchangiaji wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alisema miradi ya REA inagawiwa kwa upendeleo kwani maeneo mengine wanafika katika vijiji vingi, lakini mengine hawajafika hata katika hata kijiji kimoja na kwamba mwaka huu itakuwa mwaka wake wa mwisho kuunga mkono bajeti ya REA.
Kwa upande wa maji, takribani kila wiki maswali ya sekta ya maji yanajitokeza ambapo hivi karibuni kutokana na wabunge kuwa na kiu kutaka kujua utatuzi wa matatizo ya maji katika maeneo yao, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Issac Kamwelwe, alijikuta akiwaambia wabunge kuwa wamekuwa wakichimba visima kwa kubahatisha hali iliyomlazimu Naibu Spika Dk. Tulia Ackson kuingilia kati na kumtaka afafanue kauli hiyo
kwa kuwa bajeti yao habari za visima zipo nyingi.
Akifafanua kauli hiyo, Kamwelwe anasema sio kwamba wanafanya kwa kubahatisha bali wanapofanya wanalenga kupata maji, lakini historia inaonyesha utafiti unapofanya katika visima 10, visima saba tu ndio vinavyopatikana na maji.
“Kutokana na mabadiliko ya miamba inatokea wakati mwingine unataka kuchimba visima 100, lakini visima 80 tu ndio vina maji.” anasema.
Aidha, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, aliongezea majibu hayo akieleza kua alipoanza mradi wa vijiji kumi aliyekuwa anafanya utafiti ni mhandisi mshauri na aliyechimba kisima ni mkandarasi, lakini utaratibu huo umebadilishwa hivi sasa.
“Kwa sasa mkandarasi anapewa mkataba wa kufanya kazi zote kufanya utafiti na kuchimba na akikosa maji itakuwa ni gharama kwake kutafuta eneo jingine lililo na maji.”
Pamoja na kutolewa majibu hayo na serikali, wabunge bado kila siku wanaendelea kusimama na kuuliza hatima ya upatikanaji maji kwenye maeneo yao huku wengine wakisema wananchi wanalazimika kunywa maji na mifugo na wengine wakihoji mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda mikoa ya Tabora na mingine.
Miongoni mwa wabunge ambayo wameuliza maswali kuhusu maji ni pamoja na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige aliyetaka kujua ni lini serikali itatekeleza mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria ili wananchi wa jimbo hilo wapate huduma ya maji.
Huku Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Muftaha Nachuma, anahoji serikali iko tayari kujenga bomba la kuvuta maji toka mto Ruvuma ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu bila mafaniko.
Pia mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Joyce Mukya, anauliza serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la maji katika mkoa wa Arusha.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, anahoji serikali itekeleze ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam kwa sababu ni takribani miaka sita tangu ahadi hiyo itolewe na tatizo bado lipo pale pale.
Kutokana na maswali ya sekta hizo kuwa mengi, serikali imeahidi kabla ya mkutano huo kuisha itawapa wabunge taarifa ya maeneo yatakayopata maji na umeme ili wananchi waweze kujua.










