Haki ya kiti na kanuni kitanzi ombi la mwongozo, utaratibu bungeni

08Jun 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Haki ya kiti na kanuni kitanzi ombi la mwongozo, utaratibu bungeni

PAMOJA na kwamba bungeni kumekuwa na kelele nyingi za wabunge kuomba mwongozo wa kiti au kusema kuhusu utaratibu, wengi wakitumia kanuni ya 67 (1), kuna kanuni mwiba ambazo pia zimewatia matatani wabunge.

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson

Vifungu vya kanuni hizo vimetumika kuwasimamisha wabunge saba kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge, kikiwamo cha hotuba kuu ya bajeti inayowasilishwa bungeni leo.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa gumzo wiki iliyopita na hadi sasa, ni mwenendo wa shughuli za Bunge la 11, ambalo linaendelea na mkutano wa tatu unaojadili bajeti mjini Dodoma.

Moja ya mambo ambayo yameleta mtikisiko na msisimko wa kipekee ni pamoja na Bunge kuzuia kurushwa kwa vikao vyake moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).

Tangazo hili liliibua mvutano na watu waliomba vikao vya Bunge virushwe moja kwa moja ili wananchi waone kinachoendelea bungeni, lakini hilo limeshindikana huku serikali ikidai haina fedha za kulipia gharama za kurusha matangazo ya Bunge.

Msimamo huo wa serikali uliibua mvutano mkubwa baina yake na wabunge hususani wa upinzani ambao wamekuwa wakidai matangazo yarushwe moja kwa moja, kiasi cha wengine kuamua kususa kushiriki baadhi ya shughuli.

Mbali ya mvutano bungeni, baadhi ya wadadisi wanahoji nguvu ya wananchi katika kuisimamia serikali, wakihoji kwa nini Bunge linaweza kuidhinisha fedha za matumizi mbalimbali, lakini haliwezi kuidhinisha fedha zitakazowaruhusu wananchi kuona kinachoendelea bungeni.

Jambo hilo limesababisha wapinzani kutoka nje mara kwa mara kutokana na kutokubaliana na maamuzi ya kiti.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wabunge kufungiwa kuhudhuria vikao kwa kile kinachodaiwa wanafanya vurugu bungeni na kudharau kiti.

Katika Bunge la 10 wabunge wanne wamewahi kusimamishwa kuhudhuria bungeni ambao ni Tundu Lissu wa Singida Mashariki, Peter Msigwa wa Iringa Mjini na aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na wa Ilemela Highness Kiwia.

Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge ambayo ipo chini ya kifungu cha 30A (1) cha sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge sura ya 296 na kanuni ya 74 (4) na (6) ndio yenye jukumu hilo.

Aidha, safari hii, waliotiwa hatiani ni pamoja na Esther Bulaya, Lissu, Zitto Kabwe, Pauline Gekul, John Heche, Halima Mdee na Godbless Lema.

Baadhi ya wabunge waliofungiwa miongoni mwa mambo yaliyowaponza ni kutaka Bunge lionyeshwe ‘Live’.

Wanadaiwa kuvunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1) 68 (10), 60 (2) na (12); na 74 (1) (a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.

“Siku ya tarehe 27 Januari, 2016 baadhi ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni walifanya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika, waliletwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Spika aliwasilisha majina mengine matatu siku ya tarehe 10 Machi, 2016 ili Kamati iweze kufanya uchunguzi kuhusu ushiriki wao katika vurugu zilizotokea siku tajwa hapo juu,” anasema George Mkuchika, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Anasema Bunge linaongozwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo tulizitunga na wabunge wenyewe.

Mkuchika anasema vitendo visivyo na tija, vilivuruga shughuli za Bunge zilizokuwa zikiendelea na kuathiri heshima ya mhimili huo mbele ya umma wa Watanzania jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.

Katika adhabu ya wiki iliyopita, Bulaya na Lissu wamezuiwa wasihudhurie vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia Mei 30, 2016 pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge hilo kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika na pia walihusika kwa kiasi kikubwa kuchochea vurugu zilizotokea Januari 27, 2016.

Sambamba na hao Gekul, Lema, Zitto na Mdee wao wameadhibiwa kutohudhuria vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyosalia kuanzia Jumatatu iliyopita, kwa kuwa walifanya vitendo ambavyo ni vya utovu wa nidhamu na dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika.

Kwa upande wa Heche, amekitakiwa asihudhurie vikao 10 mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja kuanzia Jumatatu iliyopita.

KANUNI ZINASEMA NINI?
Wabunge hao wanadaiwa kuvunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha sheria ya Haki, Kinga na Madaraka Bunge sura ya 296 ambacho kinasema ni kosa kwa mtu yeyote kuzuia au kuleta usumbufu katika maeneo ya Bunge wakati wa vikao vya Bunge au Kamati vinapokuwa vinaendelea au kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa Spika au kufanya kitendo chochote kwa makusudi, kudharau shughuli za Bunge au mtu anayeendesha shughuli hizo.

Aidha, wabunge waliosimamishwa wanadaiwa kuvunja kanuni ya 72 (1) na 68 (10), kwa Kusimama na kuomba mwongozo kuhusiana na jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi.

Kanuni nyingine wanayodaiwa kuvunja ni ile ya 72 (1), inayoeleza kuwa Spika atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa, utaratibu bora unafuatwa Bungeni na uamuzi wa Spika kuhusu jambo lolote la utaratibu utakuwa wa mwisho.

Pia, kanuni ya 68 (10), inasema uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa wa mwisho.

Sharti lingine wanalaodiwa kuvunja ni kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu kinyume cha kanuni ya 60 (2) na (12) ya kanuni za Bunge, jambo ambalo lilileta fujo na kuvuruga shughuli za Bunge.

Wanadaiwa kuvunja pia kanuni ya 60 (2), inayosema Mbunge yeyote hataanza kuzungumza hadi aitwe na Spika ama kwa jina ua wadhifa wake na kumruhusu kusema na wakati wa kusema ataelekeza maneno yake kwa Spika; na kifungu kidogo cha 12 cha Kanuni hiyo kinachosema, endapo spika atasimama wakati Waziri au Mbunge anatoa hotuba bungeni au atakuwa amesimama mahali pake akisubiri kuanza kuzungumza, Waziri au Mbunge huyo ataketi mahali pake na Bunge litabaki kimya ili Spika aweze kutoa maelekezo au taarifa yake.

Kingine ni kudharau mamlaka ya Spika kinyume na Kifungu cha 24 (c) (d) na (e) cha sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya kanuni za kudumu za Bunge.

Kanuni ya 74 (1) (a) na (b) inakataza wabunge kufanya vitendo vyovyote ambavyo ni utovu wa nidhamu kwa Spika au mtu yeyote anayeongoza kikao ambayo inasema Spika anaweza kutaja jina la Mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikiwa ni (a) kwa maneno au kwa vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika au, (b) Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli za Bunge au mbunge yoyote anayeongoza shughuli hiyo.

MBOWE NA DK. TULIA
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freemon Mbowe, anasema tatizo kubwa la Bunge la 11 ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

“Mara kadhaa bunge linavurugika,mipango ya bunge inavurugika, mambo yanakwenda ndivyo sivyo kutokana na kuwepo kwa huyu mtu, tujadili ajenda ya kutokuwa na imani naye na katika kutokuwa na imani siku yoyote ambayo Naibu huyu atakuwa kwenye kiti sisi tutatoka nje tumechoka kufanywa watoto wadogo kutolewa bungeni kila mara kama ni
maagizo kutoka nje ya bunge tumechoka, tunaweza kufanya siasa hata nje ya bunge,’’ anasema Mbowe.

Tayari zaidi ya wabunge 90 wameshasaini ajenda ya kutokuwa na imani na Naibu Spika.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanakosoa uamuzi wa Bunge kuwasimamisha wabunge kuhudhuria vikao vya Bunge wakihoji kama wabunge wa CCM huwa hawavunji kabisa kanuni wawapo bungeni.