Elimu itumike kuuzindua umma uthamini vyoo Zanzibar

07Jun 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Elimu itumike kuuzindua umma uthamini vyoo Zanzibar

Ukosefu wa vyoo katika jamii za kiafrika sio jambo geni .Ni tatizo kubwa ndio maana Umoja wa Mataifa ukaweka siku maalum ili kuhimiza matumizi ya vyoo kwa lengo la kujenga afya bora na kuepukana na maradhi ya kuambukiza.

Ukosefu wa vyoo katika jamii za kiafrika sio jambo geni .Ni tatizo kubwa ndio maana Umoja wa Mataifa ukaweka siku maalum ili kuhimiza matumizi ya vyoo kwa lengo la kujenga afya bora na kuepukana na maradhi ya kuambukiza.

Hata hivyo, wakati ukosefu wa vyoo bado ni tatizo kubwa suala ambalo limekuwa likijitokeza ni kwa nini ulimwengu huu unaoitwa wa maendeleo nyumba nyingi bado hazina vyoo?.Wachambuzi,wasomi na wananchi wa kawaida wamekuwa wakitoa sababu tofauti kuhusu hali hiyo inayokera katika jamii.

Watalamu wa afya wanaeleza wazi athari za kutokuwa na vyoo kuwa ni pamoja na kuenea kwa maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu yanayoendelea kutesa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.

Katika kutafuta jibu kwa nini Zanzibar yenye wakaazi zaidi ya milioni moja na laki tatu nyumba zake nyingi hazina vyoo au watu hawataki kutumia vyoo, baadhi ya wananchi wanalizunguzmia hilo kwa mitazamo tofauti

Mtazamo wa jumla kabla kuelezea mtazamo wa wananchi wenyewe ni kwamba, tatizo la utamaduni na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia afya bora ndio sababu kuu ya ukosefu wa vyoo katika maeneo mengi ya Zanzibar haswa kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba ambapo takwimu zinasema zaidi ya kaya 40,000 kati ya kaya zaidi ya 300,000 za Zanzibar nzima hazina vyoo.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa Shule ya Kijini, Zanzibar ambae pia ni mkaazi wa kijiji hicho, Ali Makame Haji ni miongoni mwa wananchi 35 wa kijiji hicho ambaye nyumbani kwake ana huduma ya choo.

Ugumu wa maisha na uelewa mdogo wa wananchi wengi katika kijiji hicho alisema kuwa, ndicho kinachosababisha kukosekana huduma ya vyoo katika nyumba zao.

Alisema huduma ya choo ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu haswa kwa manufaa ya afya na kuepukana na kujiepusha na maradhi mbalimbali yakiwemo ya mlipuko.

“ Choo ni stara nzuri kuliko kujisaidia msituni, kwani unapokuwa na choo katika nyumba yako huwa unajiskia faraja” aliweka wazi Haji.

Hiyo ni hali ya vijijini ambayo wananchi wengi hawana huduma ya choo, lakini je hali ikoje mjini Zanzibar ambapo ni eneo linalotembelewa na watalii wengi wanaofika nchini, haswa ikizingatiwa kuwa moja ya vyanzo muhimu vya kwa Zanzibar ni kutoka katika sekta hiyo ya utalii.

Kwa upande wa mjini nako hali sio shwari, kuna vyoo vingi vya Serikali vilivyojengwa tokea enzi za ukoloni ili wananchi wanaofika katika maeneo ya mjini wa Zanzibar kwa shughuli mbalimbali kuweza kujisaidia kwa stara lakini hali ni tofauti.

Tabu Haji Burhani, mkaazi wa kijini Matemwe mkoa wa Kaskazini Unguja ni miongoni mwa wakaazi 435 kati ya 400 ambao hawana vyoo kwa miaka mingi na hilo kwake ni jambo la kawaida na familia yake yenye watu 10.

“Tunajisaidia msituni hata nyakati za usiku tumeshazowea,”alisema mkaazi huyo wa kijiji cha Kijini Matemwe, na kueleza sababu kuwa ni umaskini kwa kile alichosema kuwa uchimbaji wa choo ni gharama kubwa na kipato chake ni kidogo.

Gharama za uchimbaji wa choo alisema kwamba ni kubwa na kipato anachokipata hawezi kumudu gharama hizo kwa sababu ana mahitaji mengine ikiwemo ya kulisha familia.

Burhnai anayejishughulisha na kazi ya uvuvi, alisema kuwa amezowea kwenda kujisaidia msituni hivyo haoni sababu ya kuchimba choo wakati sehemu ya kujisaidia ipo ingawa sio rasmi.

Alisema kuwa, kwa sasa hana mpango wa kuchimba choo labda siku za baadaye kwa sababu gharama hizo kwa sasa hazimudu.

“Kama huna zaidi ya shilingi laki tano, huwezi kuchimba choo kwa sababu ardhi yetu huku kijini ni ya mawe ndio maana gharama ni kubwa,”alisema.

Wananchi mwingine wa kijiji hicho ambae hana choo, Fatma Said alisema ni zaidi ya miaka kumi sasa tangu aolewe, lakini nyumbani kwake hakuna choo hivyo yeye pamoja na familia yake wanajisaidia msituni.

Alieleza kuwa, tangu ameishi maisha ya kwao katika kijiji hicho na kuingia katika maisha ya ndoa hawakuwa na choo hivyo ameshazoea kuishi maisha hayo.

“Ninaposhikwa na haja kubwa nakimbilia msituni iwe mchana au usiku nimeshazowea,” alisema Fatma mama mwenye familia ya watoto watano.

Aidha alisema maisha hayo ya kuishi bila ya kuwa na huduma ya choo sio peke yake kijijini hapo kwani hupigana vikumbo njiani na wananchi wenzake wanapoenda msituni kujisaidia.

“Wakati mwengine mimi nakwenda msituni kujisaidia wezangu wengine wanarudi hiyo ndio hali tunayoishi hapa petu tunapishana kama daladala zinapokuwa katika ruti za safari zake,”alisema.

Fatma Hamad Khamis anayeishi na wazazi wake kijijini hapo, alisema nyumbani kwao pamoja na majirani zake wote wa karibu katika eneo hilo hawana vyoo na wanajisaidia msituni.

“Sehemu ya kujisaidia kwa ajili ya haja ndogo au kuoga ipo nyumbani, lakini sehemu ya kujisaidia haja kubwa haipo.Mimi tangu nimezaliwa mpaka sasa nina miaka 19 nimeikuta hali hii na nimeshazowea,”alifafanua.

Alisema kuwa, licha ya kuizowea hali hiyo, lakini anatamani nyumbani kwao kungekuwa na choo ambacho kingekuwa kinatoa huduma zote, lakini kwa sababu ya umaskini wa kipato,wazazi wake wameshindwa kuchimba choo.

“Tunapoenda msituni kujisaidia hakuna kuchimba shimo, labda ukafanya haja yako kisha ukafukia hapana unafanya haja yako mzigo uliyouacha(kinyesi)kinaliwa na wadudu,”alisema Fatma bila ya kutaja wadudu waliopo katika msitu huo wanaokula kinyesi.

Hata hivyo alisema kuwa, hali hiyo inaweza kumsababishia kupata maradhi kwa sababu wakati anapoenda kujisaidia msituni, muda wa kujisafisha kwa maji hadi arejee nyumbani inzi hurandanranda na kujikita kwenye vinyeshi kisha huenda kutua kwenye vyombo au maji wanayotumia na kurahisisha uwezekano wa kupata magonjwa.

Aliongeza kwa kusema” tunapoenda msituni kujisaidia huwa hatubebi maji kwa sababu huwa mtu hapendi kujulikana kuwa anakwenda kujisaidia ” aliweka wazi.

Sheha wa Shehiya hiyo ya Kijini (kiongozi wa kijiji), Haji Makame Khamis alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la ukosefu wa huduma za vyoo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Alisema kijiji hicho kinawakaazi 3,350 kina nyumba 435 lakini nyumba zenye vyoo ni 35 na ambazo hazina vyoo ni 400 idadi ambayo ni kubwa.

Alisema licha ya umaskni wa kipato walionao wananchi wa kijiji hicho, pia hawana utamaduni wa uchimbaji wa vyoo katika nyumba zao na imekuwa kama ni mazowea.

“Wapo wanaona kutokuwa na choo ni jambo la mazoea maana wengine unapowapa elimu ya umuhimu wa kuwa na choo utawasikia wakisema umeona wapi kinyesi kikakaa ndani wakimaanisha kuwa nyumba inayokaa watu na kuwa na choo ndani haipendezi,” alisema.

Alieleza kuwa, amekuwa akijitahidi kuwahamasisha wananchi wake kuchimba vyoo, ili kuweza kuepukana na maradhi mbalimbali ikiwemo maradhi ya mlipuko.

Alisema kuwa, watu wawili katika Shehia (kata) hiyo wamefariki dunia kwa maradhi ya kipindupindu katika mwezi wa April mwaka huu na wote hao waliyofariki hawakuwa na vyoo na walikuwa wakijisaidia msituni.

Mwandishi wa makala hii, alizungumza na wafanyabiashara na wananchi mbalimbali ambao harakati zao nyingi za kibiashara zipo maeneo ya mjini, wanasema kuwa vyoo vya Serikali vinavyotoa huduma hiyo havipo na hata baadhi ya majengo hayo ya vyoo yamegeuzwa kuwa maduka ya biashara.

Mohammed Juma ni Dereva wa teksi, katika eneo la Darajani anasema wamekuwa wanapata usumbufu mkubwa wanapotaka kujisaidia kwa sababu eneo hilo analofanyia biashara hakuna huduma ya choo.

“Huduma ya choo ipo kule darajani, mwanzo ilipokuwa kituo cha daladala zamani na kama huna fedha huwezi kupata huduma kwa sababu lazima ulipie, kwa upande wetu sisi Waislamu tunaofanya ibada ya sala tunapoenda msikitini wakati wa sala ndio tunapata fursa ya kwenda chooni kujisadia,”alisema.

Aidha alisema vyoo katika misikiti sio muda wote vinakuwa wazi huwa milango yake inafungwa kwa kufuli, mpaka muda wa sala ndio vinafunguliwa hivyo wanapata usumbufu mkubwa.

Alisema ni aibu kubwa kwa mji wa Zanzibar ambao hutembelewa na watalii wengi kutoka nchi mbalimbali kukosa huduma za vyoo ambazo hazina usumbufu.

Rajab Salim Rajab, afisa wa afya wa baraza la Manispaa Zanzibar, alisema kuwa vipo vyoo 10 vya Serikali ambavyo vilikuwa vikitoa huduma bure kwa wananchi lakini kwa sasa vyoo hivyo vimekodishwa na vinaendeshwa na watu binafsi.

Alisema baraza la manispaa liliamua kuvikodisha vyoo hivyo kwa sababu baadhi ya vifaa vilikuwa vikiibiwa ikiwemo milango na madirisha kwa sababu ya kutokuwepo na udhibiti mzuri wa ulinzi katika vyoo hivyo na baadhi ya majengo hayo yamechakaa.

“Tukitaka tusitake mji sasa unakua lazima Serikali tuwe na vyoo vingine vitakavyotoa huduma bora kwa wananchi kama sio bure basi iwe kwa bei nafuu ili kila mwananchi anayehitaji huduma hiyo aweze kuipata,” alisema Rajabu.

Aidha alisema kuwa, harakati hizo za kujenga vyoo vingine vimeaanza na baraza la manispaa limetiliana saini mkataba na Benki ya Afrika ili kujenga vyoo 10 vipyavya kisasa katika Manispaa ya mji wa Zanzibar.

Alisema kuwa, ili choo kiweze kutoa huduma bora ni lazima kiwe na ubora, ikiwemo maji ya kutosha, kuzingatia jinsia na makundi ya pembezoni kama watu wenye ulemavu, mwanga wa kutosha, na sehemu ya kupata haja ndogo na kubwa na viwe safi muda wote.

Alisema kuwa, vyoo vilivyopo vinavyotoa huduma, havina ubora huo kwa sababu kwanza majengo yake yamejengwa miaka 60 iliyopita na uhaba wa maji katika maeneo mengi ya Zanzibar vimechangia kutokuwa na ubora na hali ya usafi sio wa kuridhisha.

Alisema licha ya uhaba wa huduma ya vyoo iliyopo katika manispaa ya mji wa Zanzibar, lakini asilimia kubwa ya wananchi hawana utamaduni wa kujisaidia katika vyoo vya kulipia.

WATAALAMU WA AFYA WANENA

Watalamu kutoka Wizara ya Afya Zanzibar walisema kuwa, tokea Septemba mwaka 2015 hadi sasa, Zanzibar imekumbwa na maradhi ya kipindupindu yaliyochangiwa na uchafu na baadhi ya nyumba kukosa huduma ya vyoo.

Mkurugenzi Kinga kutoka Wizara hiyo Dk Mohammed Dahoma, alisema wizara hiyo imefanya ukaguzi katika nyumba mbalimbali za wilaya ya Magharibi Unguja na wamebaini kuwa nyumba zaidi ya 150 hazina vyoo.

Alisema anashangaa kuona mtu anamudu gharama za kujenga nyumba, lakini anashindwa kuchimba choo kwa kisingizio kuwa umaskini wa kipato.

Alisema zaidi ya wananchi 3,000 wameugua kipindupindu Zanzibar kutoka mwezi wa Septemba mwaka 2015 hadi Mwezi huu na watu 42 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.Miongoni mwa sababu ya ugonjwa huo ni wananchi kukosa huduma ya vyoo.

Hata Ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali Zanzibar imefanya utafiti mwaka 2014 na kugundua kuwa asilimia 28.7 za nyumba zilizopo vijijini hazina vyoo na asilimia 2.0 ya nyumba za mjini hazina vyoo huku wananchi wanajisaidia katika maeneo ambayo sio salama kwa afya zao.