Mpango wa kuhakikisha kuwa kompyuta zinatumika shuleni ulianza mwaka 2000 na inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya shule zote nchini humo zina kompyuta na zimeunganishwa katika mfumo wa intaneti lengo likiwa ni kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
Elimu bora ndio ufunguo wa uchumi ulioendelea. Zana za kufundishia za kisasa, zikiwemo kompyuta ni muhimu kuhakikisha kuwa elimu bora inapatikana, hususani katika enzi hizi za dijitali Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inaibukia kila sekta iwe ya jamii au uchumi.
Serikali inataka masomo ya msingi ya kompyuta kufundishwa shuleni hususani shule za msingi lakini ni asilimia tano tu ya shule nchini zina kompyuta hivyo uelewa wa Tehama kwa shule za Tanzania umebakia kuwa ni tatizo.
Kwa kuliona hilo Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imeandaa mikakati ya kuisaidia serikali katika kuwezesha wanafunzi kujifunza Tehama kwa kuanzisha maabara ya kompyuta pamoja na kutoa kompyuta shuleni hapa nchini.
Katika hali hiyo, kampuni hiyo wiki iliyopita ilitoa msaada wa kompyuta 20 zenye thamani ya shilingi milioni 33 zikiwa zimeunganishwa na huduma ya intaneti kwa shule tatu za sekondari mkoani Mtwara.
Msaada huo ni jambo kwa namna moja au nyingine unalenga kuleta mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya elimu nchini.
Zana hizo muhimu zinahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuendeleza na kukuza mitaala ya uendeshaji wa teknolojia.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano yaliyofanyika Shule ya Sekondari Tandahimba mkoani Mtwara, Mkurugenzi wa TiGO Kanda ya Pwani, Goodluck Charles alisema,
“Msaada huu kwa shule hizo tatu ni ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuleta mageuzi katika mtindo wa maisha ya kidijitali.
Msaada huu wa leo umekuja baada ya kukabidhi kompyuta 10 kwa Shule ya Msingi Chuda mkoani Tanga na kompyuta 25 zilizounganishwa na intaneti kwa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure mkoani Mwanza mwaka jana.
“Msaada kwa shule ya Sekondari ya Kutwa ya Masasi, Tandahimba na Siho ni kielelezo cha kweli cha uwekezaji wa TiGO katika miradi tofauti yenye mchango kijamii kupitia mkakati wetu wa kuwekeza kijamii unaowezesha jamii kupokea zana za kisasa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika nyanja zote za kijamii ikiwemo sekta ya elimu,” alisema Charles.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego aliyehudhuria tukio hilo alizitaka sekta binafsi kuisaidia serikali katika mikakati yake ya kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule nchini.
Dendego alisema, “Naipongeza Tigo kwa ukarimu wao wa kuzisaidia shule hizi; natoa wito kwa watu binafsi, kampuni za biashara na wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya elimu.”
Akipokea msaada huo kwa niaba ya wakuu wenzake wa shule za sekondari, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandahimba Messi Andililo alisema kwamba, kompyuta hizo zitawawezesha wanafunzi kuwa na uelewa wa kiteknolojia hata kuwawezesha kuipata teknolojia ya habari mapema katika elimu yao.
“Tunafurahi kwa hatua hii ya Tigo; tuna matumaini kwamba kompyuta hizi zitawaweka wanafunzi wetu katika ngazi moja na wenzao wa shule nyingine zilizoko maeneo ya mjini na duniani kwa ujumla,” alisema Andililo.
Uongozi wa shule na wanafunzi wanaonufaika na ufadhili huo walipata mgawanyo sawa wa kompyuta zilizotolewa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Sino, Mtwara wakati akipokea kompyuta hizo alisema, “Wanafunzi wetu wamezoea kupata mada mbalimbali za kielimu kutoka katika chanzo kimoja; hivi sasa hali haitakuwa hivyo tena baada ya kupokea kompyuta hizi 20 watakuwa na chanzo kingine acho kitawawezesha kupata habari yoyote kwa wakati wowote, tunaamini hili litaongeza kiwango cha mafanikio katika shule zetu.”
Nasma Sadiki ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Sino alielezea kufurahishwa kwake akisema, “Nilifurahi mno niliposikia kwamba shule yetu itapokea kompyuta hizi kwa kuwa hivi sasa ninaweza kutafuta somo lolote ninalotaka kupitia Google, nikalihifadhi na kulisoma wakati wowote kwa ajili ya kufanya rejea ya masomo yangu.
Mwanafunzi mwenzake ambaye yupo kidato cha tatu Twahiri Seleman naye aliunga mkono maoni hayo akisema, “Tumekuwa tunapambana kupata mada nzuri za masomo baada ya mwalimu kutupatia kazi za kufanya; aidha unaazima mada hizo kutoka shule nyingine au unalazimika kurudi kumwona mwalimu na kumuuliza maswali ili kupata habari zaidi, lakini sasa itakuwa ni rahisi kupata habari kuhusu masomo tunayotahiniwa kwayo kutoka katika kompyuta hizi zilizo na intaneti.
Meya wa mji wa Mtwara Godfrey Mwanchisya akizungumza katika kuhitimisha tukio hilo alisema, “Ukosefu wa walimu wa hisabati na masomo ya sayansi kumekuwa kunatupasua vichwa watu kama sisi tuliopo kwenye nafasi za umma.
Ninaamini kompyuta hizi zitatoa jibu la haraka kwa uhaba huu wa walimu. Halikadhalika, tunamatumaini kwamba zitaziba pengo la kiteknolojia na hatutakuwa na tatizo tena kwa wanafunzi wetu kushindwa katika masomo haya, na mwisho tunaamini kuwa wahandisi wa baadaye watatoka Mtwara.”
Kama alivyobainisha meya, shule za Tanzania zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinazuia kiu yake ya kupiga hatua katika Tehama.
Hizi ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu, kompyuta, walimu walio na uelewa katika Tehama, kukosekana kwa vitabu wa Tehama, jengo la kudumu kwa ajili ya kompyuta pamoja na kukosekana kwa kipaumbele kwa elimu ya Tehama.
Kwa hiyo ufadhili kama huo uliofanywa na Tigo utaweza kuzisaidia shule kupata mwangaza wa kutumia teknolojia katika njia ambayo itaongeza pale ambako hakuna mtaala wa Tehama.










