Vigogo wazidi kufuzu safari ya Gabon

06Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Tanzania
Nipashe
Vigogo wazidi kufuzu safari ya Gabon

MISRI na Senegal wamefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon baada ya kushinda mechi zao za mwisho wa wiki.

Winga wa timu ya Roma, Mohamed Salah alifunga mara mbili wakati Misri ikiifunga Tanzania mabao 2-0 na kuwawezesha Waarabu hao kupata tiketi ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010.

Senegal nayo imefuzu kwa michuano hiyo, shukrani kwa mabao kutoka kwa wachezaji wawili wanaocheza soka Ligi Kuu England, Sadio Mane na Mame Biram Diouf na kukamilisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burundi iliyokuwa ikicheza uwanja wa nyumbani.

Pamoja na kutokuwapo kwa nahodha wa Al Ahly, Hossam Ghaly aliyetemwa na kocha raia wa Argentina, Hector Cuper, Misri ilipata ushindi ugenini na kuiacha Tanzania nje ya matumaini hata kama watashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Nigeria.

Mabingwa wa mara saba Afrika - Misri walikuwa wakihitaji sare tu ili kufuzu kwa michuano hiyo baada ya kuikosa kwa miaka mitatu mfulilizo.

Salah alifunga bao la kwanza kwa mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja nyavuni dakika moja kabla ya mapumziko.

Tanzania wangeweza kusawazisha bao hilo kama mshambuliaji wao wa kimataifa Mbwana Samatta hasingekosa penalti aliyoipaisha juu ya lango.

Salah aliihakikishia ushindi Misri kwa kufunga bao la pili kipindi cha pili.

Winga wa Southampton, Sadio Mane alipeleka mbele Senegal kwa kufunga bao la kwanza katika dakika ya 16, kabla ya mshambuliaji wa Stoke City, Mame Biram Diouf kufunga bao la pili dakika chache kabla ya mapumziko.

Simba hao wa Teranga, wameshinda mechi zao zote katika kundi lao na kufikisha pointi 15, huku Burundi inayoshika nafasi ya pili ikikusanya pointgi sita tu.

Katika mechi nyingine, Namibia iliifunga Niger 1-0, huku bao pekee likipachikwa nyavuni na Peter Shalulile katika dakika ya 15.

Ushindi huo unaendelea kuipa matumaini ya kumaliza nafasi ya pili, huku Niger ikipotea kabisa kwenye mbio hizo.
Guinea-Bissau walisogea jirani kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kuwafunga 3-2 mabingwa wa mwaka 2012, Zambia.

Zambia sasa ina wakati mgumu wa kumaliza angalau katika nafasi ya pili.

Uganda walisogea jirani kufuzu kwa michuano hiyo baada ya kuifunga Botswana 2-1 katika mechi waliyocheza ugenini

Kundi D.
Mabao ya Uganda yalifungwa na Luwagga Kizito na Khalid Aucho, huku lile la wenyeji likipachikwa kwenye kamba na Onkabetse Makgantai.

Kundi C,
Mali waliichapa Sudan Kusini mabao 3-0, mabao yakifungwa na Abdoulay Diaby, Mobido Maiga na Mousa Doumbia.

Sierra Leone wamebakisha pointi moja kuwafikia kwenye msimamo mabingwa watetezi, Ivory Coast baada ya kuifunga Sudan bao 1-0 lililowekwa kwenye kamba na Sheka Fofanah.

Matokeo mengine
Kundi G
Tanzania 0-2 Misri
(Misri wamefuzu)
Kundi E
Guinea-Bissau 3-2 Zambia
Kundi K
Burundi 0-2 Senegal
(Senegal wamefuzu)
Kundi C
Sudan Kusini 0-3 Mali
Kundi H
Rwanda 2-3 Msumbiji
Kundi I
Sierra Leone 1-0 Sudan
Kundi D
Botswana 1-2 Uganda
Kundi M
Gambia 0-4 Afrika Kusini.