Simba SC, Yanga viwango vinatisha

29Jan 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Simba SC, Yanga viwango vinatisha
  • Timu hizo kongwe zaidi katika ligi ya Bara kwa pamoja na zimefunga magoli 27 na kuruhusu mabao sita katika mechi zote 15 zilizocheza mwaka huu. Yanga na Simba.

Vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga wanafukuzana vikali mwaka huu. Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kumalizika mwezi huu, timu hizo zinatisha kwa mabao.

Ikiufungua mwaka kwa ushindi wa bao pekee la Ibrahim Ajibu mjini Mtwara, Simba imecheza mechi nane mwezi huu ikishinda sita dhidi ya Ndanda (1-0), URA (1-0), JKU (1-0), Mtibwa Sugar (1-0), JKT Ruvu (2-0) na Burkinafaso (3-0), sare moja dhidi ya Jamhuri FC (2-2) na kupoteza moja dhidi ya Mtibwa (1-0) visiwani Zanzibar.

Wanajangwani wao wamecheza mechi saba mwaka huu, wakishinda tano dhidi ya Mafunzo (3-0), Mtibwa (2-1), Ndanda (1-0), Majimaji (5-0) na Friends Rangers (3-0) na kutoka sare mbili (ndani ya dakika 90) dhidi ya Azam FC (1-1) na URA (1-1 kabla ya Yanga kulala kwa penalti 4-3).

Katika mechi zote nane, Simba hawakupata kadi nyekundu, huku wakipewa penalti moja iliyofungwa na Mganda Hamis Kiiza katika ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu.

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Bara nao hawajapata kadi nyekundu katika mechi zote saba walizocheza mwaka huu, ingawa timu mbili zilizocheza dhidi yao (Azam na Mtibwa) zilipata kadi nyekundu (John Bocco upande wa Azam na Henry Joseph wa Mtibwa).

Yanga pia ilipewa penalti mbili katika mechi hizo saba, tuta la Mfungaji Bora wa ligi ya Bara msimu wa 2013/14, Amissi Tambwe likigonga besela katika mechi yao ya penalti mbili dhidi ya Ndanda FC kabla ya fundi wa penalti Kelvin Yondani kuwanusuru siku hiyo.

Tangu mwaka huu uanze, wachezaji 10 wa Yanga wamefunga mabao 16 ya timu yao katika mechi zote za mashindano. Nyota na mabao yao kwenye mabano ni Tambwe (4), Donald Ngoma (3) na Simon Msuva (2).

Wengine ambao kila mmoja amefunga bao moja ni Paul Nonga, Malimi Busungu, Issoufou Boubakar, Yondani, Thaban Kamusoko na Matheo Anthony.

Wachezaji sita ndiyo waliofanikiwa kufunga mabao 11 ya Simba mwaka huu. Wakali hao wa kufumania nyavu na idadi ya magoli yao kwenye mabano ni Kiiza (4), Awadh Juma (2), Ibrahim Ajibu (2), Jonas Mkude (1), Danny Lyanga (1) na Said Ndemla (1).