Ndoa ya Yanga na TBL shakani

29Jan 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Ndoa ya Yanga na TBL shakani

Wakati mkataba wa udhamini wa klabu ya Yanga na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ukiwa umebaki miezi sita kabla ya kufikia tamati, taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa haitakuwa tayari kuendelea na udhamini na kampuni hiyo.

Msemaji wa Yanga, Jerry Muro.

Taarifa zinadai kuwa sababu kubwa ya kukwepa kuendelea na mkataba huo ni kutokana na kushindwa kukidhi mahitaji.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo bila kutaka jina lake kuandikwa, alisema TBL wanatoa Sh. milioni 35 kila mwezi kwa ajili ya mishahara, wakati mishahara ya mwezi ni zaidi ya Sh. milioni 90.

"Hata hizo fedha za mishahara kutoka TBL hazifiki kwa wakati, huu ni usumbufu heri kutafuta wadhamini wengine," alisema mpasha habario huyo.

Msemaji wa Yanga Jerry Muro, aliliambia gazeti jana kuwa kuna vikao vya kujadili udhamini vinaendelea ndani ya klabu hiyo.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro inayodhamini klabu hiyo, Pamela Kikuli alisema hawana taarifa na malalamiko ya Yanga na kuwataka viongozi wa klabu hiyo kuwasiliana nao kama kuna tatizo.