Shule hiyo ilijengwa mwaka 1928 iliko Manispaa ya Tabora hivi sasa na iliitwa African Girls School, ambayo ilikuwa mahususi kwa ajili ya ajili ya watoto wa kike wa machifu wa kiafrika.
Kimsingi mfumowa elimu wakati huo, uligawanywa katika madaraja matatu, ikianza na watoto wa kizungu ambao walipata elimu bora zaidi katika shule zao, wakifuatiwa na Wahindi na wa mwisho walikuwa Waafrika.
Shule hiyo kwa sasa inajulikana Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora (Tabora Girls Secondary School) ina umri wa miaka 88 imetoa mchango mkubwa wa kuibua vipaji vya kitaifa na kimataifa.
Miongoni mwa wahitimu wake, saba kati yao wamekuwa mawaziri wa Tanzania na wawili majaji katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pia wamo wakuu wa mikoa, mabalozi, wanadiplomasia wa kimataifa na watendaji waandamizi katika taasisi za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) na wasomi waliowahi kushika chaki katika hadhi ya uprofesa katika vyuo vikuu.
Katika mchango huo wa wana-Tabora Girls nao hauko nyuma katika sanaa ya burudani ya muziki wa dansi kitaifa na mpira wa pete.
Katika nafasi ya kipekee, wake wa viongozi waandamizi nchini, marehemu Sofia Kawawa, Anna Mkapa mke wa Rais wa Mstaafu Benjamin Mkapa na Janeth Kahama mke wa Waziri Mstaafu Sir George Kahama, mmoja wa mawaziri wa kwanza wa serikali huru ya Tanganyika na baadaye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini leo hii shule hiyo inapofanyiwa tathmini, iko hoi kwa mengi ikiwemo taaluma, kwa kutoshika tena nafasi za juu katika mitihani mbalimbali,kama ilivyozoeleka pamoja na kaka zao katika manispaa ya Tabora; Tabora Boys na Milambo.
Wana Tabora Girls walivyotikisa
Tangu zama za kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika, jina Sofia Kawawa, mke wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TFL), Rashid Kawawa, ni kubwa sana katika siasa ya nchi.
Kawawa ambaye baada ya uhuru ameshika nyadhifa mbalimbali katika uongozi wa Taifa kama vile Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Waziri Mkuu, Makamu Mwenyekiti (Bara) na Katibu Mkuu wa CCM katika vipindi tofauti.
Sofia amekuwa Mwenyekiti wa Umojawa Wanawake wa TANU, moja ya jumuiya muhimu zenye mchango mkubwa katika siasa za chama hicho.
Anna Abdallah;.Miongoni mwa wanawake wa kitanzania waliopata fursa za kwenda kusoma elimu ya juu (kwa wakati huo) katika ngazi ya diploma nje ya nchi na aliporejea aliteuliwa kushika nafasi mbalimbali.
Pamoja na ukuu wa wilaya, mkuu wa mkoa ,mbunge,Waziri na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (wadhifa alioutumikia hadi hivi karibuni.
Anna Mkapa;Miongoni mwa dhamana zake ni mke wa Rais wa mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) Getrude Mongella; Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni Waziri, Balozi, Katibu Mkuu wa Mkutano wa Wanawake wa Umoja Mataifa (Beijing) na Rais wa Bunge la Afrika Mawaziri;mbali na Anna Abdallah pia yupo Profesa Joyce Ndalichako,Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.Kabla ya hapo alifundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA).
Aidha yupo msomi wa uchumi Profesa Anna Tibaijuka ambaye katika baraza la mawaziri lililopita alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia Profesa Tibaijuka alishakuwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat) na mwanataaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,ambako anakumbukwa sana kwa kuasisi vuguvugu la kinamama la kuunda Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA).
Naye Dk Batilda Buriani aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na baadaye Balozi.
Magreth Sita alikuwa mwalimu na mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ambaye baadaye akawa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Celine Kombani (ambaye kwa sasa ni marehemu); alikuwa Katibu Tawala katika Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro (SUA) mbunge na Waziri wa Utumishi.
Julie Manning, aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Waziri wa Sheria na Eusebia Munuo aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Asha Baraka, maarufu kama Iron Lady ni mhitimu wa shule hiyo anayepeperusha bendera yake katika sura tofauti ya sanaa na michezo , kwani ni jina lenye nafasi kubwa sana katika maendeleo ya muziki wa dansi nchini.
Kwa sasa anamiliki bendi ya African Stars.(Twanga Pepeta).
Pia alishakuwa mchezaji maarufu wa netiboli akivaa jezi ya timu ya Bima. Na katika siasa alishafikia ngazi ya juu ya kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ametangaza nia ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.
Upeo huo wa sanaa na michezo wa Asha Baraka ulijitokeza tangu akiwa shuleni Tabora, alipokuwa mwananetiboli mahiri wa shule na Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMMISETA), hatimaye akachaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji wa timu ya mkoa wa Tabora.
Aidha katika riadha alishang’ara kufikia ngazi za juu mbio za mita 100, kabla ya kumaliza shule mwanzoni wa miaka ya 1980 alipoajiriwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Historia ya Tabora ( kielimu)
Historia ya mkoa wa Tabora katika sekta ya elimu inajengwa na uwepo wa shule kongwe zilizoanzishwa wakati wa ukoloni kwa lengo la kutoa elimu kwa watoto wa Watemi wa kijadi (Chiefs).Shule hizo ni Tabora Girls na Tabora Boys
Tabora Girls inayotimiza miaka 88 mwaka huu ni shule pekee ya wasichana mkoani Tabora iliyokuwa na jukumu la kutoa elimu ya kuwaandaa wafanyakazi wataalam wa kada mbalimbali.
Tabora Girls’ ilianzishwa mwaka 1928 ikijulikana kwa jina la "African Girls School" chini ya umiliki wa Serikali ya kikoloni ya Uingereza maalumu kwa ajili ya watoto wa kike wa machifu wa kiafrika.Ilikuwa shule ya msingi yenye darasa la kwanza hadi la nne.
Mwaka 1957, ilipewa hadhi ya kuwa sekondari ya wasichana Januari 4 mwaka 1968 ilisajiliwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mara ya kwanza walianza masomo yao. Mwaka 1972 ilianza kusajili wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi (albino) na wasioona
Aidha Novemba 12, 1968,Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliweka jiwe la msingi la bwalo la shule hiyo.
Ujenzi huo ulifadhiliwa na SIDA ukiwa na dhumuni la kuongeza usajili wa watoto wa kike katika shule hiyo.
Maendeleo ya shule
Kaimu Mkuu wa shule hiyo Mathias Lubatula anasema shule hiyo imepitia hatua mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya kijeshi, mafunzo ya watoto wenye ulemavu na vipaji maalum.
Mwaka 1972 Tabora Girls’ ilisajili wanafunzi wa mwanzo wa kike wasioona ili kuwapatia elimu maalum.
Lubatula anasema mwaka 1985 ilianza usajili wa wanafunzi wa kike kutoka Zanzibar.
Usajili wa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (Albino ) ulianza mwaka 2003 na mpaka sasa kuna wanafunzi Albino 22 na wasioona 17.
Mafunzo ya kijeshi
Mwaka 1970, Tabora Girls ilianza kutoa elimu na mafunzo ya kijeshi hadi miaka ya 1990 yalipositishwa na kuendelea kuwa shule ya watoto wenye vipaji maalumu kitaaluma.
Lubatula anasema, “lengo la mafunzo ya kijeshi lilikuwa kuwaandaa wanafunzi kuwa raia wazalendo kwa kutoa mbinu, maarifa na ujuzi wa kuilinda nchi yao.Lengo hilo lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kwani wanafunzi waliandaliwa ipasavyo kuwa wakakamavu, kutochagua mazingira ya kufanya kazi na waliitumikia nchi yao kwa moyo mmoja.”
Kaimu mkuu huyo anabainisha kuwa, mafunzo hayo wakati yanatolewa Tanzania ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleo, maadui wa ndani na nje ya nchi na baadhi ya maeneo kutofikika kirahisi.
Lubatula anasema, “mafunzo ya kijeshi yaliweza kuwajenga kisaikolojia wanafunzi kuipenda nchi yao na kutanguliza maslahi ya nchi walipokuwa kwenye utumishi wao.”
Tabora Girls’ ilipewa hadhi ya kuwa shule ya vipaji maalum, wanafunzi wa kike waliandaliwa kuwa wataalam na viongozi.
Hadhi hiyo ya vipaji maalum iliwekwa kwenye misingi ya uwezo wa kitaaluma kwa wanafunzi wenye vipaji walipata fursa ya kujiunga na shule hiyo.
Matunda wa dhana hiyo yamechangia kuibua vipaji vingi vya viongozi wanawake katika kada mbalimbali za taaluma, uchumi na maeneo mengi
CHANGAMOTO
Umaarufu wa shule hiyo ya Tabora katika miaka ya karibuni umekwazwa na mengi ambayo ina nafasi ya kipekee katika kulinda hadhi ya shule na maendeleo yake ya taaluma.
Hadi miaka ya karibuni kulikuwa na hali mbaya ya huduma ya maji, wanafunzi kulazimika kuzagaa katika maeneo jirani ya Kariakoo na Ng’ambo ili kutafuta mahitaji hayo, hivi karibuni hatua za maboresho zilichukuliwa.
Jumuiya ya Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kusaidia kuboresha miundo mbinu ya maji,nyumba za walimu na mengineyo ikiwa njia ya kuienzi shule hiyo kwani baadhi ya maofisa na wataalamu wake ni zao la shule hiyo.
Zilifadhili ujenzi wa mabweni sita,vyumba vya madarasa 11, nyumba tatu zinazochukua familia mbili kila moja,tanki la maji na miundombinu ya umeme.
Pia Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Tabora (Tuwasa) kuchukua hatua kama hiyo mahususi kwa ajili ya maji safi na majitaka.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa shule Lubatula analalama kuwa hali si shwari kwa upande wa majengo ya mabweni,maktaba na maabara ambayo yamechakaa na katika umri wake unaokaribia karne moja sasa na hakuna ukarabati uliofanyika kwa muda mrefu sasa.
Upande wa miundombinu ya umeme baadhi ya milingoti mibovu na nyaya zimeungwa mara nyingi hivyo kuhatarisha maisha na athari kubwa kama hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo hazitachukuliwa.
Lutabala ana kilio kingine kuhusiana na kukosekana kwa uzio wa shule, jambo linalofanya watu wengi kuingilia na kumega eneo la shule ,sambamba na kuwapo matukio ya wizi,tatizo lililowahi kuikuta shule nyingine kongwe ya Pugu sekondari, jijini Dar es Salaam.
Walakini huo ulichukuliwa hatua ya ujenzi wa uzio kwa ushirikiano wa karibu na aliyekuwa mwanafunzi wao Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda ambaye sasa ni mkazi jirani na eneo hilo.
Kuhusu walimu Lubatula anasema upungufu ni mkubwa hasa kwa masomo ya Sayansi, huku shule hiyo ikiwa na mikondo mitatu ya masomo ya sayansi ngazi ya kidato cha tano na sita.ambayo ni; Fizikia,Kemia na Baiolojia (PCB);Fizikia,Kemia na Hisabati (PCM) na Kemia,Baiolojia na Jiografia (CBG).
Kaimu Mkuu huyo wa shule anasema somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambalo ni geni lakini muhimu sana katika mtaala wa elimu ya sekondari nalo halina mwalimu.
Huku akitaja upungufu huo wa watumishi wa kitaaluma na wengine wasio wa kitaaluma na anaongeza:“upungufu huo wa watumishi unachangia kurudisha nyuma ufanisi wa mambo mbalimbali .”
Anaongeza kuwa kuanzishwa kwa sekondari za kata kuna mchango mkubwa katika kupunguza safu za walimu waliohamishiwa katika shule hizo mpya kukabili upungufu wa walimu, athari yake ikawa Tabora Girls kufanya vibaya..
.Kuhusu zahanati iliyopo alisema kuwa ina upungufu wa vitanda na magodoro na wanafunzi wanapougua hulazimika kwenda na magodoro wanayolalia mabwenini.
Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kidogo kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu katika shule hiyo hali ambayo haimalizi tatizo kwa mara moja na kwa wakati.
Mwalimu huyo anasema shule pia inahitaji ukumbi mkubwa wa mikutanowa kisasa na gari kubwa aina ya lori au basi kwa ajili ya kubebea wanafunzi katika safari zao
Mafanikio:
Tabora Girls’ ina walimu 52 na wanafunzi 691 wote wanaishi bweni.Ina vitanda 92 (double decker) vilivyokarabatiwa na ukarabati mdogo wa maabara umefanyika.
Serikali imeipatia shule hiyo gari aina ya Hilux Pick up linalohudumia shughuli za utawala na huduma kwa wanafunzi.
Taaluma:
Tabora Girls’iliyokuwa miongoni mwa shule zinazoongoza nchini kwa kufanya vizuri, hali halisi ya sasa katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2015 imeshika nafasi ya 123 kati ya shule 3,452. Na kwenye matokeo ya kidato cha sita ilikuwa ya 33.
Wakimbizi:
Tabora Girls’ ilitumika pia kuwaelimisha wasichana waliokuwa wakimbizi nchini Tanzania hivyo kutoa mchango mkubwa wa kuwaandaa wataalamu wanaozisaidia nchi za maziwa makuu zilizokumbwa na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Shule za kijeshi
Serikali wakati huo iliamua kuzifanya shule zaTabora Girls, Tabora Boys(zote za Tabora) na Chuo cha Ualimu (TCC) Kigurunyembe kutoa mafunzo ya kijeshi hadi kwenye miaka ya 1990 ilipositisha mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliwawezesha wanafunzi wanapotoka katika shule hizo kwenda kujiunga na kambi za mafunzo za Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) wasifanye mafunzo ya ukuruta na badala yake waanzie daraja la juu (serviceman) kwa sababu tayari walikuwa wameiva kimafunzo.










