Mechi 7 zilizoinyima Simba ubingwa

23May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mechi 7 zilizoinyima Simba ubingwa

Kuna mechi saba muhimu zimeinyima ubingwa Simba msimu huu. Timu hiyo imekaa misimu minne sasa bila kushiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

wachezaji wa simba wakishangilia moja ya goli katika ligi.

Wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo wako kwenye simanzi kubwa kutokana na kukaa muda mrefu bila kutwaa ubingwa na kushiriki mechi yoyote ya kimataifa wakiamini kuwa klabu yao imekuwa ikiwakilisha nchi vizuri mno kila inapopata nafasi.

Kabla ya mechi ya mwisho wa ligi, Simba ilikuwa na pointi 62, Yanga ikiwa na pointi 72 ambazo tayari zimeishatangazwa kuwa mabingwa wa msimu huu 2015/16.

Hali ingekuwa tofauti kama Simba ingeshinda mechi saba, ambazo baadhi ya hizo imefungwa kizembe tu.

Iwapo ingeshinda, ingejikusanyia pointi 19 na ukichanganya na ilizonazo ingekuwa na pointi 81 kabla ya mechi ya kumaliza ligi ambazo zingeifanya kuwa bingwa hata ingefungwa mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu, na Yanga ingeshinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Majimaji.

Hizi ndizo mechi saba ambazo kama Simba ingeshinda, saa hizi hadithi ingekuwa kinyume chake.

1. Simba 0-2 Yanga

Hii ndiyo mechi ya kwanza Simba ilipoanza kuchanganyikiwa.
Ilipoteza pointi tatu muhimu kwa kufungwa mabao 2-0 Septemba 26, 2015 kwenye mechi ambayo hata wenyewe hawakuamini kama wangepoteza.

Yalikuwa ni magoli ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma yaliyoinyima pointi tatu ambazo kama ingezipata ukichangaya 62 ilizonazo, ingekuwa na pointi 65, huku Yanga pia pointi zake zingekuwa zimepungua kibindoni.

2. Prisons 1-0 Simba

Ilipoteza kizembe mechi hii, kwani baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ugenini, ikitegemewa ingeweza kupata ushindi mwingine.

Hata hivyo iliambulia kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na Mohamed Mkopi, Oktoba 21, 2015 kwenye Uwanja wa Sokoine.

Baadhi ya wanachama na klabu hiyo wanasema kuwa kocha Dylan Kerr baada ya ushindi dhidi ya Mbeya City, alitoa ruhusa kwa wachezaji wake kupumzika badala ya kuendelea kukaa kambini, kitu ambacho kiliwafanya wachezaji kwenda sehemu za starehe na matokeo yake ikapoteza mechi hiyo.

Zikichanganywa na pointi tatu za Yanga, Simba inakuwa imepoteza ponti sita ambazo zikijumlishwa na 62 ilizokuwa nazo kabla ya mechi ya JKT Ruvu ingekuwa na pointi 68.

3. Azam 2-2 Simba

Mechi hii iliyochezwa Desemba 12, 2015 ilikuwa ni moja ya zile zilizoinyima Simba ubingwa. Ilitoka sare ya kizembe kwenye mechi ambayo ilielekea kushinda, ikitawala kipindi kirefu cha mchezo.

Safu mbovu ya beki ndiyo iliyoinyima Simba ushindi. Wakati John Bocco akiifungia Azam bao dakika ya kwanza, Ibrahim Ajibu alifunga mabao mawili yaliyoifanya timu hiyo kuelekea kupata ushindi.

Goli rahisi lililofungwa na Bocco mechi ikielekea kumalizika, kuliifanya Simba kupoteza pointi mbili na kuambulia moja. Kama ingeshinda na kuzoa tatu siku hiyo, ingefikisha pointi 70 pamoja na zile sita za mechi mbili zilizopita.

4. Toto Africans 1-1 Simba

Uzembe wa beki Hassan Isihaka kushindwa hata kumuwekea mwili tu Evarist Benard ili asipige kichwa kwa uhuru, achilia mbali kuokoa mpira wenyewe, ulisababisha Simba inyang'anywe tonge mdomoni na kutoka sare ya bao 1-1, kila mtu akiamini kuwa ingeibuka na ushindi. Ilitangulia kwa bao ya Danny Lianga, mechi iliyopigwa CCM Kirumba Desemba 19, 2015.

Pointi mbili zilizopotea kwenye mechi hiyo, zingeifanya Simba kufikisha pointi 72.

5. Yanga 2-0 Simba

Ni mechi nyingine ya watani wa jadi iliyoiondoa Simba kwenye 'reli' ya kusaka ubingwa kwa kuchapwa mabao 2-0. Ilitegemea kama ingeweza kulipa kisasi.

Hata hivyo kwenye dakika ya 21, beki Abdi Banda akaonyeshwa kadi nyekundu ambayo iliwaondoa wachezaji mchezoni. Matokeo yake Ngoma na Tambwe kwa mara nyingine tena wakaharibu mambo.

Simba ilikosa pointi tatu kwenye mechi iliyochezwa Februari 20, ambayo kama ingeshinda, ukichanya na pointi ilizonazo sasa na zile ambazo ingeshinda kwenye mechi hizi saba, ingekuwa na 75.

6. Simba 0-1 Toto Africans

Ilikuwa ni Aprili 17 mwaka huu, Simba ilipozikosa pointi zingine tatu ambazo zingeweza kuifanya kuwa na jumla pointi 78 kama ingefanya vizuri mechi zote.

Ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Toto African kwa bao la Waziri 'Junior' Shentembo.

Wachezaji wa Simba walifungwa mechi kizembe, kwani hawakuonekana kabisa kama wako kwenye mchezo na makini na kile walichokuwa wakikifanya.

8. Simba 0-1 Mwadui

Ikiwa na wachezaji walioonekana kuwa wanakimbiakimbia tu uwanjani bila malengo, Simba iliambuliwa kipigo kingine cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Mwadui FC. Mechi hiyo ilichezwa Mei 7 mwaka huu, huku bao pekee likiwekwa wavuni na Jamal Mnyate.

Kama ingeshinda mechi zote hizi saba, ukichanganya pointi zake 62 ilizokuwa nazo mpaka Jumamosi, Simba ingekuwa na pointi 81 ambazo zingesababisha 'ipande ndege' mwakani.

Hata kama kati ya mechi hizi saba, ingetoka sare au kufungwa hata mechi moja tu dhidi ya Yanga, kimahesabu bado ingekuwa bingwa hata kama Yanga ingeshinda mechi ya mwisho dhidi ya Majimaji.