Wataalamu wanasema inapotafunwa kwa muda mrefu huleta tatizo sugu la kuvimbiwa na kuharibu mfumo wa kumeng’enya chakula kwa vile mirungi hukausha maji kwenye ukuta wa tumbo na pia huathiri njia ya chakula kuanzia mdomoni hadi mlango wa kutolea haja kubwa.
Mbali na kudhoofisha mwili kwa kuuzuia kusaga na kufyonza virutubisho vya chakula, huharibu na kumpunguzia mpenda mirungi hamu ya kujamiiana kwa vile kemikali za jani, zinakwamisha kiwango cha damu kuvifikia viungo na mfumo wa uzazi hasa kwa wanaume.
Kadhalika husababisha mishipa inayopeleka damu kwenye viungo vya uzazi hasa uume kusinyaa na wakati mwingine kukosa nguvu, haya ni maelezo yanayotolewa na Mtandao wa Wakala wa Kenya wa Kudhibiti na Kuzuia Matumzi ya Mihadarati (Nacada).
Taarifa zake zinaseme mirungi au miraa huusababisha mwili kuzalisha kiwango kikubwa cha mbegu za kiume hata kama mtumiaji wa jani hilo hajasisimka au kusisimuliwa kingono. Matokeo ya hali hiyo ni mbegu hizo za kiume kumwagika kama makamasi puani wakati ukiwa na mafua, bila mhusika kujizuia matatizo haya ya kiafya yanafahamika kitaalamu kama ‘spermatorrhoea.’
“Kuna wakati athari hizi zinafikia hatua mbaya kiasi cha kumfanya mtumiaji mirungu kutokwa na mbegu za kiume kwa wingi hata kushindwa kujizuia na wengine wanalazimika kuvaa vitu vya kujisitiri ili kuzuia kuchafuka ama kulowana na mbegu hizo kila wakati,” mtandao wa Nacada unaonya.
WANAWAKE
Wakati wanaume wakivuja mbegu hizo muda wote, wanawake nao wanaelezwa kuwa jani hili linapotafunwa hukausha ute unaopatikana sehemu za siri na kusababisha ukavu na michubuko na kuwa na malengelenge, vidonda na maumivu makali wakati wa kujamiiana.
Hali hii ni chanzo cha magonjwa ya ngono kama Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi (VVU), kaswende, fangasi na kisonono, maambukizi kwenye n jia ya mkojo.
Halikadhalika kutumia miraa kwa wajawazito kunasababisha mimba kuharibika kwani inazuia damu ya kutosha kufika kwenye mfuko wa kizazi na ndani ya nyumba ya mtotto.
Mtandao wa Nacada, unataja baadhi ya athari za mirungi kuwa ni pamoja na kujisikia mujarabu na kusisimka kupita kiasi. Wakati mwingine mhusika huongea sana tena bila mpangilio, anapoteza umakini na hata kushindwa kumudu majukumu na mambo muhimu.
Madereva hutumia jani hilo ili kujiepusha na usingizi ,lakini wanajiweka kwenye hatari ya kupata ajali nyingi zaidi.
HAIKUBALIKI KIMATAIFA
Pamoja na kwamba kisheria miraa ni haramu hapa nchini, huko Kenya ni zao halali, hutafunwa ili kupata hisia za kusisimka na pia huuzwa kwenye masoko ya ndani na nje kujipatia kipato kuendesha maisha.
Lakini kilevi hiki katika michezo ya kimataifa hakiruhusiwi kutumiwa , ukibainika kuwa unatumia mirungi hutimuliwa, mathalani wanaogundulika huzuiliwa kushiriki mashindano kama ya Olympic na hata Kombe la Dunia.
Mtandao wa Wikipedia unaeleza kuwa mirungi ni mimea ambayo majani mabichi na matawi machanga, hutafunwa ili kupata juisi yenye kemikali iitwayo ‘cathinone’ na ‘cathine’. Hivi ndivyo viambato vinavyofanya teja ajisikie yuko peponi ndani ya dhiki kuu ya dunia hii. Kutokana na kuipenda wapo watu huihalalisha na kuiita ‘halua’ wengine gomba au gambe.
Mirungi inapendwa jijini Dar es Salaam na kwenye miji mingine mikubwa ambako kumeibuka tabia za kupenda ulevi kupindukia kuanzia bhangi, ugoro na shisha. Pombe za viroba nazo zimekolea, lakini majasiri hawaachi za asili wanaendelea kubugia gongo na mataputapu yaliyosheheni vilabu vya mitaani (Uswahilini).
Ulevi huu wa mirungi hutumiwa na pombe za makabila kama dengelua au boha inayotengenezwa kwa miwa, huliwa pamoja na na mbege, chimpumu na kangara. Kuna madai kuwa pombe hizi huchanganywa na mbolea za viwandani au dawa za binadamu mfano, ‘tetrasaikilin’ au ‘ampisilin’ ili kuongeza ukali zaidi.
Si habari njema kwa wanaozinywa, japo hakuna aliyetafiti na kufahamu madhara yake, lakini ulevi huo una athari nyingi ambazo ni hatari kitaifa. Miraa hutafunwa kama zilivyo ‘Big G’, utafiti uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa inakuwa kama ‘chakula’ kwa wakubwa na wadogo mijini na vijijini tena ina wateja karibu kila mahali.
Katika mazungumzo na vijana wanaotafuta jani hili jijini Dar es Salaam wanadai kuwa wanaipata kwa urahisi na inasafirishwa kwa kuingizwa ndani ya kabichi na kupelekwa popote kwa vile si trafiki wala mtumishi wa mizani atakayehofia mboga hizo zikipita barabarani.
Njia hiyo pia husafirishia mihadarati.Wapo wanaoijaza kwenye matairi ya akiba na ndani ya mapapai na mbinu nyingine nyingi, hutumika kwa mujibu wa maelezo yao.
Ninachotaka kusema huu siyo wakati wa kuacha vijana ambao ni nguzo kuu ya taifa wahatarishe maisha kwa ulevi wa kila namna , serikali na wadau hawana budi kutoa elimu na kuhamasisha vijana kuacha uraibu (uteja) huu unaotishia taifa.
VIJIWE VYA ULEVI
Uchunguzi huu umebaini kuwa kuna idadi kubwa ya vijana wakiwamo mabinti ambao kazi yao ni ulevi kuanzia,viroba, mirungi, bhangi, sigara, wiski, bia na mihadarati.Wengi wanakuwa kwenye baa, wanaranda ukanda wa barabara za Shekilango ( Dar es Salaam), hasa usiku, wengine wapo kwenye klabu za usiku, baadhi ndani ya magari ya ‘tinted’ yenye muziki mzito ambayo huegeshwa sehemu wanazozijua ili kuvuta dawa, kutafuna mirungi na kulewa pombe.
Watuamia dawa hawa wengine wako kwenye maegesho ya magari kwenye ‘supamaketi’ baadhi kwenye viwanja vya vyuo vikuu na na bustani za mapumzika wakijiharibu kwa ulevi wa kila aina bila kusahau mirungi.
Kasi kwenye utafunaji wa miraa ni kubwa wameibukia vijana wanaofurahia mirungi inayozalishwa kwa wingi nchini Kenya na baadhi ya maeneo ya ukanda wa kaskazini kama Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Madereva wengi ni wapenzi wa jani hili hasa wanaoendesha mabasi ya abiria ya mikoani na mijini pamoja na malori ya masafa bila kusahau makondakta.
Wanatafuna mirungi kwa kutumia ‘viungo’ has, Big G, karanga, soda pamoja na gomba au gambe ambazo ni kama Big G kwa ajili ya kuchanganya na jani hili. Inaonyesha kuwa miraa husambaa kwa kasi na kupewa majina mengi mathalani, khat, mirra, ‘green grass’, gomba, gambe au halua ni hatari.
Habari za kimitandao zinasema miraa inapotafunwa humpa mtu ushujaa na uthubutu wa kufanya jambo bila hofu , mbinu inayotumiwa na baadhi ya wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika ambao husafirishwa umbali mrefu wakiwa wamefungiwa ndani ya malori ya makontena yasiyo na hewa.
Wahamiaji hawa njia nzima hutafuna mirungi, hawali, hawanywi, hawalali lakini kikubwa zaidi hupata ‘cathinone’ na ‘cathine’ viambato vinavyowafanya wajisikie wako peponi japo wako kwenye barabara mbovu, maeneo yenye joto, hupigwa na baridi usiku lakini wapo kwenye hatari ya kuachwa porini endapo polisi watastukia ‘dili’.
Nguvu ya mirungi huwapumbaza wakasafirishwa porini, bila kula ama kunywa wakiwaza kufikishwa Malawi ili kuvuka mpaka na kuingia Afrika Kusini wanapodhani kuna raha kama ilivyo Ulaya.










