Wakili na umuhimu wa akaunti za wateja wao

20May 2016
Denis Maringo
Dar
Nipashe
Wakili na umuhimu wa akaunti za wateja wao

LEO tutazungumzia jambo moja muhimu linalowahusu mawakili na wateja wao. Jambo hilo ni wajibu wa Mawakili kuwa na akaunti mahsusi benki kwa ajili ya kuhifadhi fedha za wateja wake.

mawakili.

Wajibu wa mawakili kufungua na kuendesha akaunti maalum kwa wateja wake zimeanishwa chini ya moja ya Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria ya Mawakili (Sura ya 341, Kama ilivyohakikiwa mwaka 2002).

Kanuni hizi zinaitwa The Advocates (Accounts) Regulations, kwa Kiswahili zaweza kutafsiriwa kama Kanuni za Akaunti za Mawakili. Kanuni hizi zimekuwepo tangu mwaka 1956 wakati zilipotangazwa katika gazeti la Serikali kupitia Tangazo la Serikali namba (G.N.) namba 207 la mwaka huo.

Kanuni ya 2 ya Kanuni hizi inaainisha kuwa wakili atapaswa kuwa na akaunti benki, lakini pia kitabu ama vitabu maalum vya kimahesabu kwa ajili ya utunzaji wa kumbukumbu kuhusiana na akaunti hizi.

Humo anapaswa kupambanua ni fedha zipi zimelipwa kuhusiana na shughuli fulani inayohusika na mteja wake, na fedha ambazo kalipwa mwenyewe.

Labda unaweza tu kujiuliza, kanuni hizi zina maana gani? Zipo sababu kadhaa, lakini iliyo muhimu zaidi ni kumlinda Wakili mwenyewe na kumlinda mteja wake.

Kanuni hizi zinamsaidia wakili kulinda heshima na maadili ya kazi yake kwa sababu zinamuepusha na vishawishi vya kuweza kutumia fedha anazolipwa ama kukabidhiwa na mteja wake mathalani katika kuendesha kesi mahakamani ama ufuatiliaji wa jambo fulani muhimu ambalo linaweza kuhusisha ulipwaji wa fedha nyingi ambazo wakili kama wakala wa mteja, aweza kulipa kunakohusika sanjari na uwasilishaji nyaraka nyingine pamoja na gharama nyinginezo kama usafiri au malazi katika kufanikisha hilo.

Tutoe mfano mdogo rahisi. Chukulia mathalani unamuajiri Wakili akusaidie kufungua kesi ya madai mahakamani, ili akusaidie ulipwe mamilioni ya fedha unayoidai mtu, kampuni, serikali au mwajiri wako.

Na katika kulitekeleza hili mkakumbushana kwamba, mashauri ya mahakaman, kuna wakati huweza kuchukua muda mrefu kusikilizwa hadi kutolewa hukumu, na bila kuhusisha muda huo kuongezeka kama kuna rufaa.

Ndiyo maana si jambo la ajabu basi kuona kesi kuchukua mwaka mzima, na si ajabu hadi hata miaka 10.

Basi labda mkakubaliana umlipe Wakili huyu sh.milioni 10 kama ada yake ya utaalamu na milioni 10 nyingine airtime katika gharama zinazohusika moja kwa moja na uendeshaji wa kesi yako: mfano ada ya kufungulia shauri mahakamani, gharama za utayarishaji nyaraka, gharama za usafiri wa kwenda mahakamani, gharama za mawasiliano ya simu, na kadhalika. Kumbuka kuwa, busara ya kumkabidhi Wakili fedha hizi za gharama za uendeshaji kesi ni kama jambo la lazima, kwa sababu litaepusha ucheleweshaji na hatari ya wewe kushindwa kesi yenyewe, iwapo mathalani mahakama inatoa wito wa kufika mahakamani au inamtaka Wakili wako kuwasilisha nyaraka au utetezi fulani ndani ya muda mfupi baada ya notisi.

Kama Wakili hana fedha kufanikisha haya na pengine ukawa umesafiri na haupatikani, basi ipo hatari ya kesi yako kukwama kutakana na ukwasi unaojitokeza hapo.

Lakini tuliangalie jambo hili kwa namna nyingine pia. Vipi kama Wakili huyu umempa fedha za kuendesha kesi yako, labda kwa mwaka mzima (kwa makubaliano ya wewe kumuongezea fedha za ziada inayojitokeza katika gharama ama yeye pia kukurejeshea fedha zinazobaki kama kesi inakwisha mapema huku fedha nyingine hazijatumika)?

Je, katika hili hakuna uwezekano wa wakili kushawishika kutumia fedha hizi kwa matumizi yake binafsi yasiyohusiana kabisa na kesi yako, mathalani, kuzinywea kilevi ama kuzitumia kuhonga?

Hili linawezekana kabisa kwa sababu Wakili ni kama binadamu mwingine, awezaye kupata vishawishi, japo tunatofautiana namna gani tunavishinda.

Ndiyo, maana basi hekima ikatumika kuwepo kwa kanuni hizi kwa Mawakili kupaswa kufungua na pia kuendesha akaunti mahsusi za wateja, kama kinga ya kumfanya akumbuke kukabidhiwa kwake amana hiyo kwa ajili ya shughuli maalum.

Basi kwa falsafa ya jambo hili utaona basi kwamba Wakili analindwa heshima yake kwa kumjengea uaminifu kwa wateja na jamii na pia kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima, likiwemo pia hasara ya yeye kupokonywa leseni yake ya biashara ya Uwakili iwapo inabainika amekuwa akifuja fedha za wateja wake.

Kwa mtaji huu huu, mteja analindwa pia kwa sababu iwapo hili linazingatiwa basi kawakawa na amani kiasi kwamba fedha yake iko salama na itatumika katika kuongeza ufanisi wa kesi aliyompa wakili kumsaidia.

Ndiyo maana basi, kifungu cha 5 cha Kanuni hizi kinamlinda mteja wa Wakili kwa kuamini kuwa hakuna fedha yoyote itakayopaswa kuchukuliwa ama kuchotwa kutoka ndani ya akaunti ya mteja isipokuwa tu iwapo (a) inahusika moja kwa moja na shughuli inayomhusu mteja huyo ama malipo kwa wakili kwa ada ama gharama anazoingia; ama (b) fedha inayopaswa kuchukuliwa na Wakili kama gharama za ufunguaji au uendeshaji wa akaunti hii ya mteja, au itokeapo fedha hiyo iliingizwa humo kupitia hundi moja iliyojumuisha fedha za Wakili na zile zinazopaswa kulipwa Wakili kwa mujibu wa Kanuni 4 (d); ama iwapo kama fedha hiyo iliingizwa humo kimakosa, kama ilivyoainishwa katika Kanuni 5 (c).

Faida nyingine katika kanuni hizi ni kumsaidia Wakili mwenyewe pia umma kwa kumfanya atunze vitabu vyenye kumbukumbu sahihi hasa linapokuja suala zima la kiasi cha mapato na suala zima la utoaji wa kodi na tozo nyingine za kiserikali.

Hata hivyo, jambo hili limeainishwa kwa kina zaidi katika sheria nyinginezo, hususani hizo za kodi.
Tuishie hapa kwa leo.

*Denis Maringo ni mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Simu: 0719270067; dnmaringo@gmail.com