Yanga ilistahili ubingwa

16May 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga ilistahili ubingwa

ILIKUWA hoi hoi, nderemo na vifijo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam pale nahodha Haruna Niyonzima alipokabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

kikosi cha yanga kikisahangilia ubingwa.

Wachezaji wa Yanga na familia zao, viongozi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo walionekana kuwa na furaha isiyo kifani kwa timu yao kuchukua ubingwa, ikiwa ni mara ya 26 tangu mfumo wa ligi ulipoanzishwa 1965 ikiitwa Ligi ya Taifa, baadaye Ligi daraja la Kwanza Tanzania Bara na hatimaye sasa Ligi Kuu.

Yanga imetwaa ubingwa msimu huu kwa kuweka rekodi mpya, ikiwa imezoa pointi nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Wakati ikiwa imebaki na mechi moja mkononi tayari imejikusanyia pointi 72, idadi kubwa ya pointi kwenye historia ya soka hapa nchini.

Rekodi ya juu ya pointi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inaonyesha kuwa iliwekwa na Simba mara mbili, msimu wa 2009/10 na 2011/12 ilipomaliza ligi ikiwa na pointi 62 kila msimu, pia Azam FC ilifanya hivyo msimu wa 2013/14 kwa kuchukua ubingwa ikiwa na idadi hiyo hiyo ya pointi.

Idadi ya pointi inaweza kuongezeka kama itashinda au ikitoka sare katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Majimaji itakayofanyika mjini Songea Mei 21.

Kwa jinsi Ligi Kuu ilivyokuwa msimu huu, Yanga ilistahili kuwa bingwa wa ligi kutokana na ilivyokuwa imejipanga kwenye kila idara.

VIONGOZI IMARA

Ubora wa Yanga unaanza kwenye uongozi wake pamoja na benchi lote la ufundi.

Ni watu wanaoonekana kutekeleza majukumu yao vyema kwa asilimia kubwa kama si mia moja. Hakukuwa na ubabaishaji, huku ukionekana kuwa karibu na timu wakati wowote ule ukitoa huduma zote muhimu zinazotakiwa ili kuwafanya wachezaji kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Pia uongozi ulikuwa ukifanya kazi kama taasisi, ukilinda pia mambo au matatizo ya ndani kutoka nje na kuchafua taswira ya klabu.

Na pale ilipoona mambo yanataka 'kuyumba' haikusita kumtikisa aliyekuwa katibu wao Jona Tiboroha ambaye aliamua kujiuzulu.

Hii ni tofauti na watani zao Simba ambao kikitokea kitu kidogo tu, basi tayari kinakuwa kimeshavuja.

Wachezaji wakicheleweshewa mishahara, tayari imeshajulikana. Mchezaji akijibishana na kocha, tayari liko mitaani.
Kulinda siri kumeifanya Yanga kuwa vizuri hata inapopanga mipango yake kwenda kama ilivyopangwa.

USAJILI MZURI

Moja kati ya vitu ambavyo benchi la ufundi la Yanga linastahili pongezi ni eneo la usajili.

Wamefanya usajili kwa kuzingatia mahitaji ya timu. Kwanza kabisa ilisajili wachezaji wenye uwezo na uzoefu.
Wachezaji wenye uwezo wa kupambana kwenye hali ngumu ili kutafuta ushindi.

Kingine cha kupongezwa ni kwamba benchi la ufundi likiongozwa na Mdachi Hans van der Pluijm kwa kuwa na kikosi kipana zaidi kuliko timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Yanga inaweza kuwa na timu mbili zinacheza Ligi Kuu kwa siku moja, kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo unaokaribiana, tofauti na baadhi ya timu ambazo ukipanga wachezaji 11 tu, waliobaki nje ni 'majanga'.

Wanaingia kwa sababu ni lazima kuwe na mabadiliko na si uwezo au kwenda kuisaidia timu.

Kwa Yanga msimu huu, ni kama kung'oa mti na kupanda mti, anayetoka na anayeingia uwezo wao unakaribiana.

Usajili bora kuliko wote ni wachezaji wa kigeni. Msimu huu Yanga imejitahidi sana kusajili wachezaji bora kabisa kutoka nje ya nchi ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walioibeba timu hiyo.

Donald Ngoma aliwaongoza Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Vicent Bossou, wamekuwa msaada mkubwa kwa timu.

WACHEZAJI

Ukiangalia jinsi wachezaji wa Yanga wanapokuwa uwanjani utaona raha.

Wakati mwingine si kwamba wanakuwa na uwezo mkubwa kuliko wapinzani wao, la hasha.

Ni ari, juhudi na moyo wa kupambana wanaokuwa nao, kana kwamba wameahidiwa kujengewa nyumba mara mechi itakapomalizika au watakaoshinda mchezo husika.

Haijulikani wachezaji wa Yanga huambiwa nini na viongozi au makocha wao, lakini ni wachezaji wenye ujasiri na moyo wa kupambana muda wote wa dakika 90.

Ndiyo maana ni aghalabu kuona wakitetereka hata kama wataanza kufungwa goli.

Hata wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanapoona timu yao imetanguliwa goli huwa hawana hofu sana.

Ni kweli, hurudisha na wakati mwingine kuongeza. Mechi pekee ambayo Yanga walishindwa kurudisha ni dhidi ya Coastal Union ilipofungwa mabao 2-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Mkwakwani Tanga.

Wachezaji wa idara zote wa Yanga wanacheza kwa kushirikiana, wakiipigania klabu yao kwa hali na mali, wanachama na mashabiki wao ambao mara nyingi huwa nao wakiwaunga mkono muda wote.

Hii imewafanya Yanga kushinda mechi ambazo wakati mwingine walikuwa wanaelekea kupoteza.

Na si kama baadhi ya timu ikiwemo Simba ambao baadhi ya wachezaji wake wanacheza kama wamelazimishwa, au kama wanaisaidia klabu na si kwamba wanalipwa na kazi hiyo.

WANACHAMA NA MASHABIKI

Simba na Yanga ndiyo timu zenye wanachama na mashabiki ambao wana uwezo wa kufanya kitu chochote kile, ili mradi tu kuhakikisha timu yao inashinda.

Msimu huu kidogo wanachama na mashabiki wa Simba wamenyong'onyea kutokana na mwenendo mbaya wa timu yao.

Kwa upande wa Yanga, kila inaposhinda ndipo inawapa hamasa wanachama na mashabiki wake kujitokeza kwa wingi kuishangilia na kuiunga mkono timu yao.

Hii imesababisha kuzidi kuwapa nguvu ya kujituma wachezaji.

Wengi wao mbali na kumiminika kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa wakiwa kwenye magari yao ya kukodi kutoka kwenye matawi mbalimbali jijini, lakini pia wamekuwa wakisafiri na timu hiyo kwenda mikoani kucheza mechi za ugenini.

Na wamekuwa wakiipigania na kuipa msaada kwa lolote lile litakalojitokeza ambalo litaonekana kuwa linaweza kuifanya timu ikose ushindi.

Ukiwa na haya yote kwenye klabu, sidhani kama unaweza kukosa ubingwa. Yanga ilifanikiwa kuwa na kila kitu msimu huu, kuanzia umoja, uongozi imara, wachezaji bora wenye nidhamu na kujua majukumu yao.
Kiukweli ilistahili ubingwa.