African Sports ambayo imebakisha mechi mbili, tayari imeshafikisha pointi 26 ambazo hazifikiwi na timu hiyo.
Ninaizungumzia Coastal Union. Moja ya timu kongwe na maarufu nchini Tanzania.
Ni moja kati ya timu chache nchini ukiondoa Simba na Yanga zilizowahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Iliwahi kufanya hivyo mwaka 1988. Na kwa kuonyesha kuwa haikubahatisha, ikapata nafasi ya kushiriki Kombe la Afrika Mashariki na Kati ambalo kwa sasa linajulikana kama Kombe la Kagame, ilifanikiwa kufika hadi fainali, michuano iliyofanyika nchini Kenya.
Coastal, iliyokuwa timu ya kutisha ilifungwa mabao 3-0 na Kenya Breweries, mechi iliyochezwa mjini Mombasa.
Timu hiyo imepanda na kushuka daraja mara mbili, kati ya miaka ya '90 na msimu wa 2007/08, kabla ya kurejea tena msimu wa 2011/12.
Lakini sasa imekuwa ya kwanza kushuka msimu huu wa 2015/16. Haijulikani itarejea tena lini.
Yoyote yule aliyeishuhudia timu hii kwenye mechi zake za Ligi Kuu au Kombe la Shirikisho FA, hawezi kukubali kuwa timu hiyo imeshuka daraja kutokana na kiwango kibovu cha wachezaji wake au uwezo mdogo wa benchi la ufundi.
Kwanza kabisa ina sifa ya kuwa na wachezaji wakongwe na wazoefu kwenye Ligi Kuu, waliowahi kuzichezea klabu mbalimbali kubwa nchini kama Simba, Yanga na Azam FC.
Baadhi ya nyota hao ni Abasirim Chidiebere, Miraji Adam, anayechezea kwa mkopo kutoka Simba, Abdulhalim Humud, Ally Ahmed 'Shiboli' na Ibrahim Twaha.
Na katika kuthibitisha hilo, Coastal ndiyo timu pekee iliyoweza kuzifunga timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Yanga na Azam FC.
Ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Mkwakwani, Coastal iliinyuka Yanga mabao 2-0 na kuidunga Azam bao 1-0.
Pamoja na kufungwa mechi zote mbili za Ligi Kuu na Simba, lakini Coastal iliichapa timu hiyo magoli 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Kila mmoja anakumbuka jinsi refa Abdallah Kambuzi alipokuwa 'nyota wa mchezo' kwenye mechi ya nusu fainali ya kati ya Coastal dhidi ya Yanga.
Coastal ilifungwa kwa utata wa uamuzi mbovu wa refa huyo alipokubali magoli yote ya Yanga yaliyoonekana kuwa hayakuwa sahihi.
Pamoja na kwamba ilifungwa mabao 2-1, lakini mwamuzi alifungiwa kwa kuvurunda mechi hiyo.
Hii yote ni kuthibitisha kuwa timu hiyo kama ingepata malezi mazuri, mshikamano wa wanachama na mashabiki wote wa klabu hiyo, isingeshuka daraja.
Kama ilikuwa na uwezo wa kuzifunga Simba, Yanga na Azam, sidhani kama ingeweza kushindwa kubaki Ligi Kuu au kutetemesha ligi mzima kama wote wangekuwa kitu kimoja.
Klabu hii inatafunwa na mgororo uliozuka wakati wa uchaguzi uliofanyika mwaka jana.
Ubaguzi wa kutengwa kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakiongozwa na Nassor Bin Slum ambaye naye aliamua kujiweka kando na kudhamini baadhi ya timu, zikiwemo Mbeya City na Ndanda FC.Hali hii unaweza pia kuiita ubinafsi.
Waswahili wanasema umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, Coastal ikaanza kukumbwa na matatizo ya timu kukosa huduma muhimu na 'baya' wachezaji kukosa mishahara ambayo kwa kiasi kikubwa ilisababisha wachezaji wapoteze morali.
Baada ya hali kuwa mbaya zaidi ndipo baadhi waliokuwa viongozi wakaanza kurudishwa, lakini tayari mambo yalikuwa yameshaharibika.
Ni sawa na kuacha kumtibia mgonjwa wakati bado hajazidiwa, lakini matibabu yanaanza wakati hali yake imeshakuwa mbaya kupita kiasi.
Ubaguzi na ubinafsi ndiyo ugonjwa ulioiumiza Coastal na mpaka sasa inatutoka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tunaweza kusema imefikia hatua hiyo kutokana na matatizo ya viongozi wao.
Tunachoweza kukifanya ni kuiombea mema inakokwenda. Kwaheri Coastal. Timu iliyowahi kutoa wachezaji wengi wazuri na bora kwenye timu ya taifa (Taifa Stars).
Tulikupenda, lakini Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara imekupenda zaidi. Ubaguzi, ubinafsi umekuponza.










