ikimaanisha kwamba tukio ambalo linanatokea kwa muda huu nchini Marekani hata mtu aliye katika bara la Afrika nchini Tanzania, anaweza kulishuhudia wakati huo huo.
Lakini matumizi haya nchini yamekithiri kiasi cha kusahau kuwapo kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kwani kuna picha mbaya na matukio yasiyofaa ambayo yanawekwa katika mitando hiyo kupitia simu za mkononi.
Kwa ujumla Facebook, Whatsapp, Twitter, Instagram, blogu za kijamii na mitandao mingine inatumika vibaya na kupoteza utu wa binadamu.
Kwa sasa iwapo kuna ajali imetokea au mauaji ya ukatili, mara moja utakuta makundi ya mitandao hiyo yanaanza kuwa bize kwa kutumwa na kupokea picha ambazo hazipendezi machoni, pia zinaleta msisimko na sononeko kubwa kwa watumiaji wa simu za mkononi.
Pia zipo picha zinazoonyesha watu wakiwa utupu, ama watoto na wanawake waliofanyiwa ukatili na kuwekwa katika mitandao au video kupitia You Tube.
Hivi karibuni wanaharakati wa utetezi wa haki za binadamu nchini, hususan watetezi wa wanawake na watoto, wametoa tamko la pamoja kukemea vitendo vinavyodhalilisha na kukiuka utu wa binadamu, kupitia mitandao ya kijamii, simu za mikononi na katika baadhi ya vyombo vya habari.
Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya watu wasio na taaluma au wasiofahamu maadili kuhusu upashanaji na utoaji taarifa, habari kwa jamii kutumia vibaya mitandao hiyo.
Kwa mfano kuna sheria ambazo zinakataza mtoto aliye chini ya miaka 18, kuonyesha sura yake au kutajwa jina hadharani kwani ni kinyume cha sheria hiyo.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imekataza kutuma picha ya mtoto au kutoa taarifa zake ili kulinda usalama na maslahi ya mtoto, familia na jamii kwa ujumla.
Aidha, matukio hayo yanayowekwa katika mitandao hiyo, yanakiuka haki ya mtu kuthaminiwa kwa faragha pale anapokuwa hai au akiwa amefariki, haki ambayo ipo kikatiba katika ibara ya 16 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Wanaharakati hao wanasema matukio ya picha hizo pia, hujenga dhana ya kunyanyapaliwa katika jamii kwa muathirika ama waathirika wanaokumbwa na matukio hayo na kisha kusababisha kujiua.
Matukio yasiyofaa yaliyosambazwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni ni pamoja na miili ya mama na mtoto waliouawa Bagamoyo Mei 4, mwaka huu ambazo zilionyesha majeraha ya kutisha baada ya kufanyiwa unyama.
Nyingine ni za mauaji ya watu saba wa familia moja.
Pia paliwekwa picha ya mwanamke aliyefia kwenye nyumba moja ya wageni Kimara, na picha ya mwanamke akiwa utupu anayesemekana kuwa ni msukule aliyekutwa kwenye kisima cha maji maeneo ya Kibamba, jijini Dar es Salaam.
Haya ni matukio machache kati ya mengi ambayo yanadhalilisha utu wa binadamu kupitia mitandao ya simu za mkononi, hivyo mamlaka husika zinapaswa kulisimamia hili na kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria zilizowekwa.
Pia inatakiwa ifike wakati jukumu la uhabarishaji jamii libakie kwa walio na taaluma hiyo, waliokwenda vyuoni na kupewa mafunzo ya namna ya kuchukua habari ikiwamo upigaji picha kwa kufuata kanuni, taratibu na maadili ya taaluma.
Upigaji picha na kurekodi matukio katika jamii kwa kutumia simu za mkononi kwa mtu yeyote anayemiliki kifaa hicho, kisha kutuma katika mitandao bila ya kujali kanuni na sheria za mitandao vinadhalilisha jamii, licha ya kuwa pia ni kosa la jinai.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








