Kituo cha mabasi lango la Hospitali Mwananyamala kiangaliwe

15May 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe
Tuzungumze kidogo
Kituo cha mabasi lango la Hospitali Mwananyamala kiangaliwe

LICHA ya kituo hicho kuwarahisishia watu wanaokwenda kutibiwa au kuangalia wagonjwa wao kwenye hospitali hiyo, lakini kimekuwa kero kubwa kwa wagonjwa na wafanyakazi.

Bila shaka lengo la kuwekwa kwa kituo hicho karibu na hospitali ni kuwasaidia watu wanaokwenda kutibiwa au kuangalia wagonjwa. Hata hivyo, matumizi yake yamegeuka kero kubwa kutokana na madereva wa daladala kutozingatia taratibu.

Madereva hao wamekuwa wakiegesha magari yao katikati ya lango kuu la kuingilia hospitalini hapo bila kujali wagonjwa wanaoingia au kutoka hasa wale wanaowahishwa kupata matibabu.

Magari yanayotaka kuingia kwenye hospitali hiyo hulazimika kusubiri daladala hizo kuchukua abiria wanavyotaka wenyewe na wapigadebe wamekuwa wakipiga kelele kuwaita abiria bila kujali eneo hilo ni la wagonjwa.

Waliojenga barabara hiyo, wametenga sehemu ya kituo cha daladala ambacho kiko hatua chache kutoka lango kuu la kuingilia, lakini madereva hao wamekuwa waking’ang’ania kupandisha na kushusha abiria kwenye lango hilo.

Kuna wakati mwingine hata magari ya kubeba wagonjwa yanayowahisha wagonjwa hospitalini hapo hukwama kuingia kwa sababu ya kuzuiwa na daladala hizo.

Kero nyingine ni eneo hilo la hospitali kuzongwa na wafanyabiashara wa kila aina na kufanya barabara kuminywa na kusababisha mtu anayetoka upande mwingine kushindwa kupita hadi gari lingine litakapopita.

Mara nyingi madereva wa daladala wamekuwa wakikaidi sheria za barabarani, kwa kukwepa kuegesha kwenye vituo walivyotengewa.

Ukitoka kwenye kituo cha hospitali hiyo, mbele kuna njia panda inayoelekea kwa Komakoma na ile inayoelekea Mwananyama B. Eneo hilo limekuwa kero kubwa kutokana na madereva wa daladala kuegesha mabasi hayo wakisubiri abiria.
Kinachoshangaza, mbele tu ya kona hiyo, kimetengwa kituo cha daladala tena cha kujinafasi, lakini madereva hao wameng’ang’ania kuegesha katikati ya kona huku wakijua wazi kuna magari mengine nyuma wanayoyazuia kupita.

Licha ya kupigwa marufuku kuegesha katika kituo hicho, wameendelea kukaidi na wakati mwingine askari wa usalama barabarani, wanakuwapo eneo hilo bila kuwachukulia hatua yoyote.

Kutokana na vituo vingi kukwepwa na madereva hao, wafanyabiashara ndogo ndogo wameamua kuvigeuza sehemu za kuuzia biashara zao.

Kuna ile methali inayosema mvunja nchi ni mwananchi. Ukiangalia vituo vingi visivyo rasmi vimeanzishwa na sisi abiria kwa kusimamisha magari hayo sehemu yoyote tunayojisikia kusimama kwa uvivu wa kutembea hadi kwenye kituo rasmi.

Ukichunguza, vituo vingi visivyo rasmi vilivyopewa jina la msaada ndivyo vimegeuzwa kuwa rasmi na vile vilivyo rasmi vimegeuzwa sehemu za kufanyia biashara.

Pamoja na abiria kujengewa vituo hivyo vyenye kuwakinga kwa jua na mvua, lakini wako radhi kupigwa na jua ili mradi basi lisimame pale abiria anapopataka yeye.

Nikirudi kwenye kituo cha basi kilichopo Hospitali ya Mwananyamala, nilimsikia mmoja wa wafanyakazi wa hospitali hiyo akilalamika usalama wa maisha yao na wagonjwa.

Amelalamika kuwa madereva wa daladala hawajali watu wanaotoka na kuingia hospitalini, bali wanachojali ni kuchukua abiria hali inayosababisha kero kwa wagonjwa na ndugu zao wanaokwenda kuwajulia hali.

Kwa mujibu wa taratibu, eneo lolote la hospitali halitakiwi kuwa na pilikapilika au kelele za aina yoyote kwa kuwa wagonjwa wengine wana ugonjwa wa mshituko ambao unaweza kuwasababishia madhara.

Lakini cha kushangaza, eneo hilo la Hospitali ya Mwananyamala limezungukwa na biashara ya kila aina na wafanyabiashara hao wakijiona kama wako sehemu sahihi ya kufanyia biashara zao.

Hali hii ikiendelea kuachwa inaweza kusababisha hatari si tu kwa Hospitali ya Mwananyamala bali hata hospitali nyingine zenye vituo vya daladala karibu.

Ingawa baadhi yetu tunaona ni sawa daladala hizo kuendelea kupandisha na kushusha abiria kwenye vituo visivyo rasmi, lakini tukumbuke kuwa kuna siku kama si ndugu zetu basi sisi wenyewe tutahitaji kukimbizwa hospitalini kupata matibabu halafu tukakumbana na kikwazo hicho cha kuzuiwa na daladala.
bbandawe@hotmail.com; Simu: 0774 466571