Stewart Hall umeongea kweli kuhusu soka la Tanzania

14May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Stewart Hall umeongea kweli kuhusu soka la Tanzania

Mwishoni mwa wiki ijayo, Ligi Kuu Bara itafikia tamati baada ya kuchezwa miezi tisa. Pongezi wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam kwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.

Lakini pia, Nipashe tunaona ipo sababu ya kuzipongeza timu nyingine zilizoshiriki ligi hiyo, tukiamini zimepitia changamoto nyingi hadi kufikia sasa pamoja na kwamba baadhi zimeshuka daraja.

Hata hivyo, wakati tukizipongeza timu hizo kwa safari ndefu ya kushiriki ligi, kuna mambo kadhaa yalifanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kupoteza utamu mvuto, ushindani na utamu wa ligi yenyewe.

Kocha wa timu ya Azam FC, Stewart Hall ametoa hoja, ambazo sisi kama wanamichezo hatuwezi kuziacha zipite bila kuzijadili.

Kimsingi, TFF kama taasisi iliyobeba dhamana ya kuratibu na kusimamia mchezo wa soka nchini, haiwezi kukwepa lawama za Hall.

Kocha huyo raia wa Uingereza, katika hoja zake amedai kuwa soka la Tanzania haliwezi kuendelea kutokana na kuendeshwa katika mfumo wa ubabaishaji wenye dhamira ya kutetea masilahi ya watu binafsi.

Hall ambaye anaachana na Azam baada ya kumalizika msimu, anadai kuwa TFF imekuwa kiini cha kuvuruga soka la Tanzania kutokana na kuendeshwa na viongozi waliokosa dira.

Amedai kuwa hawezi kuendelea kubaki kwenye soka la Tanzania kwa sababu, kufanya hivyo ni sawa na kupoteza muda.

Siyo nia yetu kujua kujadili sababu hizo, lakini Nipashe tunadhani Hall ana hoja za msingi hasa kwa kuzingatia ligi ilivyoendeshwa msimu huu.

Kama kuna msimu ambao ligi yetu ilitawaliwa na manung'uniko na malalamiko mengi, basi msimu huu umevunja rekodi.

Karibu kila mdau wa michezo hasa soka, katika namna fulani amelinyoshea kidole na kulikosoa shirikisho hilo kutokana na mwenendo mbovu wa usimamizi wa ligi kuwahi kutokea katika miaka ya karibuni.

Ligi yoyote inayotawaliwa na malalamiko mengi, inaweza kuwashawishi wadau kukosa imani na viongozi wao.

Kosa kubwa la TFF msimu huu ni kuruhusu malalamiko mengi kuelekezwa kwao kutokana na namna wanavyoshughulikia baadhi ya mambo yanayoletwa mbele yao kwa ajili ya kuyafanyia uamuzi.

TFF imeshindwa kusimama kwenye mfumo mzuri wa usimamizi wa soka ndiyo maana mambo mengi yamekuwa yakiamriwa katika staili ya kuzima moto.

Upanguaji ovyo wa ratiba za mechi za ligi kuu usio na ulazima, umesababishwa michuano hiyo kupoteza taswira ya ushindani.

Lakini pia tuhuma dhidi ya waamuzi ni kidonda kikubwa, ambacho hakuna mdau wa soka hajawahi kuilalamikia TFF.

Tiketi za kielektroniki kwa ajili ya kuingia viwanjani ni tatizo lingine kubwa lilisoiacha TFF kwenye kapu la lawama
Ucheleweshaji wa kutoa uamuzi kutokana na malalamiko mengi yaliyopelekwa TFF ni jambo lingine kubwa linalotafsiri mfumo mbaya wa uongozi.

Haya yote, kocha Hall anayaona kuwa kiini chake ni uongozi mbovu TFF unaojali zaidi ulindwaji wa masilahi ya watu binafsi.

Tunaungana na wadau wengine waliochoshwa kuendelea kushuhudia mfumo mbovu wa usimamizi wa soka unaofanywa na baadhi ya viongozi waliokosa dira.