Balozi Kuwait: Nimejitolea kudhamini uchimbaji visima vya maji Kimara

12May 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Balozi Kuwait: Nimejitolea kudhamini uchimbaji visima vya maji Kimara

KUWAIT ni miongoni mwa nchi zilizomo katika orodha ya wanaosaidia miradi mbalimbali nchini.

Hii ndiyo hali halisi ya adha ya maji katika kata ya Kimara, jijini Dar es Salaam. (PICHA NA MTANDAO)

Miongoni mwa maeneo yanayonufaika ni katika sekta za elimu, afya, miundombinu, kilimo na uwekezaji katika ustawi wa uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi wa Kuwait nchini, hiyo ni sehemu ya kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Wiki iliyopita katika Kata ya Kimara, iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al –Najim, alitangaza rasmi kuwa Mlezi wa Kata hiyo, kutatua changamoto mbalimbali zinazowkabili wananchi wake.
Balozi huyo anasema alifikia uamuzi huo, baada ya kufahamishwa rasmi na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea.
Hatua ya kwanza, ilianzia kwa wakazi kwa kupokea ombi la wakazi wa Mtaa wa Golani waliochimbiwa kisima chenye kina cha mita 90 ili kuwahudumia wakazi 12,000.

Baada ya ujenzi wa kisima, Balozi Al Najim aliambatana na mbunge Kubenea, kukizindua rasmi.

Alipofika na kuona hali halisi, alifanya mazungumzo rasmi na wakazi, Balozi Al Najim na alieleza kuguswa na kuamua kuwa mlezi wa Kata yote ya Kimara na si Mtaa wa Golani pekee yake.

Mbunge Kubenea baada ya kuona Balozi huyo ameguswa na shida ya maji katika eneo hilo, alimweleza kwamba tatizo hilo halipo Golanio pekee, bali sehemu kubwa ya Ubungo inakabiliwa na tatizo hilo.

Baada ya maelezo hayo, Balozi Al Najim aliahidi nchi yake itashughulikia tatizo hilo. Anafafanua:

“Nilipoambiwa kuhusu tatizo la maji Golani, sikufikiria kama ni kubwa kiasi hiki. Lakini, nimejionea mwenyewe na wakati nikishangaa hapa, mbunge wenu akaniambia hivi ninavyoona hapa, ndivyo ilivyo karibu asilimia kubwa ya jimbo lote la Ubungo.

“Ninaamini kwamba maji ni muhimu katika maisha ya binadamu. Sasa ninashindwa kuelewa tatizo ni nini hadi mnapata shida namna hii.

“Mimi naomba nishirikiane nanyi kutatua tatizo hili. Nitahakikisha kata hii inapata maji ili muondokane na tatizo hili. Kukosa maji kunaweza kusababisha hata mkapatwa na matatizo mengine.”

Anasema katika kukabiliana na tatizo hilo, nchi yake imejitolea kuchimba visima vya maji katika Kata ya Kimara, pamoja na kusaidia miradi mingine.

WAKAZI WA KIMARA

Bahati Juma ni mkazi wa mtaa huo wa Golani, anayesema kuwa tatizo la maji katika eneo lao limekuwa sehemu ya kila siku, kwa kuwa umekuwa wimbo wa kudumu.

Anasema, hata mbunge wa sasa alipoahidi kulitatua hawakuamini.

Bahati anasema tangu ahamie eneo hilo baada ya kujenga nyumba mwaka 2010, alikuta maji ni ya kununua, ya chumvi wanauziwa kwa ndoo moja Sh.300 na ya bomba Sh.500, ambayo upatikanaji wake ni wa shida.

“Wakati mwingine tunaletewa maji ya miferejini ambayo si salama, lakini ukiangalia shida uliyonayo unalazimika kununua hivyo hivyo angalau ya kusaidia hata kufulia na kufanyia usafi,” anasema Bahati.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Golani, Laurent Mtoi, anataja katika changamoto mbalimbali zilizopo katika maisha ya Kimara, tatizo la maji ndilo limekuwa likiwatesa zaidi.

Anasema viongozi wa eneo hilo wamekuwa wakifanya jitihada kumaliza changamoto hiyo kwa kuzungumza na mamlaka zinazohusika na huduma ya maji, lakini hawakufanikiwa.

Mtoi anaeleza imani yake kwamba tatizo hilo sasa linaelekea ukingoni baada ya Kuwait kujitolea kusaidia.

Mbunge Kubenea anaelekeza pongezi zake kwa Balozi wa Kuwait, kwa kujitolea kuingilia kati tatizo la maji katika eneo hilo.

“Mimi na ubalozi wa Kuwait tuna uhusiano wa muda mrefu. Hivi karibuni nilikutana na Balozi na tukawa tunazungumza masuala mbalimbali, lakini nikamdokezea kwa kuogopaogopa kuhusiana na tatizo la maji, akaniambia ataliangalia.

“Baada ya siku chache nikaambiwa kwamba niwaonyeshe eneo lenye tatizo zaidi, tunashukuru Mungu wametusaidia na wameahidi kuendelea kutusaidia na kumaliza tatizo hili kabisa kwa Kata ya Kimara,” anasema Kubenea.

“Wamenisaidia kupunguza mzigo kwa asilimia kubwa, maeneo mengine yaliyobaki katika jimbo langu nitaendelea kupambana mpaka pale nitakapohakikisha tatizo la maji Ubungo linabaki kuwa ni historia,” anasema
Ikumbukwe tatizo la maji jimboni Ubungo ni sugu ana limekuwa likipigiwa kelele na wananchi wake.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika, ambaye sasa ni mbunge wa Kibamba, anasema wakati mwingine alilazimika kuandamana na wananchi wake kwenda kufikisha malalamiko katika mamlaka husika.

Pia hali hiyo ndiyo aliilekeza kwa mawaziri husika, kupitia hija binafsi bungeni kuhusu shida ya maji Ubungo
Wakati kuna hali hiyo kuna mipango mkakati inayotekelezwa kutoka vyanzo vya Ruvu Chini, mkoani Pwani.