Nimeamua kutumia methali hii kutokana na vishindo vya utumbuaji majipu vinavyoendelea Tanzania bara, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli; na namna ulivyoathiri utendaji wa Zanzibar.
Tangu kuapishwa kwa Rais Magufuli na kuahidi kusafisha serikali ya Muungano na kuja na msemo wa utumbuaji majipu ukiwa na maana ya uwajibikaji, kupambana na ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma, utendaji umekuwa gumzo siyo tu Bara bali hadi Zanzibar.
Wafuatiliaji katika utekelezaji wa mambo serikalini wanaona umeleta faida na kuimarisha utendaji.
Kutokana na hali hiyo, Wazanzibari wamekuwa na shauku kubwa ya kutaka Rais wao afuate njia hizo hizo, wakidai kuwa kunamajipu makubwa zaidi kuliko ya Tanzania bara ambayo bado hayajashughulikiwa kwa muda mrefu.
Makundi mbalimbali yamekuwa yakitoa ujumbe katika mikutano rasmi na katika mitandao ya kijamii ya kumtaka Dk. Ali Mohamed Shein kufuata nyayo za Dk. Magufuli.
Makundi hayo ya watu yamekuwa yakimtaka Dk. Shein kuanza kuyatumbua majipu yaliyopo karibu yake ambayo yanaleta kero kwa wananchi.
“Majipu yaliyopo karibu yako yameshaiva tena wala hayana kazi kubwa katika utumbuaji ukisema uyaanze kuyashika tu yanatumbuka jinsi yalivyoiva,” kauli hiyo aliambiwa Dk. Shein wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi, alimtaka Dk. Shein, kuanza haraka kazi ya utumbuji majipu na kuyatoa moyo ili yasiwapo tena.
Aidha, alimtaka pia ajiandae vilivyo na dawa nyingine za kushughulikia maradhi mengine yaliopo serikalini kwani mengine yamezidi hatua ya majipu.
“Kunaukurutu, mapele na hata madonda ndugu ambayo yanahitaji dawa,” alisema Khamis katika maadhimisho hayo mbele ya Dk. Shein.
Kwa upande wake, Dk. Shein ambaye anaiyongoza Zanzibar kwa kipindi chake cha mwisho kwa mujibu wa katiba, alisema atayatumbua majipu yote yaliopo serikalini.
Alisema majipu hatoyaacha yatambae na wala hatokubali majipu yamkaribie kwani yapo baadhi ya majipu yamevuka kiwango cha majipu na yamekuwa makumri.
“Vijipu uchungu na majipu yenyewe hayanishindi kuyatumbua nia na mwelekeo wa serikali katika kipindi hiki cha pili ni kubana matumizi yasiokuwa ya lazima, watakaofanya dharau katika uamuzi huu ndio yatakuwa majipu ya mwanzo kuyatumbua,” alisema Dk. Shein.
Alisema Serikali itadhibiti na kuzuia safari za nje na ndani za kikazi zisizo za lazima, semina, kongamano na mikutano inayofanywa kwa kutoa posho wakati wa saa za kazi, itawekewa utaratibu mpya.
“Nimebaini katika kipindi kilichopita viongozi wanaomba safari, wanaomba mialiko waalikwe ili wapate kusafiri, kwa kipindi hiki cha pili cha uongozi wangu hayo hayatokuwapo maana fedha zenyewe ni chache hivyo ni vyema kuzitumia kwa maslahi ya wananchi,” alisema.
Alisema waliopewa dhamana ya kuziongoza idara mbalimbali za Serikali watapaswa watekeleze wajibu kwa kuwasimamia wafanyakazi walio chini yao na kama hawatawawajibisha wafanyakazi wao, basi watawajibishwa wao.
Dk. Shein alisema katika kipindi hiki, atahakikisha kwamba Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inafanya kazi ipasavyo ili viongozi wote waliotajwa katika sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanatangaza mali zao kwa mujibu wa sheria hiyo.
Alisema kila kiongozi atatakiwa atekeleze wajibu wake kwa wakati uliowekwa katika kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi na kwamba Serikali haitomvumilia yeyote atakayebainika kubeza na kutaka kuzirudisha nyuma jitihada za Serikali yake.
Aidha, Dk. Shein alisema lazima watendaji wawajibike katika utendaji kazi na kufuata sheria za uwajibikaji na taratibu za kazi za utumishi wa umma.
Aliwataka watendaji wa umma kufanyakazi ya kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo na mtendaji yeyote ambaye anaogopa kuwatumikia wananchi atamuondoa kazini.
“Wafanyakazi wafahamu kuwa mshahara ni matunda na tunzo mtu anayopata kutokana na juhudi aliyoifanya katika uzalishaji,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya watu wamejenga tabia ya kudai mishahara mikubwa na kuilaumu Serikali kuwa haipandishi mishahara bila ya wao kuwa na ari na dhamira ya kweli ya kujitahidi kufanya kazi na kuzalisha.
Alisema ni lazima watumishi wa umma wabadilike na kuondoa tabia ya kufanyakazi kwa mazoea akifafanua kuwa viwango vya utendaji na nidhamu kazini bado havijaongezeka sana.
“Ni jukumu letu tufanye kazi kwa bidii na tuipende kazi... wapo baadhi ya wafanyakazi ambao hawapendi kufanyakazi kwa vitendo vyao na wengine hawataki kufanyakazi, lakini wao ndio wa mwanzo wanaotaka mishahara mikubwa, posho nzuri, safari za kila wakati na kuhudhuria kwenye semina na mikutano kila mara,” alisema Dk. Shein.
Alisema watumishi wa umma wa namna hiyo huwavunja moyo wananchi na kuwafanya waichukie serikali yao bila ya sababu za msingi.
“Wafanyakazi wenye sifa mbaya nilizozielezea katika kipindi hiki tutawachukulia hatua watakapobainika na kama hapana budi tutawafukuza kazini…hatuwezi kuwa na wafanyakazi wasio nidhamu.”
Hata hivyo, alisema atahakikisha utumbuaji majipu unazingatia taratibu na sheria za serikali na namna ya kuwashughulikia watumishi wa umma kuwa na uhakika wa jambo ili isiwe kigezo cha kuwaonea.










