Kuna jasiri wa kurudisha 80% ya maoni ya wananchi kwenye Katiba?

11May 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
Kuna jasiri wa kurudisha 80% ya maoni ya wananchi kwenye Katiba?

PAMOJA na mabilioni ya fedha yaliyotumika kukusanya maoni, kuandika rasimu zote mbili hadi kuzalisha Katiba inayopendekezwa, matumaini ya Watanzania kuipata yameendelea kuyoyoma siku hadi siku.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju.

Tunakumbuka kwamba baada ya lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba kutoa nakala ya Katiba inayopendekezwa Oktoba mwaka 2014, wachambuzi kadha wa kadha walifanya uchambuzi na kuainisha kwamba wajumbe walizingatia asilimia 20 tu, ya maoni ya wananchi.

Kwa lugha nyingine ni kwamba Bunge Maalum lilitupa asilimia 80 ya maoni ya wananchi yaliyokuwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba ambayo ilitolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba.

Kujibu swali hilo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine (Saut), Prof. Mwesiga Baregu, anasema: “Hili ndilo swali au changamoto kubwa inayoikabili Tanzania hivi sasa.”

Anasema kinachoweza kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwaandaa wananchi na kuwarudisha kwenye mchakato wa Katiba kwa kuanzia kwenye rasimu ya pili.

Hata hivyo, anasema wasiwasi uliopo ni kwamba kwa utendaji wa sasa, jambo hilo ni gumu. “Kwa sababu Magufuli (Rais John Magufuli), anataka aonekane yeye ndiye mbadala wa Katiba ndio maana ameikwepa kabisa Katiba hadi sasa,” anasema. Anasema:

“Ni kwamba tumerudi kule tulikokuwa kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katibahaijaundwa. Tunakwenda kwenye utendaji wa mtu mmoja badala ya kujenga mfumo imara wa uongozi kama nchi.

” Anasema tatizo la Tanzania ni mfumo mbovu wa utawala kwa kuwa ukiwapo, kiongozi yeyote akiingia madarakani atalazimika kuuzingatia.

“Anachokifanya (Rais Magufuli), ni kutafuta huruma ya wananchi na ndio maana utamsikia akisema wananchi wamuombee…anataka wananchi walie.

Ambacho angeweza kufanya ni kuwapatia Katiba nzuri,” anaongeza Prof. Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

“Hataki kugusa Katiba kwa sababu anaonekana ni mtu asiyetaka kuwa na mipaka…anataka aingie kwenye mihimili yote.” Aidha, akiwasilisha bajeti bungeni wiki iliyopita, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema serikali imedhamiria kukamilisha mchakato wa Katiba kwa kuziwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufanya kazi hiyo.

Pia, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaeleza kuwa mchakato wa Katiba utaendelea pale ulipoishia kwa maana kwamba chama kitaielekeza serikali kuhitimisha kura ya maoni.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Wachambuzi wanaeleza kuwa Katiba inayopendekezwa ilitupa asilimia 20 ya maudhui ya rasimu ya pili huku ikiweka masharti yasiyotekelezeka kwa mtu anayetaka kuwa mgombea binafsi.

Pia wanaeleza namba muundo wa Muungano unavyoiweka Zanzibar pabaya zaidi, kumomonyolewa kwa madaraka ya Bunge kuisimamia Serikali na kutupwa kwa maadili.

Kwa ujumla, Katiba inayopendekezwa na ina mambo mengi yenye utata na ambayo hayawezi kuleta mabadiliko ya maana ambayo yalitazamiwa na wananchi wengi.

Katiba inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk. Mohamed Shein, Oktoba 04, mwaka 2014, baada ya Bunge Maalum la Katiba kumaliza kazi ya kujadili Rasimu, ilielezwa kwamba imezingatia kwa asilimia 81.8 maoni ya Rasimu ya Tume na asilimia 19 ndiyo imetokana na BMK.

Hata hivyo, Jaji Warioba aliwahi kupinga maneno hayo akieleza: “Kama ukihesabu Ibara unaweza kufikia hitimisho hilo, lakini hili siyo suala la Ibara bali ni mambo muhimu yaliyo katika Rasimu.”

MAPENDEKEZO YA TUME YALIYOTUPWA NA BMK

Mapendekezo hayo kuwa nimaadili, mamlaka na madaraka ya wananchi kuwajibisha viongozi wao, mgawanyo wa madaraka, muundo wa Muungano, malengo muhimu ya kitaifa, Haki za Binadamu na Utawala na mgombea huru.

Maadili ambayoyalikuwa ni mapya yalikuwa katika sura ya tatu, Ibara ya 13 hadi 20, lakini yote yalikataliwa na BMK. Rasimu ya Tume ilipendekeza katika sura ya tatu Ibara ya 13 ikieeleza miiko ya Maadili na Miiko ya Uongozi ikielezea madaraka aliyopewa kiongozi wa umma, dhamana ya uongozi na heshima kwa kiongozi wa umma, mwenendo wa kiongozi wa umma awapo kazini, kazi binafsi na kwenye jumuiko.

Mengine ni kiongozi akipewa zawadi wakati akitekeleza majukumu yake itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na atatakiwa kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi ikiwa na mchanganuo.

Mengine ni kiongozi wa umma kutoruhusiwa kumiliki akaunti ya benki nje ya nchi isipokuwa kwa namna sheria za nchi zinaruhusu, kuomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.

Pia, kutangaza na kuwasilisha ndani ya siku 30 baada ya kupata na kuacha uongozi, mali na thamani yake na madeni yake kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.

Kiongozi wa umma hatashiriki katika kufanya maamuzi kwa jambo au shughuli yoyote ambayo ana maslahi nayo yeye binafsi, familia na rafiki, kutoruhusu kutumika kwa mali ya umma zikiwamo zilizokodishwa kwa serikali kwa madhumuni ya kujipatia yeye au mtu mwingine manufaa na kwamba Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA INASEMAJE?

Katiba inayopendekezwa chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa kamati ya uandishi, Adrew Chenge, ilipendekeza katika sura ya nne, Ibara ya 27 na 28, ikiondoa masuala ya iwapo akipewa zawadi na kutaka sheria itoe maana ya zawadi au aina, thamani, kiwango na uhifadhi wa zawadi.

Katiba hiyo imeondoa ibara ya kiongozi wa umma hatafungua au kumiliki akaunti nje nchi na kuomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanahusisha hadi au heshima ya utumishi wa umma.

Pia BMK liliondoa Mamlaka na Madaraka ya wananchi kuwawajibisha wabunge wao viongozi wao kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye Ibara ya 129. Ibara hiyo ilikuwa inawapa nguvu wananchi haki ya kumwondoa Mbunge wao madarakani endapo atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake, kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la Uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi.

MGAWANYO WA MADARAKA Rasimu ilipendekeza mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge na serikali kwa maana ya Rais na Bunge, kwa kufanya Rais asiwe sehemu ya Bunge, lakini BMK liliyaondoa.

Pendekezo hili la wananchi lilikuwa kubwa kwa maana Mawaziri wasingetokana na wabunge na Rais hatakuwa sehemu ya Bunge.

MAZURI KWENYE KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Mambo mazuri ambayo yalipendekezwa na yakakubalika ni malengo muhimu ya kitaifa, Misingi ya Mwelekeo wa shughuli za serikali na sera ya kitaifa, ambayo ni sura iliyopo katika Katiba ya 1977.

Tume iliweka ufafanuzi mzuri kwa kuainisha malengo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na mzingira. Kingine ni malengo ya kisiasa ambayo ni kuzuia, kuondoa dhuluma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa na mambo mengine.

Uchumi pia ni miongoni mwa mazuri yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa lengo likiwa ni kuimarisha vyama vya ushirika,kuchakata bidhaa za kilimo, ufugaji, uvuvi na madini na kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya shughuli zao.

Kijamii nihifadhi ya jamii hasa kwa wasiojiweza, wazee, watoto na watu wenye ulemavu na kutoa nafasi ya elimu na huduma za afya kwa wote ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi salama.

Hata hivyo, mazuri hayo hayatakuwa na matokeo yoyote ya maana kwa kuwa kuna kipengele kinachozuia upatikanaje wake. Hii ni kwa sababu hayatatiliwa nguvu kisheria.

Hivyo kilichofanywa na BMK ni kutoa kwa mkono huu na kuchukua kwa mkono mwingine. Aidha, Tume yenyewe ilipendekeza kuwa,masuala hayo yatakuwa ni mwongozo kwa serikali katika kuandaa sera na kufanya mipango ya utekelezaji na itatoa taarifa Bungeni mara moja kila mwaka.

Tume ni Haki za Binadamu ziliboreshwa zaidi na ni eneo linaloonekana kuwa bora zaidi kwenye Katiba inayopendekezwa ikiwamo haki za wazee, watoto, wanawake na watu wenye ulemavu, vijana na wafanyakazi.

MADARAKA YA RAIS

Wakati wa kukusanya maoni ya wananchi, nafasi ya Rais na madaraka yake ni mambo yaliyozungumzwa sana wakitaka yapunguzwe kwa kuwa ana madaraka mengi.

Ilipendekezwa kuwa badala ya Rais kuchaguliwa kwa wingi wa kura, apate zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kuonyesha anaungwa mkono na wengi.

Pia Katiba ya 1977 hairuhusu matokeo ya Urais kuhojiwa mahakamani, lakini katiba inayopendekezwa imeruhusu na wanaoweza kuhoji ni wagombea wa nafasi hiyo wa vyama vingine.

Katika hili, BMK lilikubali mapendekezo ya Tume kuwa Rais awe na madaraka katika ngazi ya Taifa na viongozi wa chini ziachiwe Tume za Utumishi, Mahakama na Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, pendekezo la Tume la kutaka baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kama Mawaziri, Manaibu Waziri, Jaji Mkuu, Wenyeviti wa Tume mbalimbali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wathibitishwe na Bunge, lilikataliwa na BMK. Badala yake, madaraka ya Rais kuteua mtu yeyote kushika nafasi fulani kwa jinsi anavyoona yako pale pale.

Kwenye rasimu ya pili, wananchi walipendekeza Tume Huru ya Uchaguzi na kuweka Kamati ya uteuzi ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu na sifa za watu wanaoweza kuwa wajumbe wa Tume ziliwekwa wazi na ikifika wakati wanaomba kuwa wajumbe, kamati ya uteuzi ndiyo itawachuja na kumpelekea orodha kwa Rais.

Katika hilo Jaji Warioba alikaririwa akisema kuwa: “Tulifikiri ni muhimu kwa sababu inatoa uwazi wa uteuzi na wabunge ndiyo wa wakilishi wa wananchi, tulifikiri kwa vyeo vizito anayeteuliwa awe anapata Baraka za wananchi ili asijisikie ni mteule wa rais bali ana Baraka za wananchi, lakini kwa kuacha hivyo wataendelea kujiona ni wateule wa Rais.”

MGOMBEA BINAFS

I Katiba inayopendekezwa ni kama ilikataa mgombea binafsi kutokana na masharti ambayo ni magumu yenye nia ya kuzuia wasiwepo wagombea huru.

Kwa mujibu wa Katiba inayopendekezwa, Ibara ya 140 inaweka sifa za mtu kugombea Ubunge, awe raia aliyetimiza miaka 21, anajua kusoma na kuandika lugha za Kiingereza na Kiswahili, ni mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au Mgombea huru.

Licha ya masharti hayo, Katiba inayopendekeza imeweka masharti maalumu kuhusu Mgombea binafsi ambayo ni“Bunge litatunga sheria ambayo itaweka masharti ya Mgombea huru, ambayo ni kwanza, kuhusu idadi ya watu watakaomdhamini.

Sharti jingine ni kipindi ambacho atakuwa amekoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kwamba kwa kusema hivyo ni lazima mgombea awe kwanza mwanachama wa chama cha siasa.

Jingine ni asijiunge na chama cha siasa akiwa kiongozi na aainishe utaratibu ambao utampati mapato nje na ndani ya nje, kwa ajili ya gharama za kampeni na kuweka wazi Ilani yake.

Wadadisi wanaeleza kuwa hayo ni msharti ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kuyafikia. Wanahoji, je, kama mtu anataka kugombea kuwa mwenyekiti wa kitongoji ni lazima awe na ilani au atokane na chama cha siasa? Pia, kwanini mashatri ya fedha yawe kwamgombea binafsi tu na siyo kwa wote?

MWENYEKITI WA KAMATI YA UANDISHI

Siku ya kukabidhi Katiba inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema asilimia 81.8 ya Ibara za Katiba inayopendekezwa zimetokana na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema ibara 42 hazikufanyiwa marekebisho, ibara 200 zilifanyiwa marekebisho ya kiuandishi na maudhui, ibara 29 ambayo ni sawa na asilimia 10.7 zimefutwa na ibara 54 ambayo ni sawa na asilimia 18.2 za katiba inayopendekezwa ni mpya kutokana na mapendekezo ya wajumbe wa BMK.

“Rasimu ilikuwa na sura 17 ibara 271 na nyongeza moja iliyoanisha mambo saba ya Muungano, Katiba inayopendekezwa ni 19 ibara 296 na nyongeza tatu,” alifafanua Chenge.