Nikataja misingi ya ndoa ikiwamo, kumfanya Mungu kuwa kiongozi wa ndoa na pia Mawasiliano. Leo nikumegee msingi mwingine ambao ni Upendo na Kujitoa.
Maisha ya ndoa ni safari ndefu, anasema Mtumishi wa Mungu, Nabii B.G.Malisa, kiongozi mkuu wa kanisa la Ukombozi, kwenye kitabu chake cha ‘Mwanamke Jitambue’. Kanisa hili liko Skanska, Tegeta DSM.
Anaongeza kuwa upo wakati mtafurahi na wakati mwingine mtalazimika kulia.
Wakati mwingine wanandoa watapishana katika maamuzi. Upo wakati maisha yaweza kutetereka kiuchumi. Kuna wakati mnaweza kugongana kimawazo.
Mmoja anaweza kuugua. Hapo ndipo upendo wa kujitoa unatakiwa kudhihirika kwa kila mmoja. Maisha Ndivyo Yalivyo!
Ndoa hii itaweza kusimama tu pale wanandoa watakapokuwa na upendo wa kujitoa kama vile Kristo alivyolipenda kanisa.
Pia Mungu alionyesha upendo wake kwa kumtoa mwanae wa pekee ili afe kwa ajili yetu. Yohana 3:16, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.
Katika nyakati hizi tunazoishi, yamekuwepo matatizo makubwa sana ya ndoa na nyingi ziko katika hatua ya kufa. Wanandoa wengi sana leo wameshazifungasha ndoa zao na kuzitupa mbali kabisa.
Wanawake na wanaume wengi sana leo wanajitahidi kutafuta mbinu mbadala za kujiridhisha wao wenyewe, kwa kuwa wameshindwa kabisa katika ndoa zao. Wasomi wengi leo, wafanyabiashara, maprofesa, wanasiasa, watu wenye majina makubwa duniani hawajafanikiwa katika eneo hili la ndoa.
Wapo wanasaikolojia ambao wameacha wake zao, jambo ambalo linaonyesha kuwa elimu yao ya kisaikolojia haijawasaidia kuishi vizuri na wake zao. Ukweli ni kwamba tunahitaji msaada wa ki-Ungu(msaada wa Mungu) ili tujinasue na tatizo hilo. Ni jambo linalosikitisha tunapojiuliza kama watu wa Mungu wanakumbwa na masahibu hayo, je, wale wa mataifa wasiomjua Mungu wala hali gani?
Kama wakristo wa leo wanashindwa kupata amani, ushindi na mafanikio katika ndoa zao, je, wale wasiokuwa na uhusiano mzuri na Mungu wana hali gani?
Eneo hili la ndoa siyo la kupuuzia, hivyo ni lazima tutafakari na kulitafutia jawabu kwani linawatesa watu wengi. Pindi tutakapogundua chanzo cha matatizo ya ndoa, ni dhahiri tutapata msaada kutoka juu kwa MUNGU, utakaobadilisha maisha yetu ya ndoa. Katika eneo hili tunahitaji hekima ya Mungu kwani hekima ya kibinadamu haiwezi kutatua matatizo haya.
Hebu tizama andiko hili la kibiblia: Ayubu 32:9, “Sio wakuu walio wenye akili, wala sio wazee watambuao hukumu”. Kwa mantiki hiyo, mtu aweza kuwa na tatizo kubwa lakini akashindwa kupata msada kutoka kwa Mungu aliyeumba mbingu na nchi.
Suluhu ya matatizo ya ndoa huanza pale tu mtu anapomruhusu Mungu kuingilia kati tatizo hili la ndoa. Hakuna tatizo la ndoa linaloweza kumshinda Mungu. Yeremia 33:27, “Tazama mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je, Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?” Hapa Mungu anadhihirisha kuwa yeye ni muweza wa vyote.
Watu wengi ambao wamefanikiwa katika ndoa zao walianza na matatizo makubwa sana wasiyoyatarajia. Na watu wa aina hii wanao uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa katika ndoa zao. Tatizo ni kwamba wanadharau huo uwezo (kuleta mabadiliko) ulio ndani yao.
Kwa hiyo, wengi wamekata tamaa wakati walitakiwa kuongeza bidii kuita neema ya Mungu ishuke juu ya ndoa zao. Mungu atabadilisha matatizo yako kuwa muujiza na ushuhuda wako utawatia nguvu maelfu.
Wengi wamepoteza mwelekeo katika eneo la ndoa. Baadhi waliotarajia kufaulu eneo hili, ndio kwanza wanapambana. Wengi wamepoteza fedha, fursa na wadhifa kwa masuala haya ya ndoa.
Wengi sana leo wamechanganyikiwa, maana wanakumbana na maadui zao kila kona, wanashambulia biashara zao, familia zao na jamii zao. Wanajiuliza; je, nina tatizo gani? Kitu gani kinaendelea katika maisha yangu? Mbona nimeombewa sana makanisani na kuungama? Mbona bado nateseka kwenye ndoa? Kwanini nateseka? Jawabu tafuta neema ya Mungu uondokane na matatizo katika ndoa yako!
Niishie hapa.
Wiki ijayo mada zitajikita kwenye vyanzo vya matatizo ya ndoa! Je, ndoa yako iko salama?Ukiwa nalo jambo kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz

.jpg?itok=nfwjwDzv)









