Katika mechi hiyo dhidi ya Yanga, mwamuzi wa mchezo Abdallah Kambuzi alilazimika kumaliza mchezo kabla ya muda baada ya hali ya usalama kuwa tete.
Hadi mechi hiyo inavunjika, Yanga walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-1 ndani ya muda wa nyongeza baada ya timu hizo kumaliza dakika tisini za mchezo zikiwa sare ya bao 1-1.
Kama wanamichezo, tunaipongeza TFF kwa uamuzi wa kuipiga faini Coastal Union kwa niaba ya mashabiki wake.
Lakini pia uamuzi wa kumfungia kuchezesha soka kwa mwaka mmoja mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo, ni jambo lingine tunalounga mkono.
Lakini hata hivyo, tunadhani adhabu hizi ni ndoto kulingana na aina ya vurugu zilizofanywa na mashabiki hao kiasi cha kusababisha hata mwamuzi msaidizi kuumizwa vibaya karibu na jicho baada ya kupigwa na jiwe.
Kuipa faini ya Sh. milioni 2 klabu ya Coastal Union ni kama utani kulinganisha na madhara yaliyotokea kwenye mchezo huo.
Tunadhani, adhabu hiyo haiwezi kuwa alama ya kuzuia kufanyika vitendo hivyo tena. Adhabu hiyo haiwezi kukomesha tatizo.
Kuiadhibu timu peke yake na kuwaacha mashabiki, hakuna maana. Kwamba, wataendelea kufanya vurugu kwa vile adhabu hiyo haiwaumi hata kidogo.
Nipashe tunadhani, TFF ilipaswa kutoa adhabu kali kwa kila mhusika badala ya kutoa adhabu ya jumla kwa timu.
Kwanini wahusika hawakukamatwa na walionekana waziwazi wakifanya vurugu hizo? Hivi unapoitoza timu faini ya Sh. milioni 2 kwa vurugu za mashabiki wake hata kusababisha mechi kuvunjika, tuna maana gani?
Ni rahisi kwetu kusema kuwa, adhabu iliyotolewa na TFF kwa mwamuzi na timu ni sawa na kujifurahisha.
Vurugu zile zimetia doa baya katika soka letu hasa kwa kuzingatia kuwa ziliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini vinavyorusha au kusambaza taarifa zake hadi nchi jirani.
Kwa ushauri wetu, tunaiomba TFF kushirikiana kwa karibu na jeshi la polisi ili kuimarisha ulinzi kwenye viwanja vyote vitavyochezwa mashindano yanayosimamiwa na taasisi hiyo.
Bila TFF kushirikiana na vyombo vya usalama, tunaendelea kushuhudia vurugu kwenye michezo.
Ni wakati sasa wa kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya washabiki wachache wenye dhamira ya kufanya vurugu kwa kigezo cha kufikisha ujumbe wa malalamiko dhidi ya waamuzi.










