Ni kweli, hakuna haja ya kuingiza mchele kutoka nje

29Apr 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni kweli, hakuna haja ya kuingiza mchele kutoka nje

SERIKALI imepiga marufuku uingizaji wa mchele kutoka nje ya nchi kwa maelezo kuwa, uzalishaji wa mpunga unaozalishwa na wakulima nchini umekuwa ukiongezeka na kukidhi mahitaji.

Hatua hiyo ilitangazwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bungeni wakati akihitimisha mjadala wa hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2016/17.

Katika utekelezaji wa agizo hilo, Waziri Mkuu aliviagiza vyombo vya dola kuimarisha ulinzi kwenye mipaka ya nchi hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi, ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema ikiwa patatokea upungufu wa mchele nchini, serikali itaangalia uwezekano wa kuruhusu kuagiza mchele kutoka nje.

Tunaunga mkono hatua hiyo ya serikali kwa kuwa inaonekana kwa miaka kadhaa sasa wakulima wa mpunga katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakiongeza uzalishaji, hivyo kuwapo na mchele wa kutosha.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Mkuu, katika kipindi cha miaka sita iliyopita, kumekuwa na ongezeko la asilimia 14 katika uzalishaji wa mpunga nchini, hivyo kufanya kiwango cha uzalishaji kiwe kikubwa kuliko mahitaji.

Takwimu hizo za kipindi hicho zinaonyesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga kutoka tani 1,699,825 mwaka 2009/2010 hadi tani 1,936,909 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14.

Sababu nyingine ya kutokuwapo haja ya kuingiza mchele kutoka nje ni kwamba, mchele unaozalishwa nchini ni mzuri na wa kiwango cha juu kuliko wa kutoka nje.

Ziko taarifa kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza mchele kutoka nje wamekuwa wakiuchanganya na mchele unaozalishwa nchini ili uonekane ni wa kiwango cha juu. Hali hiyo ndiyo inayothibitisha kwamba mchele unaizalishwa nchini ni bora zaidi.

Ni matarajio yetu kuwa, kuanzia sasa serikali itachukua hatua kwa kotoruhusu uingizaji wa mchele nchini kutoka nje, lakini pia vyombo vya dola kutekeleza kwa dhati agizo alilolitoa Waziri Mkuu la kudhibiti uingiaji wa mchele kutoka nje kwa njia za magendo kupitia Bahari ya Hindi.

Kwa kuwa eneo la bahari hiyo lina bandari nyingi ‘bubu’ zinazotumika kuingiza nchini bidhaa za magendo kutoka nje, tunavishauri vyombo vya dola kuhakikisha kwamba vinafanya doria wakati wote, vinginevyo itakuwa vigumu kutekeleza agizo la Waziri Mkuu hivyo mchele kutoka nje kuendelea kuingizwa nchini.

Kupigwa marufuku mchele kutoka nje itakuwa neema kwa wakulima wetu wa mpunga kunufaika kwa kuwa itakuwa rahisi kwao kupata soko la uhakika na bei nzuri ya mchele wao.

Hatua hii itasaidia wakulima wetu kupata soko la uhakika na bei nzuri, jambo ambalo linawaongezea kipato na kuwahamasisha kuongeza uzalishaji zaidi.

Tunawashauri wakulima wa mpunga kuhamasika kuchangamkia fursa hiyo kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji sambamba na ubora.

Kwa upande wake, serikali itimize jukumu lake la msingi la kuwawekea mazingira mazuri hususan kuwawekea miundombinu ya uhakika ili iwe rahisi kwao kusafirisha zao hilo kwenda kwenye soko.

Suala hili halinabudi kutupatia funzo kwamba nchi yetu inazo fursa nyingi ambazo hatuzitumii. Inaonekana dhahiri kwamba tukiamua tunaweza kuzalisha mchele mwingi zaidi na bora na kuusafirisha nje kisha tukapata fedha za kigeni.