Nia njema ya rais isiwe kikwazo cha demokrasia

27Apr 2016
Bangila Balinsi
Dar es Salaam
Nipashe
Nia njema ya rais isiwe kikwazo cha demokrasia

SERIKALI ya awamu ya tano chini ya uongozi wa rais John Magufuli imekuwa na staili ya utendaji ulioleta msisimko, sababu kubwa ikiwa ni utendaji wa rais Magufuli na mawaziri wake katika kupambana na ufisadi na uzembe papo kwa papo, ikijulikana zaidi kama utumbuaji majipu.

mwanasheria mkuu wa serikali, George Masaju.

Ama kwa hakika watu wengi wamemuunga mkono rais katika harakati zake za kutaka kuondoa uoza huku yeye mwenyewe akiapa kupambana hadi afanikiwe kuwa na serikali inayowatumikia wananchi bila mizengwe na usumbufu.

Aidha, utendaji huu umeleta msisimko kwa sababu serikali ya awamu ya nne ya rais Jakaya Kikwete kwa kipindi kirefu ilionekana kuwa likizo na hivyo kuacha mwanya wa baadhi ya mambo kwenda shaghara bagara. Ufisadi na rushwa vikashamiri, wizi wa mali za umma ukawa kama umehalalishwa na uoza wa aina mbalimbali ukiachwa kuendelea.

Ni kwa sababu hiyo watu walibaki katika maisha duni zaidi badala ya kuwa na maisha bora kama Kikwete alivyokuwa ametuahidi kupitia kauli mbiu yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Katika mazingira kama hayo, akitokea kiongozi anayeonyesha kwamba yuko tayari kurudisha matumaini ya wananchi kwa kupambana na rushwa na uzembe na kusimamia utumishi wa umma unaowajibika kwa watu bila shaka ataungwa mkono na kwa hulka ya Watanzania atashabikiwa na kusifiwa kila kona.

Kwa hakika haya ndiyo yanayotokea sasa. Rais Magufuli anasifiwa kila kona na sasa Watanzania wengi wanashabikia staili yake ya utubuaji majipu. Mitaani kwa sasa msamiati au tuseme neno la msimu ni kutumbua jipu, kiasi kwamba ofisini na majumbani watu wakifanyiana jambo baya wanasema wametumbuana majipu!

Lakini kwa bahati mbaya kama waswahili wasemavyo hapana uzuri usiyo na kasoro, au kama marehemu Remmy Ongala alivyo imba barabara mrefu haikosi kona. Utawala na staili ya rais Magufuli una mambo mengi mazuri, lakini pia kuna mengine yanastaili kutazamwa na kufanyiwa kazi maana yanakwaza.

Bila shaka kama tulivyoona rais anafanya mambo kwa nia njema ya kutaka kuleta mabadiliko yatakayowezesha wananchi kupata maendeleo. Hili halina ubishi, lakini tatizo wakati mwingine njia anazozitumia zinaleta maswali kwa sababu tunadhani utaratibu unakiukwa.

Mathalani kitendo cha rais kumtumbua jipu mkurugenzi wa jiji Kabwe kimezua malalamiko miongoni mwa wanajamii kikilalamikiwa kwamba utaratibu umekiukwa. Wanaharakati wa haki za binadamu wameenda mbali zaidi na kudai kwamba rais amekiuka pia haki za binadamu kwa vile licha ya kumuumbua hadharani, lakini mtuhumiwa hakupata nafasi ya kujitetea.

Kwa vyovyote vile kuna tataizo katika njia ya utumbuaji aliyoitumia rais kwa vile limelalamikiwa na wataalamu wa mambo ya haki za binadamu na pia kuna taratibu za kikazi zimekiukwa. Kwasababu sisi wengine siyo wataalam katika fani hizo tunashauri tu kwamba wataalam wasikilizwe.

Si jambo la ajabu rais kukosea kwa sababu yeye siyo malaika. Kwa hiyo inapobainika kakosea katika kufanya jambo fulani ushauri ni kwamba akiliatambua akubali na anapoweza aombe msamaha.

Nilipekuwa katikia mtandao wa Google nikatafuta “Obama apologizes” nilipata majibu 700000! Ingawa sikuyafatilia yote, lakini kumi niliyoyapitia niliona rais wa Marekani anaomba msamaha kwa yale aliyokosea au selikali yake. Narudia; Rais wa Marekani!

Si jambo jepesi kwa rais yeyote ndani ya bara la Afrika kuomba msamaha kwa sababu tamaduni zetu huko nyuma zilitufundisha kusema na kuamini kwamba mfalme hakosei! Kwahiyo huenda kumwambia rais Magufuli kuomba msamaha alikokosea itakuwa ni kitu kigumu (asking of him too much).

Lakini basi tumuombe atambue kwamba anaweza kukosea kama binadamu na hilo likitokea basi avumilie atakapokosolewa.

Matahalani katika tukio la kumtumbua mkurugeni wa jiji Kabwe tulishangazwa na jinsi rais alivyopokea maoni ya wakosoaji wake. Vyombo vya habari vilimnukuu rais akisema: “ilimradi waliiba hadharani watatumbuliwa hadharani.”

Na kwa kuonyesha kwamba rais Magufuli alikasirishwa na wakosoaji wake akaendaelea kusema: “Kwa hiyo unaweza kuona hawa wanaowatetea nao ni majipu. Tutaanza kuwafatilia”

Kuna kauli tata nyingi rais amezitoa, lakini kwa leo tuangalie hizi mbili za hapa juu.

Kauli ya kwanza kwamba waliiba hadharani ni kauli tata kwa sababu rais ametoa hukumu. Kumtangaza mtuhumiwa kwamba ameiba kwa kadri ya utaratibu wa kisheria na kidemokrasia tuliojiwekea kupitia mgawanyo wa madaraka kakatika mihimili ya dola kikatiba ni kazi ya mahakama.

Kwa hiyo ni jambo la kushutusha sana kwa kiongozi mkuu wa nchi kaingilia kazi za muhimili mwingine wa dola bila tahadhari na kwa wazi wazi namna hii.

Pili rais akishaanzisha mtindo wa kuhukumu na kupoka kazi za mahakama kitakachofuata ni mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na kila kiongozi katika ngazi zote hadi wenyeviti wa vijiji na mitaa watafanya hivyo hivyo.

Aidha hatari kubwa zaidi inayotokana na kauli hiyo ni kwamba inazidi kuchochea tatizo kubwa tulilonalo kama nchi la watu kujichukulia sheria mkononi.

Tumeshuhudia watu wakiuawa mitaani kwa sababu watu wanatoa hukumu wenyewe bila kufuata utaratibu wa kwenda mahakamani. Sasa itakuwaje kama rais ndiye anakuwa kinara wa mambo haya.

Kinacho sikitisha zaidi ni ukweli kwamba rais amekuwa akitoa kauli kama hizi mara kwa mara. Itakumbukwa kwamba wakati akihutubia majaji na mahakimu katika maadhimisho ya siku ya sheria, rais alisema kwamba alikuwa anashangazwa na mtu kushikwa na kitu “red handed” na uchunguzi unaendelea na hukumu hazitolewi mara moja.

Bila shaka rais haoni sababu ya uchunguzi kufanyika maana ushahidi upo.Tatizo lililopo hapa ni kwamba kuna watu huwa wanabambikiziwa vitu. Kwa hiyo mtu ‘kushikwa red handed” si kigezo pekee cha kudhihirisha kwamba amekiiba au anakimiliki kama chake.

Tumesikia kesi chungu mzima ambapo wajanja hasa wa dawa za kulevya walivyo washikisha watu vifurushi kwa kuwasihi kwamba wanaenda chooni wakidai wanarudi punde, lakini wakijua vifurushi vyao ni hatari na wakatokomea. Kwa hiyo aliyekutwa na kifurushi si muhusika halisi na kwahiyo lazima uchunguzi ufanyike.

Hebu sasa tuangalie kauli ya pili kwamba wanaowatetea nao ni majipu. Utata wa kauli hii ni kwamba kwa jinsi alivyo lisema rais inaweza kutafsiriwa kuwa yeyote atakaye toa maoni tofauti na anavyo ona rais basi ashughulikiwe.

Ni kauli ambayo mtu akiitafakari inatisha. Hii ni kwasbabau kwanza aliye itoa ni kiongozi mkuu katika nchi, lakini kwa bahati mbaya zaidi ni kauli inayo ondoa uhuru wa kutoa maoni au uhuru wa kujieleza uhuru ambao upo kikatiba.

Licha ya ukweli kwamba wengi tunaunga mkono juhudi za kurudisha nchi katika mstari, lakini tutafurahi juhudi hizi zikifanyika kwa kuheshimu na kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Kama itabidi kuzibadili basi taratibu za kuzibadili zifuatwe. Lakini kubwa zaidi kuliko yote demokrasia ilindwe.