Pamoja na hilo, kwao daima huweka rekodi mpya na Jumapili iliyopita ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wakali hao wote sita kufunga katika raundi moja ya ratiba ya ligi.
Kufikia sasa, ilikuwa ni katika raundi ya 13 ya ratiba pale nyota hao wengi zaidi walipofunga wote isipokuwa mmoja tu -- Karim Benzema ambaye hakutupia katika mechi ya Real Madrid dhidi ya Eibar.
Kwa upande mwingine, siku ambayo idadi kubwa zaidi ya wakali hawakufunga ilikuwa ni watano, huku Luis Suarez pekee akifunga katika mechi za ufunguzi wa msimu na katika raundi ya sita ya ratiba.
Safu ya BBC inayoundwa na Bale, Benzema na Cristiano Ronaldo, hii ni mara yao ya saba kwa wote watatu kufunga, mara ya tatu msimu huu, wakati kwa safu ya MSN (Messi, Suarez na Neymar) hii ni mara ya pili kwa wakali wote watatu wa Barcelona kufunga baada ya kutupia mabao manne katika raundi ya 13 ya mechi dhidi ya Real Sociedad Jumapili.
Angalau mmoja wa wakali huo watatu wa Barcelona amefunga katika mechi 17 za raundi 20 za ratiba ya ligi msimu huu, wakati wakali hao wa Real Madrid kuna mechi tano ambazo walicheza bila hata mmoja wao kufunga hata bao moja.
Jumla ya magoli 10 ambayo safu hizo zimeyafunga wikiendi hii yamekuwa ni rekodi bora zaidi kwao, ikizipiku rekodi za magoli tisa waliyofunga katika raundi ya 16 na ya 19.
MSN 2015
Klabu za Barcelona na Real Madrid zimekuwa zikishindana kuweka rekodi kubwa za ufungaji wa mabao.
Barcelona walimaliza mwaka 2015 kwa staili yake wakiivunja rekodi ya Real Madrid ya kufunga magoli mengi zaidi katika mwaka mmoja wa kalenda (kuanzia Januari 1 hadi Desemba 31).
Madrid waliweka rekodi mpya ya mabao chini ya Carlo Ancelotti walipomaliza mwaka 2014 wakifunga magoli 178 katika michuano yote.
Lakini ushindi wa Barcelona wa 4-0 dhidi ya Real Betis uliwafanya miamba hao wa Catalunya kumaliza mwaka 2015 wakiwa wamefunga magoli 180.
Ili kujua mabao ya safu ipi yalikuwa na mchango mkubwa zaidi katika mafanikio yao: Lionel Messi, Neymar na Luis Suarez walifunga magoli 137 kati ya mabao 180 ya Barcelona 2015 - sawa na asilimia 76.
Kwa upande wa Madrid 2014, katika magoli yao 178, mabao 108 yalifungwa na Cristiano Ronaldo (56), Gareth Bale (24) na Karim Benzema (28), ambayo ni sawa na asilimia 61 ya mabao yao yote.
Hata hivyo, rekodi ya Madrid ya washambuliaji wao watatu kufunga magoli mengi ilikuwa katika msimu wa 2011-12 ikiundwa na Ronaldo (60), Benzema (32) na Gonzalo Higuain (26), ambao walifunga jumla ya mabao 118. Msimu huo, Madrid walitwaa ubingwa kwa kukusanya pointi 100 ambazo pia ni rekodi na kufunga jumla ya magoli 121 kwenye La Liga pekee, ambayo pia ni rekodi.
KINARA ULAYA
Kufikia sasa msimu huu, Luis Suarez ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi kuliko mwingine yeyote katika ligi kubwa tano za Ulaya.
Kufuatia 'hat-trick' yake katika ushindi wa Barca wa 6-0 dhidi ya Bilbao Jumapili, Suarez sasa amefunga jumla ya magoli 29 katika mechi 29 za michuano yote, ambayo yanachangiwa na mabao 18 katika mechi 18 za La Liga.
Orodha ya vinara wa mabao katika michuano yote Ulaya msimu huu 2015-16:
Luis Suarez (Barecelona) 29
Cristiano Ronaldo (Real Madrid) 27
Pierre Aubameyang (Borussia Dortmund) 27
Robert Lewandowski (Bayern Munich) 23
Gonzalo Higuain (Napoli) 22










