Inawezekan tangu wakati huo, idadi imeshakuwa kubwa zaidi, na takwimu zinaonyesha kuwa jijini Dar es Salaam kuna asilimia kubwa ya vijana wenye umri wa miaka 15-35 ambao hufika kwa lengo la kutafuta fursa za ajira na maboresho ya maisha yao.
Vijana hujazana mijini wakitokea maeneo mbalimbali ya vijijini ambako kwa kawaida ajira za huko ni kilimo ambacho, hata hivyo, kimekuwa kikisuasua kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa soko na madadiliko ya hali ya hewa.
Mbali na hilo, kilimo chenyewe hakipewi kipeumbele na badala yake wananchi kuendelea kutumia jembe la mkono ama plau hali ambayo inasababisha wasipate mazao ya kutosha na hivyo kuona kilimo hakifai tena. Sababu hizo na nyingine zinachangia kuwafanya vjana wakimbie vijijini kwa vile wanaona mazingira ya vijijini siyo rafiki kwao tena hasa kutokana kilimo kushindwa kuwakomboa.
Pamoja na hayo, serikali za vijiji hazitengenezi mikakati ya kuwamilikisha ardhi, ambayo ni rasilimali ya kubwa kwa shughuli za maendeleo, matokeo yake vijana wanabaki kuwa maskini na hivyo kuamua kukimbilia mijini ili kujaribu maisha mengine.
Katika maeneo ya vijijini ni wakulima wachache wanaotumia trekta huku wengi wao wakisota kwa jembe la mkono na plau, kilimo ambacho ni cha mwaka 47 na ndiyo maana unapomtaja mkulima maana yake ni mtu maskini ingawa kwa wenzetu ni tajiri.
Takwimu zinaonyesha kuwa maeneo ya vijijini umaskini bado upo kwa kiwango kikubwa kwani asilimia 84.1 ya Watanzania vijijini ni maskini ukilinganisha na asilimia 14.4 ya wale waishio mijini.
Nikumbushe tu kwamba Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ni muhimu kutekeleza kwa vitendo; hasa sura ya nne ya sera hiyo ambayo imeanisha malengo 13, ikiwamo mipango mizuri ya ajira.
Hiyo itawasaidia vijana kutatua matatizo yao ya ukosefu wa ajira na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi kwani inabainisha mahali walipo, idadi na shughuli zao na mahitaji ili kuweza kutumia takwimu hizo katika upangaji wa shughuli za maenedeleo yao.
Vijana wamekuwa wakionyesha nia ya kujiari na ndiyo maana wanafanya biashara ndogondogo ambazo kimsingi haziwezi kuwafikisha kokote.
Lakini mazingira ya vijijini yakiwa rafiki, wanaweza kurudi na kufanya shughuli nyingine zenye tija. Shughuli waanzofanya kwa sasa haziwezi kuwawezesha hata kulipa kodi ya serikali na pia wanapoteza nguvu zao bure kwa biashara ambayo kama nilivyosema haiwezi kuwafikisha kokote.
Wakiwa kwenye vikundi na kuwezeshwa vizuri kama ambavyo serikali ya Rais John Magufuli imekuwa ikisema, nina uhakika watakuwa na mchango mkubwa kwa taifa lao kuliko ilivyo sasa, ambapo wanakimbilia mijini kujishughulisha na biashara ndogondogo tu.
Kwa ujumla ni kwamba vijijini kuna changamoto nyingi za maisha na hata vijana ambao wanabaki huko, baadhi yao wamekuwa wakizurura tu huku wakiwaza maisha makubwa ambayo hawana uwezo wa kuyafikia.
Ndiyo maana nikasema kuwa serikali inapopanga mikakati ya kuwezesha vijana, basi ifanye mazingira ya vijijini yawe rafiki kwa vijana kwa kuweka miundombinu muhimu kwao ili wasipaone kama mahali pasipofaa.
Kwa wakazi wa jijini Dar es Salaam watakuwa wanaona hali halisi ilivyo, kwani ukipita maeneo mbalimbali ya jiji utakutana na vijana wakiuza pipi, karanga, maji ya chupa na vitu vingine vidogovidogo ambavyo kama nilivyosema haviwezi kuwafikisha kokote.
Inawezekana katika mazingira hayo wapo wengine ambao wamejiingiza kwenye vitendo vya uhalifu kwa lengo la kutafuta maisha baada ya kukimbilia mijini na kukuta mambo ni magumu kwao.
Kama wataachwa waendelee kuishi katika mazingira na kufanya biashara ndogondogo watakuwa na maisha gani hapo baadaye? Ni vyema wasaidiwe mapema wakiwa vijijini kabla mambo hayajawa mabaya.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







