Kama ilivyokuwa katika maeneo kama Tanga na Kyela, Jumapili iliyopita mvua kubwa ilianza kunyesha kuanzia saa 4.00 usiku na kuendelea mfululizo hadi asubuhi saa 5.00 siku iliyofuata (Jumatatu iliyopita).
Ni janga lililowaacha wakazi na simanzi ya kifo cha mkazi wa Migombani, aliyetoka nje nyumbani kwake alfajiri kukagua athari na ndipo alipoangukiwa na ukuta wa uzio wa nyumba yake akafariki.
Hali ni mbaya kutokana na nyumba na majengo mengi ama yamebomoka kabisa na miundombinu yake kusambaratika, baadhi ikielea kwenye maji hadi juzi.
Sehemu ya miundombinu iliyoathirika ni karo za vyoo zilizobomoka, kuta zilizoanguka, makaburi kutitia na viwanja vya michezo ya watoto iliyoko Kariakoo kujaa maji na barabara kuharibika, ikiwamo ya Mwanakerekwe.
Jingine ni shule zilizoharibika, zikiwamo za Bububu, Jang'ombe na Mtoni Kidato.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Tomondo, Fuoni, Mwanakerekwe, Mtoni, Kikwajuni, Jang'ombe, Kwahani na Magomeni.
Hadi sasa, waathirika wa mvua hizo waliokosa makazi wamehifadhiwa katika Shule ya Mwanakerekwe ambako wasamaria wanatoa misaada mbalimbali, ikiwamo ya vyakula na maji.
Serikali imekuwa ikitoa sababu kuu ya hali hiyo kuikumba Zanzibar, kuwa ni kutokana na mitaro ya kutiririsha maji kuziba na ujenzi holela.
TATHMINI YA SMZ
Kwanini Zanzibar, nchi ndogo iliyozungukwa na bahari, inakabiliwa na mafuriko ya kila mara bila ya kuwapo hatua za kuidhibiti?
Ni swali alilokumbana nalo Waziri anayehusika na maafa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aboud Mohammed, katika ziara fupi ya walioathiriwa na mvua.
Waziri Aboud anatoa ufafanuzi, akisema ni zao la ujenzi holela unaosababisha kuziba njia za maji taka na uchafu uliokithiri katika mazingira hayo, bila ya hatua kuchukuliwa.
Ni jibu ambalo amekuwa akilitoa kila mara, mfano mmojawapo ni mwezi Mei mwaka jana, yalipotokea mafuriko yaliyonayo watu.
Maeneo mengi yalijaa maji na njia zikawa hazipitiki, hata kuwafanya watu kuhama makazi yao, kwani nyumba walizokuwa wakiishi zilijaa maji.
Katika Shehia (Kata) ya Kianga, baadhi ya makaburi ya waumini wa Kikristo, yamedidimia kutokana na kufurika maji.
Waziri Aboud anasema taratibu za kuwahifadhi wananchi walioathirika na mvua hizo zimeshakamilishwa.
Anasema Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya SMZ, imeshaanza kupokea wananchi waliopata maafa ya mvua kwa kuwahifadhi katika Shule ya Sekondari ya Mwanakwerekwe, ambako kuna wakazi zaidi ya 400 wamehifadhiwa.
Katika tathmini yake, Waziri Aboud anasema mvua hizo zilizofikia ukubwa wa milimita 212.4v kiwango anachokitaka kuwa kikubwa sana, imeathiri nyumba zaidi ya 900 na kuua mtu mmoja.
Anasema mbali na nyumba hizo zilizoko Mkoa wa Mjini Magharibi, pia barabara imeharibika hasa ya Mwanakwerekwe ina hali mbaya na hadi sasa haipitiki.
Waziri huyo anawataka wanaoishi mabondeni na katika vyanzo vya maji wahame, kabla serikali haijaanza kuchukua hatua ya kuzibomoa, kwani hazijajengwa kisheria.
TAHADHARI
Waziri Aboud anawataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya milipuko kama vile kipindipindu, ambacho kimeibuka kwa kasi kubwa Zanzibar.
Hamad Rashid, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, anasema ni lazima kuwapo hatua madhubuti kuwahamisha watu wote wanaoishi mabondeni.
Anasema mvua kubwa iliyonyesha Jumapili iliyopita, Zanzibar imeleta athari kubwa ya kiuchumi.
Waziri Hamad,katika ukaguzi wa maeneo yaliyoathirika na kuwapa pole waathirika, anataja athari mahsusi kuwa ni wahusika kushindwa kufanya kazi za kiuchumi.
Anafafanua kuwa, kazi za kiuchumi zilikwama kutokana na wananchi kujikuta katika kuokoa mali na maisha yao.
"Kwa hali hii, hakuna aliyefungua duka au aliyeweza kufanya biashara yoyote ambayo ingeweza kumuingizia kipato," anasema.
Anataja hatari kubwa ya kuongezeka maradhi ya kipindupindu ambayo yametua visiwani, kutokana na maji taka kutuwama, huku mengine yamechanganyika na kinyesi.
"Mwenyezi Mungu atuepushe salama na maradhi haya ya mlipuko, maana kipindupindu kitawakimbiza watalii na uchumi utaathirika," anasema waziri huyo.
Anaongeza kwamba, ili kuepuka maafa ya mvua, cha muhimu ni kurejesha mpango wa ujenzi wa maghorofa ya makazi yaliyowekwa na Rais wa Kwanza wa SMZ, Abeid Amani Karume, yanayowawezesha
wananchi kuishi katika mazingira bora.
"Hali hii ya mafuriko ikiendelea, kiwango cha umaskini kitazidi. Bado kuna wajibu wa kuangalia maeneo ya ujenzi, biashara na kilimo kwa maana ya hivi sasa mabondeni na sehemu za kilimo, zimeshavamiwa na kujengwa," anasema.
BALOZI SEIF IDDI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, anasema serikali imeshaandaa viwanja kwa wananchi wanaokukumbwa na mafuriko ya mvua, huku akitoa tahadhari dhidi ya wanaoviuza na kurejea walikotoka.
Balozi Seif anasema baadhi ya wananchi wanaopewa viwanja, huamua kuviuza na baadaye wanarejea katika maeneo wanayohamishwa bila ya kuzingatia usalama wao.
Anaongeza kuwa, athari za mara kwa mara zinazoendelea kuwakumba wananchi, umefika wakati wanaopewa viwanja kuzingatia mipango miji, ili kujikinga na athari zinazoweza kuepukika.
MHANDISI ANENA
Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Mzee Juma Khamis, anasema kuna uwezekano mkubwa wa kudhibiti mafuriko kwa maji mengi kuishia baharini, lakini tatizo lililopo sasa ni kutofuatwa sheria za mipango miji.
Mhandisi huyo anaahidi kuwa,
maji yaliyotuwama katika mtaro wa Uwanja wa Mnazi Mmoja, yataondolewa mara baada ya kina chake kupungua.
Anasema maji ya bahari hivi sasa yako juu, hali inayosababisha kufungwa mlango wa kutoa maji ya mvua yaliyopo kwenye uwanja huo, kuelekezwa pwani.
Kutokana na mafuriko ya mvua, maafa ya kipindupindi nayo yameibuka kwa kasi Visiwani na kuna wagonjwa zaidi ya 400 waliolazwa katika hospitali mbalimbali zinazowapokea.
WAZIRI WA AFYA
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo, anasema kipindupindu Zanzibar kiko katika kiwango cha kutisha na idadi ya wagonjwa imeongeka.
"Kwa mwezi huu wa Aprili wagonjwa wa kipindupindu 40 wameshafariki dunia, ni lazima tuchukue tahadhari kubwa na sasa tumeshapiga marufuku uuzwaji wa vyakula vya majimaji na Mama Ntilie," anasema Kombo.
Anaongeza kwamba, maji mengi yanayotolewa na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa ajili ya matumizi ya wananchi yameathiriwa kwa kinyesi.
Anawataka wananchi kudumisha usafi na kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuosha mikono yao kwa sabuni kabla ya kula, ili wanusuru afya zao.










