Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Bunge, hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17, itasomwa Juni 9, ikitanguliwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa nchi itakayosomwa siku hiyo asubuhi. Aidha, katika mkutano huo, Serikali itawasilisha miswada mbalimbali ya sheria.
Tunatarajia kuwa serikali itakuwa imejiandaa kuwasilisha mipango mizuri ya bajeti kuanzia bajeti za wizara zitakazojadiliwa na kupitishwa kabla ya bajeti kuu ikizingatiwa kuwa hii itakuwa bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais John Magufuli. Kwamba mipango itakayowasilishwa itakuwa inaonyesha kwa uhalisia utekelezaji wa mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiahidi kuyatekeleza.
Kuna ahadi nyingi alizozitoa Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana na baada ya uchaguzi kama kuboresha huduma za afya, miundombimu, kupambana na umaskini pamoja na utoaji wa elimu bure kuanzia msingi hadi kidato cha nne.
Kikubwa zaidi ambacho Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi ni kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati kupitia viwanda. Kwa hiyo, tunatarajia kuona serikali ikitimiza ahadi hizo kupitia bajeti itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
Wakati akiwasilisha taarifa ya kiwango cha ukomo wa bajeti kwa wabunge wote kwa mwaka 2016/17 Aprili 6, mwaka huu, Waziri Mpango alisema bajeti ya mwaka ujao wa fedha itakuwa Sh. trilioni 29.53 na kwanba kati ya fedha hizo, mapato ya ndani ni Sh. trilioni 17.79 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya Sh. trilioni 15.1.
Alisema makusanyo yasiyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 2.69 huku makusanyo ya halmashauri zote yakiwa Sh. bilioni 665.41 na erikali inatarajia kupata Sh. trilioni 3.6, ikiwa ni misaada ya wahisani kwenye bajeti kuu ya serikali na miradi mbalimbali wanayoifadhili moja kwa moja.
Pia, serikali inatarajia kukopa mikopo ya masharti ya kibiashara Sh. trilioni 2.1 kutoka vyanzo vya nje na Sh. trilioni 5.37 kutoka vyanzo vya ndani.
Picha halisi ya taarifa hiyo inaonyesha kuwa Serikali italazimika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufidia pengo la mapato ya ndani ambayo ni takribani Sh. trilioni mbili.
Ili kuhakikisha kwamba lengo hilo linafikiwa, wabunge wetu wanatakiwa kutoa michango yenye tija katika mjadala wa bajeti ambayo itaisaidia serikali kufanya maamuzi sahihi, lakini pia kuhakikisha kwamba bajeti hiyo inazingatia maslahi ya wananchi wote.
Tunatarajiwa kwamba Wabunge wataweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuihoji serikali pale watakapoona imetenga fedha kidogo katika sekta zinazopaswa kutengewa fedha za kutosha.
Kwa kuwa bajeti inayo inaonyesha kuwa serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukusanya fedha za kutosha ikiwamo kuongeza vyanzo vipya, hatutarajii kusikia tena yakifanyika madudu kama uzembe katika ukusanyaji mapato, matumizi mabaya ya fedha za umma na misamaha ya hovyo ya kodi.
Ni wajibu wa Wabunge kuhakikisha kwamba haya yote wanayapigia kelele wakati wa mjadala wa bajeti na kubwa zaidi watoe michango yenye tija wakati wote wa mkutano wa bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 na wakiona kuna mambo ya msingi hayakuzingatiwa wasikubali yapitishwe.










