Akiwa kwenye ziara mikoa ya Kanda ya Ziwa, Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni, Sanaa na Wasanii, Nape Nnauye aligusia suala la viongozi wababaishaji kwenye michezo.
Pamoja na mambo mengine, Nnauye alisema itakuwa ndoto kwa sekta ya michezo kupiga hatua kama vyama vya michezo na klabu zitaendelea kuongozwa na viongozi wababaishaji.
Alisema viongozi wababaishaji wenye dhamira ya kujishibisha na siyo kuongoza ka manufaa ya wananchi, ndiyo walioifikisha sekta ya michezo mahali ilipo sasa.
Ni kweli, viongozi wengi kwenye vyama vya michezo na klabu ni wababaisha na wasio na malengo wala ubunifu wa kutafuta maendeleo.
Viongozi wa aina hii ndiyo hao ambao wamekuwa kiini cha migogoro kwenye vyama na klabu na hii yote ni kwa sababu ya kuongoza kwa kuwinda masilahi binafsi.
Ni viongozi haohao wababaishaji ambao leo wamekuwa mstari wa mbele kuandaa katiba mbovu za kutetea masilahi yao.
Wamekuwa wakitumia muda mwingi kujilinda kwa kuvuruga katiba ili waendelee kukaa madarakani na kutimiza kiu yao ya kusaka utajiri kwa mwamvuli wa vyama.
Tunashukuru jambo hili serikali imeliona na kutoa onyo. Kama wapenda michezo wenye nia ya kuona taifa linasonga mbele, lazima tuhakikishe tunaongozwa na viongozi wenye moyo wa kuleta maendeleo.
Ingawa Waziri amekemea viongozi wababaishaji kwenye klabu, lakini bado ukweli unabaki palepale kuwa, viongozi wa aina hiyo huwekwa na wananchi wenyewe.
Utamaduni wa kuchaguana kwa kigezo cha urafiki, undugu, uswahiba na mambo mengine, ndiyo chanzo cha kuwa na viongozi wababaishaji.
Tunarudia tena, kama wapenda michezo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunajenga utamaduni wa kuchagua viongozi wenye sifa za kuongoza kwa maendeleo ya nchi.
Kuendelea kubebana kwa kuchagua viongozi kwa kigezo cha kujuana, maana yake tunajiandaa kutengeneza kizazi cha viongozi wababaisha.
Tuungane na kauli ya serikali kukemea utitiri wa viongozi wababaisha kwenye vyama vya michezo ili tuweze kufikia malengo ya kupita hatua za maendeleo katika sekta ya michezo.










