Bunge limsaidie Rais Vita Kuu ya ufisadi

17Apr 2016
Mhariri
Dar
Nipashe Jumapili
Bunge limsaidie Rais Vita Kuu ya ufisadi

Katika hali inayoonyesha kugwaya kwa mhimili mmoja wa dola katika Vita Kuu ya Kwanza dhidi ya ufisadi nchini, Bunge juzi lilitoa taarifa inayopingana na mkakati wa utekelezaji wa moja ya vyombo vyake vya utendaji - Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly mapema mwezi huu aliagiza Jeshi la Polisi kuwasilishwa mbele yake mkataba kati yake na Kampuni ya Lugumi Enterprises kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS).

Mkataba wa mradi huu, ambao ni lazima tuseme wazi mapema, Nipashe, kwamba hakuna ushahidi mpaka sasa kuwa ni wa kifisadi hata hivyo, ni wa ufungaji wa mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108 wenye thamani ya Sh. bilioni 37.

Lakini, inasemekana, ni vituo 14 tu ndivyo vina mashine hizo mpaka sasa, wakati kampuni hiyo ilishalipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote kinyume na taratibu za manunuzi ya umma, hali iliyoilazimu PAC kuhitaji kupatiwa mkataba huo ili kuupitia.

Kati ya vituo 14 hivyo vilivyofungwa mashine hizo za kieleketoriniki, imedaiwa pia kuwa ni mashine za vituo nane tu ndizo zinafanya kazi.

Bahati nzuri, kamati hiyo ya Bunge haikukurupuka kudai mkataba baina ya Polisi na Lugumi kwani ilifanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) katika ripoti yake ya hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Tumeshasema, Nipashe, kwamba hakuna ushahidi mpaka sasa kuwa mkataba wa Lugumi ni wa kifisadi hata hivyo.
Lakini, tunaona, Nipashe, wingi wa fedha za mkataba, fununu za utekelezaji mbovu wa mkataba wenyewe na ukweli kuwa 'jicho la tatu' la serikali, ofisi ya CAG, ndilo lililoibua malalamiko hayo, Bunge linapaswa kufuatilia jambo hili mpaka mwisho bila woga wa aina yoyote.

Hivyo tuchukue fursa hii, kwanza, kumsifu Mwenyekiti wa PAC Hilalaly kwa kuvalia njuga ufuatiliaji wa mkataba huo licha ya kuwa yeye ni Mbunge kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinaunda serikali iliyo madarakani chini ya Rais John Magufuli.

Tunafahamu, Nipashe, ni kwa nini Hilaly, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu walikaribia kufanikisha upatikanaji wa mkataba huo kabla ya kauli ya juzi ya ofisi ya Bunge.

Tunafahamu kwamba pande tatu hizo zimeona umuhimu wa kupekuliwa kwa mkataba wa Lugumi ili kujiridhisha hakuna sheria na kanuni za matumizi ya serikali ambavyo vilikiukwa, ikiwa ni kuunga mkono Vita Kuu ya Kwanza dhidi ya ufisadi ambayo ilianzishwa na Rais pindi alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana.

Ambacho hatufahamu, Nipashe, ni nia ya Ofisi ya Bunge kutangaza kuwa Hilaly hajaomba mkataba wa Lugumi tena katika kipindi ambacho limetoka kusifiwa na Rais kwa kubana matumizi kwa kiwango cha Sh. Bilioni 6 ambazo zimeelekezwa kwenye kuchonga madawati nchi nzima.

Kama kuna ufisadi kwenye mkataba wa Lugumi, kwa mfano, Sh. Bilioni 37 zingechonga madawati mangapi?