TPDC: TRL, Bandari zitarajie neema kutoka bomba la mafuta

15Apr 2016
Salome Kitomari
Dar
Nipashe
TPDC: TRL, Bandari zitarajie neema kutoka bomba la mafuta

TANZANIA inatarajia kunufaika na ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Kaskazini mwa Uganda hadi Bandari ya Tanga, huku wafanyabiashara na wadau wengine wakijipanga kudaka fursa zilizopo.

MACHIMBO ya mafuta mkoani Bunyoro nchini Uganda, katika eneo la Ziwa Albert. (PICHA NA MTANDAO).

Hatua hiyo ya wafanyabiashara, inaendana sana na utekelezaji wa wito ambao mtaalamu wa kimataifa katika fani ya uchumi, aliyewahi kufika nchini kwa mwaliko wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuwasilisha mada katika ukumbi wa BoT, akieleza namna ya kunufaika na mradi wa gesi Songosongo.

Kikubwa alichohimiza ni kwamba Watanzania wajitahidi kujinufaisha na fursa zitokanazo na gesi na si lazima iendane moja kwa moja na gesi inayozalishwa, ikizingatiwa kikwazo cha mtaji.

Kimsingi, mradi huo wa kusafirisha mafuta kutoka Hoima hadi Tanga, baadaye unatarajiwa kuchukuliwa na meli kwenda katika masoko ya kimataifa, ikiwemo nchi za Ulaya.

Orodha ya kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda inajumuisha Tullow kutoka Ireland, Total ya Ufaransa na CNOC ya China.

Mafuta yamegunduliwa katika wilaya ya Buliisa, mkoa wa Bunyoro, iliyoko kando ya Ziwa Albert tangu mwaka 2006.

Pia, kuna kampuni nyingi zimeingia mkataba na serikali ya Uganda kwa ajili ya uchimbaji huo wa mafuta.

Kabla ya hata kuanza kusafirishwa mafuta hayo, wananchi wa Uganda wamenufaika kwa kupata ajira 15,000za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Tullow ambayo ni kampuni kutoka Ireland inaelezwa kuwa na shughuli nyingine mbali na uchimbaji za kununua mazao ya wakulima.

Pia, kuna huduma mbalimbali za kijamii zinazofanywa na kampuni hiyo ni ya
ujenzi wa hospitali ya kisasa katika wilaya ya Buliisa, soko la kisasa wilaya ya Hoima na wananchi kuwa na uhakika wa soko wa mazao yao ni moja ni baadhi ya manufaa.

TPDC NA BOMBA LA MAFUTA

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio, anasema eneo husika ambako bomba la mafuta litafikishwa ni tambarare, hivyo kuendana na mahitaji ya uwekaji bomba la mafuta.

Anasema atahri za mlima ni kwamba, unaleta changamoto ya gharama za ziada katika ujenzi.

“Tanga iko tambarare kwa kiasi kikubwa, kuna milima midogo midogo. Pia, bandari yake ina mazingira mazuri, kwani ili kuweza kuwa na uzalishaji kwa mwaka mzima, ni lazima meli ije kuchukua mafuta kwa mwaka mzima,” anasema.

Anafafanua wasifu wa Bandari ya Tanga, kwamba ina kingo za asili ambazo ni adimu sana kwa bandari nyingi duniani.

Mkurgenzi huyo TPDC anafafanua umuhimu wa kingo hizo kuwa ni katika baadhi ya vipindi baharini kunakuwepo upepo mkali na meli zitashindwa kupakia bandarini.

Anasema manufaa ya bandari hiyo ni kwamba, kuna kisiwa cha Pemba kwa upande wa Mashariki, ambacho kinazuia mawimbi kutoka bahari kuu, hivyo inaipa uwezo bandari ya Tanga kupakia mafuta mwaka mzima.

Mkurugenzi huyo anasema, bomba hilo la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga litakuwa na urefu wa kilomita 1,444 na katika umbali huo, kilomita 1,144 ambazo ni asilimia 79 zitakuwa upande wa Tanzania na kilomita 300 zitakuwa upande wa Kenya.

Mataragio anabainisha kuwa, wakati wa ujenzi wa bomba hilo, kutakuwapo na fursa nyingi zitakazojitokeza kukiwepo na ajira kati ya 10,000 na 15,000 kwa kipindi cha ujenzi.

Anasema katika uendeshaji wa bomba lenyewe litazalisha ajira kati ya 1,000 na 2,000 na kwamba Bandari itakuwa na shughuli nyingi zinazoendelea, ambazo nazo zina viashiria vya uchumi.

Faida nyingine ni kupatikana kwa mkuza mkubwa ambao utatumika kwa siku za baadaye kwa ajili ya kusafirisha gesi kwenda mikoa ya Kaskazini na nchi jirani.

“Hatua zilizofikiwa hadi sasa ni kutia saini mkataba wa maelewano kati ya Tanzania na Uganda, Oktoba 12, mwaka jana, ambao ni mwangozo utakaotumika kutekeleza mradi. Machi Mosi mwaka huu marais walikutana Arusha na kukubaliana kujenga bomba hilo,” anasema.

Aidha, anabainisha kuwa wanakutana na kampuni za mafuta na wataalamu kutoka nchini za Uganda, ili kupanga mikakati na kutengeza ripoti itakayowalishwa kwa Mawaziri wa Nishati na Madini wa nchi husika.

WATANZANIA WAATARAJIE NINI?

Anasema ujenzi wa bomba hilo utaharakisha utafutaji wa mafuta nchini, hasa maeneo ya Kaskazini ambako korido ya Kaskazini, ambako utafiti haujafanyika kwa kutosha kwa vile hakuna miundombinu ifaayo.

“Uwepo wa bomba utachochea uwekezaji kwani kampuni nyingi zitakuja kufanya utafiti na iwapo yatapatikana itakuwa rahisi kuingiza kwenye bomba lililopo na kuendelea,” anabainisha na kuongeza:

“Ni sawa na una barabara ukilima utasafirisha mazao kwa kuwa una barabara. Uzuri uliopo tayari kuna kiwango cha mafuta kimeshaonekana, lakini tutashindwa kusafirisha kwa kuwa hatuna miundombinu.

“Kampuni zilisita kwa kuwa eneo la Ziwa Tanganyika liko porini. Ukichimba gharama, zitakuwa kubwa na mafuta ni kidogo,” anasema Dk. Mtaragio.

Anasema uwepo wa bomba, utaongeza idadi ya wawekezaji wanaokuja nchini, utaimarisha matumizi ya bandari ya Tanga na kuongeza mapato ya serikali.

“Bandari itaboreshwa na itawezesha meli nyingi kuweka nanga. Ujenzi wa barabara takribani kilomita 200 na nyingine zitaboreshwa kwa kiwango cha changarawe kilomita 150.

Pia reli itaboreshwa na kutoa fursa kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), kutumika kusafirisha vifaa mbalimbali wakati wa ujenzi.

Anasema matarajio ni mabomba 123 yatakayosafirishwa na ni fursa mpya kwa TRC.

Mkurugenzi huyo anasema miundombinu itakuwa inamilikiwa na TPDC na moja ya majukumu yake ni kushiriki katika uwekezaji wote wa miundombinu katika mkono wa chini, hivyo wao ni wasimamizi wakubwa.

KWANINI TANZANIA?

Anasema awali kulikuwa na makubaliano ya nchi za Kenya na Uganda kupitisha mradi huo Kenya kutoka Hoima hadi bandari ya Lamu, lakini kwa sababu mbalimbali Uganda waliamua kupitisha bandari ya Tanga.

Anabainisha kuwa ingawa umbali kutoka Uganda hadi bandari za Kenya na Uganda ni kilomita chache kuliko Tanga lakini zipo sababu zilizofanya bomba hilo kufikishwa Tanga.

Dk. Mtaragio anataja mojawapo ni gharama ndogo za ujenzi kwa bandari ya Tanga kuwa na kingo za asili na hivyo kuweza kusafirisha mafuta mwaka mzima.

Pia, ujenzi wa bomba hilo hadi bandari ya Tanga haupiti sehemu yenye makazi ya watu wengi hivyo kupunguza gharama, huku bomba likipita maeneo mengi ya tambarare bila miinuko inayofanya kuongeza gharama za kupampu.

SERIKALI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, anasema serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mradi huo na tayari imekutana na wafanyabiashara na kuwapa elimu ya fursa zilizopo katika mradi huo na jinsi wanavyoweza kunufaika nazo.

Profesa Ntalikwa anasema mradi huo unatarajia kuanza mwakani na utamalizika baada ya miezi 36, ukigharimu Dola za Marekani bilioni nne.

Anabainisha kuwa Tanzania ina uzoefu wa ujenzi wa mabomba kama hayo, kwa kuwa ilishajenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ina kina kirefu cha bahari inayoweza kuchukua meli mbalimbali kuchukua mafuta.

Mbali na hilo anataja kivutio kingine cha Bandari ya Tanga ni usalama.

Anasema Tanzania haikuwa inashirikishwa au kuwekwa kwenye kamati maalumu ya Afrika Mashariki ya ufuatiliaji wa miradi ya aina hiyo iliyoundwa Nairobi, Kenya kwa ajili ya kuchukua takwimu kwa kuanzia bandari ya Lamu na Mombasa nchini Kenya na baadaye Tanga.

“Tumedhamiria kupeleka ombi letu kwa serikali ya Uganda kwenye utafutaji wa takwimu hatutashiriki,”anasema Profesa Ntalikwa.

“Ikiwa serikali ya Uganda na wataalamu wake wakitaka kutafuta takwimu, watashirikiana na wataalamu wetu kutafuta na siyo hiyo kamati, lengo letu ni kuupata mradi na kuutekeleza kwa haraka,” anasema.

Kuhusu uwezekano wa kuingia kwenye mvutano na serikali ya Kenya baada ya Tanzania kukosa bomba hilo, Katibu Mkuu anasema ni lazima ushirikiano uendelee kuwapo na hatua za kidiplomasia zitatumika kutatua mgogoro, iwapo utajitokeza.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC), Dk. Gideon Kaunda, anasema wafanyabiashara wamejipanga kikamilifu kunufaika na fursa zilizopo, ikiwamo kushindana katika zabuni zitakazotangazwa

HUDUMA ZA JAMII UGANDA

Wakati Watanzania wakifungua macho kufuatilia mradi huo wa ujenzi wa bomba la jipya la gesi, kwa Waganda sura ya neema imeshaanza ko bayana zaidi.

Jamii zimeshanufaika katika namna nyingi kuanzia maisha ya kawaida, hadi kiuchumi.

Katika wilaya ya Hoima, tayari wananchi wameanza kunufaika na huduma za jamii ikiwamo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha cha lami na soko kubwa litakalobeba wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Mafuta yaligunduliwa katika visima 14 wilayani Buliisa mkoa wa Bunyoro, ndani ya Ziwa Albert tangu mwaka 2006. Hadi sasa uchimbaji umekamilika na kuna visima zaidi ya 10.

Kampuni ya Tullow imetoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000.
Wilaya ya Buliisa ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya wafugaji na wavuvi, kwa sababu ya kupakana na Ziwa Albert, kampuni ya Tullow imejenga hospitali ya kisasa, ikiwa na vifaa tiba vyenye ubora wa juu.

Kampuni ya Trade Links imekuwa ikiendesha kampeni ya kuwaelimisha wakulima, namna ya kuzalisha mazao ubora ili kuuza kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, kabla soko hilo halijatekwa na wageni na watumishi wa kampuni hizo walikuwa wanaagiza chakula kutoka nje.

Mwaka 2014, Nipashe ilitembelea eneo hilo na kukutana na Mratibu wa Chama cha Wakulima wa Hoima, Moses Byenkya, anayeeleza kwamba vikundi 500 vyenye wakulima 7049, walipewa elimu na sasa wanaendesha kilimo kwa mbinu za kisasa na kukiuza kwa wawekezaji hao.

Mwenyekiti wa Manispaa ya Hoima, Emmanuel Banya, anasema kugundulika mafuta katika eneo lao kumesaidia kukua kwa mji huo, ikiwa pamoja na wawekezaji kupiga hodi kwenye wilaya hiyo na kujenga majengo ya kisasa.

"Manispaa yetu ni kongwe na kubwa yenye kilomita za mraba 1,000, lakini iko nyuma kimaendeleo. Moja ya manufaa ya kugundulika mafuta, ni ujenzi wa soko kubwa la kisasa, reli itakayounganisha manispaa na eneo la uzalishaji mafuta, nyumba za kisasa na mapato ya mwaka yameongezeka kutoka Sh. bilioni moja hadi Sh. bilioni tatu," anasema.

Mwandisi wa makala hii alishatembelea machimbo ya mafuta inakotoka bomba hilo nchini Uganda.